BAADA ya Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ kuondoka Simba, timu aliyoitumikia kwa takribani miaka kumi, sasa kuelekea msimu wa 2025-2026, mikoba yake ipo kwa David Kameta ‘Duchu’.
Tshabalala ambaye alikuwa nahodha wa Simba, msimu ujao atakuwa na kikosi cha Yanga alichojiunga nacho akiwa mchezaji huru.
Mikoba aliyokabidhiwa Duchu si unahodha, bali ni jezi namba 15 aliyokuwa akiivaa Tshabalala ndani ya Simba kwa muda mrefu aliokuwa akiitumikia timu hiyo.
Duchu anayecheza beki wa kulia, msimu uliopita alikuwa akivaa jezi namba 3 ambayo naye amemuachia mshambuliaji mpya wa Simba, Jonathan Sowah.
Sowah alikuwa anaivaa jezi yenye namba hiyo tangu akiwa Singida Black Stars aliyojiunga nayo dirisha dogo la usajili msimu uliopita huku akifanikiwa kufunga mabao 13 kwenye Ligi Kuu Bara akicheza mechi 14.
Hayo yote yamebainika wakati wa utambulisho wa kikosi cha Simba uliofanyika leo Septemba 10, 2025 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam katika kilele cha Tamasha la Simba Day.
Wakati Duchu akirithi jezi ya Tshabalala, jezi iliyokuwa ikivaliwa na kiungo na nahodha msaidizi wa kikosi hicho, Fabrice Ngoma haina mtu.
Ngoma ambaye ameondoka Simba baada ya mkataba wake kumalizika mwisho wa msimu uliopita, alikuwa akivaa jezi namba sita.
Simba imetambulisha kikosi chake kwa msimu wa 2025-2026 kikiwa na nyota 31, wakiwemo 13 wapya ambao ni Yakoub Suleiman, Naby Camara, Antony Mligo, Rushine De Reuck, Wilson Nangu, Vedastus Masinde, Alassane Kante, Morice Abraham, Mohamed Bajaber, Hussein Daud Semfuko, Jonathan Sowah, Seleman Mwalimu na Neo Maema.
Pia katika hao 31, wapo watatu waliopandishwa timu ya wakubwa kutoka Simba U20 ambao ni Alexander Erasto, Ally Mbegu na Bashir Salum.
Kwa ujumla jezi ambazo zimepata wavaaji wapya ndani ya kikosi hicho ni namba 28 iliyokuwa ikivaliwa na Aishi Manula, Mohamed Hussein (15), Omary Omary (8), Hussein Kazi (4), Debora Mavambo (17), Edwin Balua (37) na Saleh Karabaka (23).
Ambazo hazijapata waavaaji wapya namba 6 ya Fabrice Ngoma, Valentine Nouma (29), Augustine Okejepha (25), Kelvin Kijili (33), Che Fondoh Malone (20), Leonel Ateba (13) na Valentino Mashaka (27).
Hawa hapa wachezaji wa Simba kwa msimu wa 2025-2026 ambapo kwenye mabano ni namba za jezi kwa kila mmoja atakayovaa.
Moussa Camara (26), Husein Abel (28), Yakoub Suleiman (22), David Kameta ‘Duchu’ (15), Antony Mligo (5), Naby Camara (30), Abdulrazack Hamza (14), Rushine De Reuck (23), Chamou Karaboue (2), Vedastus Masinde (4), Wilson Nangu (31) na Shomari Kapombe (12).
Wengine ni Yusuph Kagoma (21), Alassane Kante (8), Awesu Awesu (33), Morice Abraham (18), Kibu Denis (38), Hussein Daud Semfuko (37), Joshua Mutale (7) na Mzamiru Yassin (19).
Pia kuna Mohamed Bajaber (17), Ladack Chasambi (36), Neo Maema (35), Jean Charles Ahoua (10), Elie Mpanzu (34), Steven Mukwala (11), Seleman Mwalimu (40), na Jonathan Sowah (3).