Namna bidhaa feki, zisizo na ubora zinavyoingia nchini na athari zake

Ni janga. Uingizaji bidhaa feki na zisizo na ubora nchini unaweza kusema ni janga linalosubiri kulipuka kutokana na athari zake kiuchumi, kiafya hata kimaendeleo.

Uchunguzi uliofanywa na Mwananchi bidhaa feki/bandia zinazidi kushamiri katika masoko nchini hasa kwenye miji mikubwa kama Dar es Salaam, Morogoro, Mwanza, Pwani nk na mikoa ya mipakani; Kigoma, Songwe, Kagera, Mbeya, Musoma nk. Imefahamika.

Tumeshuhudia jinsi gani mamlaka za serikali zinavyopambana na hili, mfano Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) kwa sasa TMDA (Mamlaka ya Udhibiti wa Dawa, Vipodozi na Vifaa Tiba) ikiteketeza bidhaa feki zisizo na ubora za tani 1.6 za vyakula vya aina mbalimbali ambavyo havifai kwa matumizi ya binadamu vilivyokuwa na thamani ya zaidi ya Sh2.8 milioni habari iliyowahi kuripotiwa na gazeti Mwananchi.

Bidhaa zilikamatwa kutokana na ukaguzi wa kushtukiza uliofanywa katika mikoa ya kanda ya ziwa kwenye maduka ya bidhaa za chakula; chumvi aina ya Kaysalt, mafuta ya kupikia yenye nembo ya ufuta.

Pia mwaka 2016/2017 TFDA ilikamata na kuteketeza tani 63.7 za bidhaa mbalimbali za vyakula zisizo na ubora zenye thamani ya Sh136.3 milioni katika mikoa ya kanda ya ziwa; Shinyanga, Mwanza, Geita, Mara, Simiyu na Kagera. Bidhaa zilizokamatwa zilikuwa zimeisha muda wake lakini zilikuwa sokoni tayari, Mwananchi iliripoti.

Mathalani, katika eneo la dawa pekee, Mamlaka ya Udhibiti wa Dawa, Vipodozi na Vifaa Tiba (TMDA) inasema katika moja ya ripoti zake kuwa miaka miwili iliyopita, zaidi ya tani 435 za dawa za binadamu, dawa za mifugo na vifaa tiba visivyo na ubora na bandia vyenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 30, zilikamatwa na kuteketezwa.

Aidha, utafiti uliofanywa na Shirikisho la Wenye Viwanda nchini (CTI) miaka kadhaa iliyopita ulibaini kuwa wakati huo hasara inayotokana na bidhaa zisizo na ubora na bidhaa bandia inafikia asilimia 15 na 20 za pato la taifa kwa mwaka.

Mfano hivi karibuni TMDA ilitahadharisha uwepo wa sabuni za Dettol feki, Agosti 16, 2015 Mwananchi iliripoti taarifa hii, uwepo wa Dettol feki za maji zilizokuwa zikitengenezwa kinyume cha sheria katika nyumba ya kulala wageni mtaa wa Namanga, Kahama Mjini mkoani Shinyanga, taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa TMDA, Adam Fimbo.

Jinsi zinavyoingia, kuzalishwa

Akizungumza na Mwananchi, Profesa Abel Kinyondo wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam aliyebobea katika uchumi, anahoji kuhusu uingiaji wa bidhaa feki nchini, Serikali yetu ina taasisi nyingi zenye mamlaka ya kuzidhibiti na kusimamia uingiaji wa bidhaa feki, lakini tunashindwaje kuzui uingiaji wa bidhaa hizi.

“Tuna sheria na mamlaka za kutosha za kudhibiti uingiaji wa bidhaa hizi feki, lakini swali la kujiuliza hapa, kama mamlaka hizo tunazo na ziko kisheria tatizo liko wapi kwenye udhibiti wa bidhaa hizi? Na hizi bidhaa zinaingiaje? Hili suala litafutiwe ufumbuzi kwa maslahi ya taifa,” Anasema.

