KIUNGO wa Singida Black Stars, Khalid Habib ‘Gego’ amesema ndoto imetimia baada ya uongozi kuinasa saini ya Khalid Aucho, mchezaji ambaye amekuwa akimfuatilia na kujifunza vitu kutoka kwake sasa atacheza naye timu moja.
Mwanaspoti liliwahi kufanya mahojiano na kiungo huyo ambaye alidai kumkubali Aucho kipindi anacheza Yanga , ila sasa ni rasmi watacheza pamoja msimu huu.
Akizungumza na Mwanaspoti, Gego alisema kutoka kumtazama kwa lengo la kujifunza vitu hadi kucheza naye timu moja ni fursa pana kwake kuzungumza naye na kuendelea kuchota madini kutoka kwake.
“Aucho ni mchezaji mzuri ana vitu vingi vya kutoa darasa kwa viungo kama mimi. Nimefurahi kuona atakuwa sehemu ya kikosi chetu tukicheza timu moja naamini nitakuwa na nafasi nzuri ya kuwa mwanafunzi wake,” alisema.
“Bado sijapata nafasi ya kuzungumza naye kutokana na kutokuwa karibu na mimi kutokana na majukumu ya timu yake ya taifa lakini naamini akirudi nitazungumza naye na kumueleza ni namna gani namkubali na nimekuwa nikimfuatilia.”
Gego akizungumzia ujio wake kwa mannufaa ya timu alisema ni mchezaji mzoefu na amecheza mashindano mengi makubwa hivyo atakuwa chachu kwao kuwapa uzoefu wa mashindano hasa ya kimataifa wakiiwakilisha nchi Kombe la Shirikisho Afrika.
“Tumepata uwakilishi wa michuano ya kimataifa kikosi kilikuwa kina hitaji wazoefu na wachezaji bora usajili umefanywa naamini timu itatoa uwakilishi mzuri na lengo ni kufanya vizuri;
“Ukiondoa Aucho kuna nyota wengine bora wamesajiliwa kikosini nina imani kubwa timu yetu itafanya vizuri chini ya kocha mwenye uzoefu wa michuano hiyo na ligi ya Tanzania Miguel Gamondi.” Gego alisema Sigida Black Stars imekam,ilika kila eneo kilichobaki sasa ni kufanya kazi kwa vitendo kwenye ligi ya ndani na kimataifa huku akiweka wazi kuwa malengo yao ni kutetea nafasi waliyomaliza msiomu uliopita au kuvuka zaidi lakini kimataifa ni kucheza hatua ya makundi.