Msajili, CAG waguswa kesi ya rasilimali Chadema

Dar es Salaam. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimekana kuwa na nyaraka kuhusu rasilimali zake zilizoombwa katika kesi ya mgogoro wa mgawanyo wa rasilimali inayokikabili.

Kimesema Msajili wa Vyama vya Siasa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), ndio wenye baadhi ya nyaraka zinazoombwa.

‎Kesi hiyo ya madai namba 8323 ya mwaka 2025 imefunguliwa na Makamu Mwenyekiti mstaafu wa  Chadema, Said Issa Mohamed na wajumbe wawili wa Bodi ya Wadhamini wa Chadema kutoka Zanzibar, Ahmed Rashid Khamis na Maulida Anna Komu. ‎Walalamikiwa ni Bodi ya Wadhamini wa Chadema na Katibu Mkuu wa chama hicho.

‎Walalamikaji wanadai kumekuwa na mgawanyo usio sawa na wa mali na rasilimali fedha kati ya Zanzibar na Tanzania Bara, kinyume cha Sheria ya Vyama vya Siasa na Katiba ya chama hicho.

Vilevile wanadai kuna ubaguzi wa kidini na kijinsia, pamoja na kutoa maoni na matamko yaliyo na nia ya kuvuruga muungano kati ya pande mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

‎Kabla ya kuanza kusikilizwa kesi hiyo, walalamikaji kupitia mawakili wao, ‎Shaban Marijani, Gido Simfukwe na Alvan Fidelis, waliwasilisha shauri dogo.

Katika shauri hilo, wanaomba Mahakama iwaamuru walalamikiwa wawapatie nyaraka zinazoonesha mali zinazomilikiwa na chama, za fedha na za vikao kuanzia mwaka 2019 mpaka 2024, wanazotarajia kuzitumia katika kuthibitisha madai yao.

‎Nyaraka zinazoombwa ni Tamko la Mwaka la Mali zinazomilikiwa na chama hicho, taarifa za fedha zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na mihutasari ya vikoa vya bodi ya wadhamini wa Chadema.

Nyingine ni mihtasari ya ajenda za vikao vya kamati kuu, mihtasari yote ya ajenda za vikao vya Kamati Maalumu ya Zanzibar, mihtasari yote ya ajenda za vikao vya Sekretarieti ya Ofisi ya Makao Makuu ya Chadema -Zanzibar.

Taarifa nyingine ni za kibenki za akaunti namba 011103010075 yenye jina Chama cha Demokrasia na Maendeleo iliyoko Benki ya NBC.

‎Maombi hayo yamesikilizwa leo Septemba 9, 2025 na Jaji Hamidu Mwanga. Mawakili wa walalamikaji wamewasilisha hoja kuunga mkono maombi yao kabla ya kujibiwa na mawakili wa walalamikiwa.

Wakili Fidelis amedai katika maombi wamekidhi matakwa ya kisheria, akieleza nyaraka zinahusu kesi ya msingi, kama sheria inavyoelekeza.

‎Amedai nyaraka zilizoainishwa zinawiana na hoja bishaniwa (madai yaliyoainishwa katika hati ya madai) kwani zitasaidia kufikia uamuzi katika kuamua kesi ya msingi, kama kuna usawa katika mgawanyo wa rasilimali kati ya Bara na Zanzibar au la.

‎Amedai nyaraka hizo ziko mikononi mwa wajibu maombi na kwamba, hawajakataa kuwa haziko mikononi mwao badala yake wamesema hawawezi kuziwasilisha kwa sababu kuna amri ya zuio.

‎Amedai itakuwa ni haki nyaraka hizo zikiwasilishwa mahakamani kwa ajili ya kuamua kesi hiyo. Akaomba maombi yakubaliwe wapewe nyaraka hizo.

‎Mawakili wa Chadema, Hekima Mwasipu na Dk Rugemeleza Nshala wamepinga maombi hayo.

Mwasipu amedai nyaraka za kumbukumbu na ajenda za vikao vya kamati kuu hazina uhusiano na kesi ya msingi na kwamba, Chadema vikao vya kamati kuu vinafanyika mara nne kwa mwaka.

