CECAFA Kombe Cup 2025 utamu uko hapa

MICHUANO ya Kombe la Cecafa Kagame imeendelea kunoga huku baadhi ya wachezaji waliotwaa tuzo ya mchezaji bora wa mechi wakifunguka kuhusu ugumu wa michuano hiyo ambayo imefika hatua ya nusu fainali, itakayoanza kuchezwa kesho, Ijumaa.

APR ya Rwanda, Singida BS na KMC za Tanzania ndizo timu za kwanza kutinga hatua hiyo kabla ya mechi za jana, Jumatano, ambapo ilifahamika timu moja kutoka kundi C ambayo itaungana na hao.

Kwa mujibu wa baadhi ya wachezaji hao, tuzo za mchezaji bora wa mechi zimekuwa nguzo ya kuongeza ushindani wa michuano ambayo tayari imejipatia heshima katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

Mmoja wa wachezaji hao, Ilyas Akram Khamis wa Mogadishu City, ambaye aliibuka mchezaji bora kwenye mechi dhidi ya Kator iliyomalizika kwa suluhu, alisema tuzo hiyo ilimfanya kuona ana kazi kubwa zaidi ya kufanya katika mechi zilizofuata.

“Kwetu sisi wachezaji, hii ni motisha. Unajua, unapotambuliwa mbele ya wachezaji wengine ambao nao walifanya vizuri, inakupa nguvu ya kuendelea kupambana,” alisema Khamis.

KAGA 01


Kuhusu mashindano hayo kwa ujumla, alisema; “Tangu tunakuja Tanzania tulijua kuwa mashindano yatakuwa magumu kwa sababu mara zote mashindano haya yamekuwa yakijumuisha timu bora. Nadhani watu wameona, mfano tazama kundi letu lilivyokuwa.”

Kabla ya mechi za jana, Jumatano, timu nne za kundi C, Al-Hilal Omdurman, Al-Ahly Wad Madani, Kator na Mogadishu City, kila moja ilikuwa imejikusanyia pointi mbili dakika 180 ilizocheza katika mechi mbili zilizopita za michuano hiyo.

Kwa upande wake, Ammanuel Admasu, ambaye aliweka rekodi ya kufunga mabao matatu ya kwanza hat-trick katika mashindano hayo dhidi ya Garde-Cotes, wakati Ethiopian Coffee ikiibuka na ushindi wa mabao 6-0, alisema licha ya timu yake kuishia hatua ya makundi, kuna mambo mengi wamejifunza.

“Mashindano ni magumu na yamekuwa na ushindani mkubwa. Naamimi utaendelea hadi katika hatua ya fainali. Nilitamani kuona tukifika huko lakini bahati haikuwa upande wetu baada ya kupoteza mechi ya mwisho,” alisema.

KAGA 02


Ethiopian Coffee imemaliza hatua ya makundi ikiwa na pointi nne ambazo ilivuna baada ya kutoka suluhu dhidi ya Singida BS na kuichapa Garde-Cotes ya Djibouti, huku ikipoteza mechi ya mwisho dhidi ya Polisi ya Kenya kwa mabao 2-0.

Katika hatua ya makundi, Ethiopian Coffee ni kati ya timu ambazo wachezaji wake wametwaa tuzo ya mchezaji bora wa mechi mara mbili, sawa na APR na Mogadishu. Mbali na Admasu, mchezaji mwingine ni Divine Nwachukwa ambaye alitwaa tuzo hiyo dhidi ya Singida BS.

KMC ndiyo timu pekee katika mashindano ya msimu huu ambayo imetwaa tuzo ya mchezaji bora wa mechi katika mechi zote tatu ambazo ilicheza katika hatua ya makundi. Ametwaa mara mbili Kelvin Tondi Revocatus na mara moja Redemtus Jeremia Mussa.

Abdelkader Ouabdi wa Al-Ahly Wad Madani naye alieleza; “Unapokuwa kwenye mashindano makubwa kama haya, kila mchezaji anapigania jina lake na klabu. Hii tuzo imenipa nafasi ya kuonyesha kile ninachoweza na pia kuipa heshima klabu yangu.”

KAGA 03


Kwa upande wa Hakim Kiwanuka wa APR, alisema kuwa ushindani mkubwa ndio unaofanya tuzo hiyo iwe na maana zaidi.

“Hapa hakuna mechi rahisi. Kila timu inakuja ikiwa na lengo la kushinda, hivyo ukipewa heshima ya kuwa bora, unajua kwamba kuna kazi umeifanya. Naamini tuzo hii itawasaidia vijana wengi kuamini katika uwezo wao,” alisema Kiwanuka.

APR, ambayo ilimaliza kinara wa kundi B ikiwa na pointi saba, sawa na KMC iliyotinga nusu fainali kama best loser, ina historia ya kutwaa ubingwa wa michuano hiyo. Pia ni wanafainali wa msimu uliopita ambapo walipoteza dhidi ya Red Arrows ya Zambia.

Naye Revocatus wa KMC alisema; “Kama mchezaji, kuna nyakati unahisi umefanya vizuri lakini haonekani. Hii tuzo inanifanya niamini kwamba kila dakika ninayopambana uwanjani inahesabika.”

Kuhusu hatua inayofuata katika mashindano hayo, Revocatus anaamini itakuwa ngumu zaidi kulingana na ubora wa timu ambazo zimetinga nusu fainali, lakini wapo tayari kwa changamoto hiyo.

KAGA 04


Katika hatua ya nusu fainali, KMC itacheza dhidi ya Singida BS, ambazo msimu uliopita walikutana mara tatu; mara mbili kwenye ligi na mara moja Kombe la FA. Katika mechi mbili za ligi, kila mmoja alishinda kwake. Ilianza Singida BS kwa kushinda mabao 2-1 nyumbani kabla ya KMC kujibu mapigo kwa mabao 2-0.

Katika mechi ya mwisho kwa timu hizo kukutana, ilikuwa katika Kombe la FA ambapo Singida BS ilishinda kwa bao 1-0.

Ni wachezaji wawili tu ambao wamebeba tuzo ya mchezaji bora wa mechi katika hatua ya makundi mara mbili kabla ya mechi za jana. Wachezaji hao ni Revocatus na Mosengo Tansele wa Polisi ya Kenya.

Revocatus ana nafasi ya kuendelea kukusanya tuzo hizo na kujiweka katika mazingira mazuri ya kuwa mchezaji bora wa mashindano hayo kama ataendelea kufanya vizuri, kutokana na timu yake kutinga hatua ya nusu fainali ambayo itacheza dhidi ya Singida BS.

(Kelvin Tondi Revocatus X2, Redemtus Jeremia Mussa)

Mogadishu City Club – tuzo 2

(Ilyas Akram Khamis, Quttara Said Mohamed)

(Hakim Kiwanuka, Dao Rouaf Memel)

Ethiopian Coffee FC – tuzo 2

(Ammanuel Admasu, Divine Nwachukwa)

Singida Black Stars FC – tuzo 2

(Malanga Horso Mwaku, Idd Khalid Gego)

Alahly Wad Madani SC – tuzo 1