JKT Queens mzigoni tena | Mwanaspoti

MABINGWA wa Ligi Kuu ya Wanawake, JKT Queens leo wanashuka tena uwanjani kusaka tiketi ya kwenda nusu fainali ya michuano ya Klabu Bingwa kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) watakapowakabili Yei Joint Stars kutoka Sudan Kusini.

Mechi hiyo itapigwa kwenye Uwanja wa Ulinzi Complex uliopo jijini Nairobi, Kenya ikiwa ni mechi ya mwisho ya Kundi C.

Hadi sasa Rayon Sports ya Rwanda ndio pekee iliyofuzu nusu fainali baada ya kumaliza na pointi nne katika Kundi B.

Kundi la maafande hao wa kike,  tayari JKU Princess ya Zanzibar imeondolewa kutokana na vichapo viwili mfululizo na mechi ya leo itaamua kati ya Yei na JKT nani aenda nusu fainali.

Timu hizo zote zimecheza mechi moja na JKT ilianza kwa kutoa ushindi mnono wa mabao 5-0 dhidi ya ndugu zao JKU, huku Yei ikiitandika maafande hao wa Zanzibar mabao 4-2.

Kocha Msaidizi wa JKT, Azishi Kondo alisema wanaingia katika mechi hiyo wakiwa na matarajio makubwa ya ushindi licha ya ugumu wa wapinzani wao.

“Tunaitaka nusu fainali, tunajua ugumu wa timu kama Yei na hatutaingia tukiwadharau wapinzani wetu, kile tulichokifanya mechi iliyopita kwenye mapungufu tumerekebisha na tulipopatia tumeongeza zaidi,” alisema Kondo.

Kocha wa Yei Stars, Isaac Lomoro alisema wanafahamu ubora wa JKT, lakini malengo ya timu ni kucheza nusu fainali na kuchukua kombe la CECAFA.

“Tunaifahamu vyema JKT ni timu nzuri na yenye ushindani kwenye mashindano haya, tunajua tutakutana na upinzani mkubwa lakini malengo yetu ni yale yale.”

Hadi sasa katika michuano hiyo inayotoa tiketi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Rayon Sport Women ndio iliyofuzu nusu fainali kutoka Kundi B hadi sasa imeshapata timu moja iliyotinga nusu fainali.