Amedai miongoni mwa ajenda ni kuwa na uhusiano na vyama vingine duniani jambo ambalo halina uhusiano na kesi ya msingi

‎Hivyo, Mwasipu amedai haina mantiki kuomba kumbukumbu za vikao vyote hivyo, akidai ni kinyume cha sheria na waombaji walipaswa kuainisha zile tu zinazohusu kesi.

‎Wakili huyo amedai Kamati Maalumu ya Zanzibar pia inakutana mara nne kwa mwaka na kuna vikao vya dharura. Amesema hujadili mapendekezo ya kuwasilisha mambo yote yanayohusu Zanzibar kwa kamati kuu, pamoja na yahusuyo sera Zanzibar.

Amedai walipaswa wabainishe ni kikao gani kilijadili mambo yanayohusu kesi yao.

‎”Kwa msingi huo, wenzetu walipaswa wawe specific. Waeleze ni kikao gani na cha lini kilijadili mambo yanayohusu kesi yao,” amesema.

‎Kuhusu tangazo la mwaka la mali za chama na taarifa iliyokaguliwa na CAG amedai haziko katika mikono ya walalamikiwa.

Ameeleza chini ya kifungu cha 33 (2) (ii) cha Sheria ya Vyama vya Siasa nyaraka hizo ziko kwa Msajili wa Vyama vya Siasa na ndiye anahusika na taarifa ya ukaguzi ya CAG.

Pia, amedai kuna utaratibu wa kuomba nyaraka kwa Msajili wa Vyama vya Siasa, akieleza Mahakama ndiyo inaweza kumwelekeza msajili kuziwasilisha mahakamani.

Mwasipu amedai si sharti la kisheria kuwa lazima walalamikiwa wabaki na nyaraka hizo.

‎Amedai walalamikaji wanaomba nyaraka hizo ili kufukia mashimo katika kesi yao kutokana na pingamizi lililoibuliwa na walalamikaji kuwa hawana shababu ya mada.

Dk Nshala amedai hakuna viapo vya walalamikaji Ahmed Rashid Hamis na Maulida Anna Komu kuunga mkono maombi hayo na kwamba, kiapo kilichopo cha Said kina kasoro za kisheria.

‎Amedai katika chama hakuna nafasi ya kiongozi mwandamizi Zanzibar, kama alivyojitambulisha katika kiapo hicho.

‎Ameeleza kuwa Said aliwahi kuwa Makamu Mwenyekiti wa Chadema (Taifa), lakini sasa hana wadhifa wowote ndani ya chama hicho.

‎Vilevile amedai Said katika kiapo ameeleza alijaribu kupata nakala hizo bila mafanikio lakini akasema aliomba nakala za mwaka mmoja pekee, hivyo anayoyasema ni uongo, kwani hajawahi kuwaomba walalamikiwa nyaraka alizotaja.

Ameiomba Mahakama ikifute kiapo cha Said kutokana na kuwa na uongo, hatua ambayo itaathiri maombi hayo kwa kutupiliwa mbali, akieleza hayawezi kusimama mahakamani bila kiapo.

Wakili Marijani amesema madai ya uongo kwenye kiapo cha Said ni mamlaka ya mahakama kuamua baada ya kupitia hoja na si walalamikiwa.

Kuhusu utambulisho wa Said kuwa kiongozi mwandamizi, amesema ni tafsiri yenye maana kuwa inaweza kuwa ukongwe na si wadhifa.

Marijani amedai nyaraka wanazoziomba walalamikaji zinahusu majadiliano ya mgawanyo na matumizi ya rasilimali na wamezianisha kwa kuzitaja majina na miaka.

Amedai katika viapo vyao vyote viwili walalamikiwa hakuna mahali walikokana kuwa hawana nyaraka hizo.

Wakili Fidelis amedai kama walalamikaji wanapinga, walipaswa wapinge kwenye kiapo kinzani.

Jaji Mwanga amesema atatoa uamuzi Septemba 29, 2025 saa tano asubuhi.