SIMBA jana ilikuwa bize na kilele cha tamasha la Simba Day linalotambulisha uzi na kikosi kipya, lakini kuna mmoja wa mastaa waliotakiwa kutambulishwa mbele ya mashabiki kuwa kipa mpya, Yakoub Seleman, huku Moussa Camara akiimpa maua yake mapema na kumkaribisha.
Yakoub aliyesajiliwa Simba akitokea JKT Tanzania ni miongoni mwa wachezaji waliofanya vyema msimu uliomalizika, huku kiwango chake kikiwavutia zaidi mabosi wa Wekundu.
Camara ameliambia Mwanaspoti kuwa ameona usajili mkubwa na mzuri ambao klabu hiyo imeufanya kwa Yakoub ambaye ni kipa chaguo namba moja wa Tanzania.
Alisema kuwa hana shida na usajili wa Yakoub, huku akiwasifia viongozi na benchi la ufundi la kikosi hicho kwa kuwaongezea mtu mwingine bora anayetua ili washirikiane.
“Nimeona kuna kipa amesajiliwa, namjua alikuwa ile timu ya jeshi ni kipa mzuri sana Yakoub, umri wake bado mdogo na amefanya vizuri sana msimu uliopita,” alisema Camara na kuongeza:
“Namkaribisha Simba ni klabu kubwa ambayo tunatakiwa kushirikiana ili tuipe mafanikio na sio kuangalia tutashindana vipi kwenye kucheza.”
Camara alisema makipa wote Simba ni wazuri ambapo uamuzi wa nani atacheza au atakuwa chaguo la kwanza litakuwa kwa makocha.
“Hakuna mchezaji anayepanga acheze, makocha ndio wanaamua kila mmoja atafanya juhudi na sio tu huyu kipa mgeni, lakini hata wengine waliobaki ni wazuri ndio maana wapo Simba. Kwetu sisi kazi yetu ni kujituma kuanzia mazoezini mpaka kwenye mechi.
“Jukumu la nani atacheza hilo wataamua makocha, mimi na wenzangu tunatakiwa kushirikiana kujipanga na kushauriana namna gani Simba itafanikiwa hilo ndio la muhimu,” alisema.
Camara ambaye pia ni kipa namba moja wa timu ya Taifa la Guinea aliogeza kuwa anaamini ujio wa Yakoub utaongeza kitu kikubwa katika timu hiyo ambapo lengo ni Simba kufanikiwa. Katika mechi mbili za kuwania kufuzu Kombe la Dunia, Camara akiwa na Guinea amekuwa kwenye kiwango bora akicheza mechi dhidi ya Somalia wakishinda 3-0 na suluhu na Algeria akitoka bila kuruhusu bao.
Wakati Camara akipata matokeo hayo, Yakoub aliruhusu mabao mawili kwenye mechi dhidi ya Congo Brazaville na Niger.