Beki mpya Simba afunguka, alichokisema balaa

SIKU moja baada ya kutambulishwa na Simba, beki Vedastus Masinde amesema anafurahia kujiunga na timu aliyoitaja kuwa ni bora kwake na anakwenda kufanya kazi na wachezaji wengi ambao anafahamiana nao akimtaja Wilson Nangu.

Masinde amejiunga na Simba akiwa mchezaji huru baada ya kumaliza mkataba na TMA inayocheza Ligi ya Championship.

Akizungumza na Mwanaspoti, alisema ni fursa kubwa aliyoipata na kazi yake ni kwenda kuipambania Simba na anafuraha kuungana na nyota wengi ambao anafahamiana nao kutokana na kucheza pamoja.

“Pacha yetu na Nangu inaenda kufanya kazi Simba, ukiondoa beki huyo ambaye tulikuwa pamoja TMA pia nimefanya kazi na Abdulrazack Hamza kwenye kikosi cha timu ya taifa, hivyo naamini nitafanya kazi na watu ninaofahamiana nao kwenye eneo langu isipokuwa beki wa kigeni. “Kilichobaki ni kuomba uzima tu na nafasi. Nipo tayari kuipambania nembo ya Simba na naamini nipo sehemu salama, naomba kuaminiwa ili nifanye kazi yangu juhudi zangu nitazionyesha kwenye uwanja wa mazoezi.”

Alisema amejiunga na timu ambayo ina presha ya matokeo akiwa na kazi kubwa ya kusaka nafasi kikosi cha kwanza, hivyo atahakikisha anafuata maelekezo ili kuweza kuingia kwenye mfumo haraka.

“Unajua Simba imepoteza mataji misimu minne mfululizo haitarajii kurudia makosa naamini msimu huu hautakuwa rahisi na ili kupata namba kikosi cha kwanza ni kuhakikisha kila mchezaji anafanya kazi yake kwa kujituma ili aweze kuipambania nembo ya timu hiyo,” alisema.

Usajili wa Masinde unaongeza ushindani kwenye safu ya ulinzi ambayo itabebwa na mabeki Hamza, Chamou Karaboue wote walikuwa sehemu ya kikosi msimu uliopita na kuongezewa Nangu na Masinde.