Gor Mahia katikati ya mtego wa Simba

WAKATI tamasha la kilele la Simba Day likihitimishwa leo, kikosi cha Gor Mahia ya Kenya kiko katika mtego wakati kikiwa nyuma kwa bao 1-0 dhidi ya ‘Wekundu hao wa Msimbazi’.

Iko hivi, mara ya mwisho kwa Simba kupoteza mechi ya Simba Day dhidi ya timu kutoka Kenya ilikuwa mwaka 2012, jambo linalosubiriwa kuona kama Gor Mahia itavunja uteja au kikosi hicho cha Msimbazi kitaendeleza ubabe wake leo kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.

Katika pambano hilo la mwaka 2012, Simba ilichapwa mabao 3-1 na Nairobi City Stars ya Kenya, ambapo kikosi hicho kilikuwa chini ya Kocha Mkuu, Mserbia Milovan Cirkovic.

Mwaka huo, Simba ilikuwa ya kwanza kupata bao kupitia kwa Mzambia Felix Sunzu katika dakika ya 15, kisha wageni kuchomoa kupitia kwa Duncan Owiti katika dakika ya 57, Bruno Okullu dakika ya 69 na Boniphace Onyango dakika ya 79.

Hata hivyo, pambano la mwisho la Simba Day dhidi ya timu kutoka Kenya, lilipigwa mwaka 2016, ambapo AFC Leopards ilikubali kichapo cha mabao 4-0.

Ibrahim Ajibu ambaye kwa sasa yupo KMC ndiye aliyekuwa shujaa wa mechi hiyo kwa kufunga mabao mawili, huku straika raia wa Burundi aliyekuwa amejiunga na timu hiyo akitokea Vital’O, Laudit Mavugo alifunga moja.

Bao lingine la kikosi hicho lilifungwa na winga, Shiza Kichuya aliyekuwa akiicheza timu hiyo kwa mara ya kwanza akitokea timu ya Mtibwa Sugar.

Katika pambano linaloendelea sasa Kwa Mkapa katika Tamasha la 17 la Simba Day, Wekundu wa Msimbazi wanaongoza kwa bao 1-0 lililofungwa kichwa na beki wa kati Abdulrazack Hamza.