ADC yaahidi mapinduzi ya kilimo, mikopo, miundombinu na kodi

Simiyu. Mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanznaoa kupitia Chama cha Alliance for Democratic Change (ADC), Wilson Mulumbe, ameahidi kujenga kiwanda cha vifaa tiba mkoani Simiyu kwa lengo la kuongeza thamani ya zao la pamba, endapo kitashinda katika uchaguzi mkuu ujao.

Akizungumza leo, Jumatano, Septemba 10, 2025, mjini Bariadi, Mulumbe amesema lengo la kiwanda hicho ni kuhakikisha mkulima wa pamba ananufaika moja kwa moja na jasho lake, tofauti na sasa ambapo faida kubwa ya zao hilo huishia katika viwanda vya nje ya nchi.

“Kwa sasa wakulima wa pamba hawapati bei nzuri kwa sababu hakuna viwanda vya kuongeza thamani ya zao hilo nchini. Hii inapelekea wanunuzi wa nje kupanga bei, hali inayomnyima mkulima sauti na uwezo wa kujinufaisha,” amesema Mulumbe.

Ameeleza kuwa mradi huo utasaidia pia kuongeza ajira kwa vijana wa Mkoa wa Simiyu, kukuza uchumi wa ndani, na kupunguza utegemezi wa bidhaa za afya kutoka nje ya nchi.

Mulumbe ameongeza kuwa chama chake kinaamini katika uchumi wa viwanda vinavyomgusa mwananchi wa kawaida moja kwa moja, na kwamba ADC ipo tayari kulipa kipaumbele zao la pamba, kwa sababu ni miongoni mwa mazao ya kimkakati yenye mchango mkubwa katika pato la Taifa.

Baadhi ya wanachama na viongozi wa chama cha ADC mkoani Simiyu wakimsikiliza Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia chama hicho,Wilson Elias Mulumbe wakati akizungumza na waandishi wa habari mkoani Simiyu. Picha na Samwel Mwanga



Kwa upande wake, mgombea mwenza, Shoka Hamis Juma, amesema Serikali ya chama hicho itaweka mfumo wa utoaji mikopo kwa wananchi wote bila ubaguzi na bila riba, ili kuwaepusha kuingia kwenye mikopo ya ‘kausha damu’.

“Hatutabagua makundi maalumu kama ilivyo sasa. Kila mwananchi atapata mkopo bila riba, na muda wa kurejesha utakuwa mrefu, ili kila mmoja aweze kujiendesha na kujiendeleza,” amesema Juma.

Aidha, amebainisha kuwa Serikali ya ADC itatoa ruzuku kwa wavuvi ili wafanye shughuli zao kwa ufanisi na kuchangia kukuza uchumi wa taifa.

“Tuna bahari na maziwa makubwa, lazima tuyatumie kuhakikisha wananchi wanapata kitoweo cha uhakika, na taifa linaongeza kipato,” amesisitiza.

Akizungumzia miundombinu, Juma amesema changamoto ya barabara zinazounganisha wilaya bado ni kubwa, hivyo chama hicho kimepanga kujenga barabara zitakazounganisha kata kwa kata kote nchini.

Kuhusu kodi, alisema kila raia mwenye umri wa kuanzia miaka 18 atalipa kodi ili kuongeza mapato ya Serikali kwa ajili ya kutoa huduma bure kwa wananchi.

“Tutasitisha kodi ambazo ni mzigo kwa wananchi na kuondoa utitiri wa kodi usio na tija,” amesema.

Mtoro Fanuel, mkazi wa mjini Bariadi, amesema kwa jinsi kampeni zinavyoendelea mwaka huu, anaziona hazina msisimko. Pia, wagombea urais wengi wameshindwa kujikita kwenye matatizo yanayowakabili wananchi.

“Ukilinganisha na chaguzi mbili zilizopita, wagombea wengi wa urais wameshindwa kujikita na matatizo ambayo yanawakabili wananchi, kama vile wakulima kutopata bei nzuri ya mazao yao, na wamekuwa wakiongelea masuala mepesi mepesi tu,” amedai.