Dk Nchimbi aeleza sababu CCM kuomba ichaguliwe tena

Katavi. Mgombea mwenza wa urais wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Emmanuel Nchimbi amesema mafanikio makubwa yaliyopatikana miaka mitano iliyopita, yanakifanya chama hicho kutoka kifua mbele kuomba tena ridhaa ya Watanzania kuwaongoza.

Amesema maeneo mbalimbali nchini kuna miradi mingi imekamilika au inaendelea kutekelezwa mathalani ya afya, elimu, barabara, kilimo, ufugaji, uvuvi na maji inayochochea uchumi wa wananchi.

Dk Nchimbi amesema hayo leo Jumatano, Septemba 10, 2025 katika mikutano ya kampeni Jimbo la Nsimbo na Jimbo la Katavi, mkoa wa Katavi.

Mikutano hiyo miwili, imehitimisha kampeni za Dk Nchimbi mkoani humo aliyoanza jana Jumanne, kuzisaka kura za mgombea urais, Samia Suluhu Hassan, wabunge na madini wa CCM katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Jumatano ya Oktoba 29, 2025.

Tayari Dk Nchimbi amekwishafanya mikutano kama hiyo mikoa ya Mwanza, Mara, Simiyu, Shinyanga, Geita, Kagera, Rukwa na Katavi. Mikoa inayofuata ni kaskazini ya Arusha, Kilimanjaro na Tanga.

Kwa upande wake, Samia amechanja mbuga mikoa ya Morogoro, Dodoma, Songwe, Njombe, Mbeya, Iringa, Singida na sasa yupo mkoani Tabora.

Turufu ambayo Samia na Dk Nchimbi wanaitumia kwenye kampeni hizo ni utekelezaji wa ilani waliyoinadi mwaka 2020 wakieleza imetatua matatizo ya wananchi na kuomba tena ridhaa ili waendelee walipoishia kwa kasi.

Akiwa Nsimbo aliposimama kuwasalimia, Dk Nchimbi amesema shule za msingi na sekondari zimejengwa na wanatarajia kijenga zingine. Vituo vya afya na zahanati,”hapa Nsimbo tumejenga na tunakwenda kujenga zingine.”

“Ilani yetu tumeitekeleza kwa kiwango kikubwa chini ya Rais Samia.  Kila eneo kuna miradi imeisha na ninyi wananchi mnapata huduma. Sasa kasi ya utekelezaji mkitupa ridhaa, mama Samia akasema itakuwa kubwa zaidi,” amesema Dk Nchimbi.

Kuhusu kilimo, Dk Nchimbi amesema Serikali imekuwa ikiongeza bajeti ya ruzuku ya mbolea na mbegu kila mwaka. Tutaangalia uwezekano wa kujenga kongani ya viwanda ili wakulima baada ya kulima wasihangaike kupata soko.

Mgombea mwenza huyo amesema, Serikali imewekeza nguvu katika uvuvi ili wavuvi wasitegemee uvuvi tu bali wategemee vizimba na mabwawa na hilo linakwenda kufanyika ikiwa wananchi watakichagua tena chama hicho.

Dk Nchimbi amesema miaka mitano ijayo watahakikisha inaongeza upatikanaji wa dawa, chanjo za mifugo na upatikanaji wa minada ya kuuzia bidhaa.”

Lengo tunataka mwananchi wetu kwa kila anachokifanya, Serikali imtengenezee mazingira wezeshi.”

Akihutubia mkutano, uwanja wa mpira wa Inyonga, Jimbo la Katavi, Dk Nchimbi amewaomba wananchi wa Katavi kuendelea kumwamini Samia ambaye amefanya kazi kubwa miaka minne iliyopita.

Amesema miaka mitano iliyopita, Serikali ya CCM imejenga hospitali ya wilaya, zahanati na vituo vya afya. Madarasa yameongezeka kutoka 135 hadi 322, shule za sekondari zimeongezeka kutoka 96 hadi 115. Walimu walikuwa 147 sasa wapo 286.

Dk Nchimbi amesema Sh10 bilioni zimetumika kugharamia miradi 12 ya maji ikiwamo kuchimba visima vikubwa na kufikia 61 kutoka tisa.

“Vitongoji vilivyokuwa na umeme vilikuwa 34 lakini sasa viko 68. Mbolea ya ruzuku ilikuwa tani 240 sasa imefikia tani 2,122,” amesema Dk Nchimbi.

Awali, akimkaribisha Dk Nchimbi kuzungumza, Mwenyekiti wa CCM, Mkoa wa Katavi, Idd Kimanta amesema mkoa huo ulipokea Sh1.3 trilioni zilizopelekwa kwenye miradi iliyokamilika na mingine inaendelea ikiwamo ya maji.

Kimanta amesema kazi kubwa,”inayotukabili ni kusema asante mama Samia na asante hiyo tutaisema Oktoba 29 na sisi wana Inyonga lazima tuwe sehemu ya ushindi huo.”

Mkuu huyo wa zamani wa Arusha amesema:”Katavi tumeitika, Katavi tumeikubali CCM na Katavi haina shida. Tunakuombea kheri Dk Emmanuel Nchimbi. Mungu akusimamie na kukuongoza katika safari hii ya kutafuta ushindi wa CCM.”