Arusha warudisha hadhi ya marathoni

MKOA wa Arusha umeanza mkakati wa kurudisha hadhi ya riadha baada ya kutangaza kuwa mbio za Tanfoam zifanyika zikitumia umbali wa kilomita 42.

Arusha ndiyo waanzilishi wa mbio ndefu za kilomita 42 na awali zilijulikana kuwa Mount Meru Marathon ambazo zilikuwa za kwanza kuwa na hadhi ya kimataifa kwa kuleta wanariadha nyota sehemu mbalimbali.

Mount Meru Marathon ilipoteza  hadhi na mvuto baada ya kuasisiwa kwa Kilimanjaro Marathon ya Kilimanjaro.

Kwa miaka mitatu iliyopita Tanfoam Marathon ilikuwa ikiishia kilomita 21 ikiwa pia na tano na 10.

“Mwaka huu tutakuwa na marathoni kamili ya kilomita 42 kama mbio kuu ya mchezo,” alisema Glorious Temu ambaye ndiye mwandaaaji mkuu.

Kwa mujibu wa Temu kuna zaidi ya wanariadha 1300 ambao wamejiorodhesha kutoka ndani na nje ya Tanzania.

Marathoni kamili ya Tanfoam itafanyika Desemba 7, mwaka huu na itakuwa sehemu ya mandalizi ya sherehe za Uhuru, Desemba 9.

Alisema mbio ndefu zitaanzia katika viwanja vya General Tyres katika vilima vya Temi, Arusha ambako zaidi ya wanariadha 1300 watakusanyika.

Licha ya mbio za kilomita 42 kuwa ndizo kiini cha mashindano, Glorious Temu alisema vilevile kutakuwepo na mbio za kilomita tano kwa watoto, 10 na 21.