Katika uchunguzi uliofanywa na Mwananchi, bidhaa feki huingia nchini kupitia njia mbalimbali, ikiwamo:

Bandari na mipaka ya nchi: Wafanyabiashara haramu hutumia bandari na mipaka ya nchi kupitisha bidhaa zao, kwa kushirikiana na maofisa wasio waaminifu.

Njia za panya: Hizi ni njia zisizo rasmi za kuvuka mipaka ya nchi. Wafanyabiashara haramu hutumia njia hizi kuepuka ukaguzi.

Mara nyingi njia hizi hupatikana mipakani ambazo wafanyabiashara hutumia kusafirisha aidha kwa magari madogo au pikipiki ambapo huwa vigumu kwa maofisa wa mipaka kuwakamata, na mara nyingi bidhaa husafirishwa usiku.

Kutumia njia za usafirishaji zisizo rasmi: Bidhaa hizi huweza kusafirishwa kwa kutumia magari, boti, au ndege ndogo zisizo rasmi ili kuepuka ukaguzi.

Akizungumza na Mwananchi, Dk Mwinuka Lutengano wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) anasema, “njia nyingi za panya zinatumika kwenye uingizaji wa bidhaa feki nchini, haswa kwa njia ya maji (bahari, ziwa) haya majahazi yanahusika sana kwenye usafirishaji, naona inapaswa mamlaka sasa zisimame kwenye hizi njia ili kufanya udhibiti wa haya magendo, maana mwisho wa siku taifa ndio linaathirika pakubwa.”

Pia kupitia mitandao holela na udhaifu katika mifumo ya utekelezaji wa sheria. Imefahamika. Kuwapo kwa bidhaa feki kunadhoofisha utawala wa sheria na kuonyesha kuwa sheria hazifuatwi ipasavyo. Hii inaweza kuathiri maadili ya jamii na kuongeza tabia ya kutojali sheria.

Aidha, kuwapo kwa viwanda bubu nchini, nako kunachangia uzagaaji wa bidhaa feki zisizo na ubora ambazo ni hatari kwa jamii.

Katika ripoti maalum iliyofanywa na Mwananchi, Desemba 14, 2013 kuhusu Vita ya Viwanda Bubu Vipiganwe na Wote, inaonyesha jinsi gani viwanda bubu nchini vinavyosababisha ongezeko la bidhaa feki na zisizo na ubora haswa kwenye vinywaji; pombe, juisi, maji; vifaa vya umeme, mbolea, biskuti hata dawa. Hii inachochea kuporomosha uchumi wa nchi hata kuleta madhara kwa jamii kiafya.

Hivi karibuni Julai 9, 2025 watu wawili walikamatwa kwa kumiliki kiwanda bubu cha biskuti zinazochanganywa na bangi kilichoko Sinza jijini Dar es Salaam, hayo yalithibitishwa na Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo.

Akizungumza na Mwananchi, Aboubakary Mlawa Ofisa Uhusiano wa kampuni ya MMI Steel Mills LTD ambao ni wazalishaji wa mabati na nondo anasema;

“Viwanda vinavyotengeneza bidhaa zisizo na ubora vinaumiza sana soko la ndani na hata usambazaji wa bidhaa nje ya nchi. Bidhaa feki hazitoki tuu nje ya nchi, hata ndani zinazalishwa sana, kuna viwanda bubu vipo vingi wanachofanya wanachukua chapa ya bidhaa ya kampuni husika wanaweka kwenye bidhaa wanazotengeneza.”

Anasema MMI walishafanya misako kwa wasambazaji wa bidhaa zao na hata wenye maduka wanaouza bidhaa wanazozizalisha.

“Tulikutana na balaa! Bati nyingi na nondo zilizoko dukani si za viwandani kwetu lakini ukizikagua zinachapa yetu. Tukifanya msako mara nyingi tunashirikisha Jeshi la Polisi kwa hiyo wahusika hukimbia na kuacha maduka yao baada ya kupata fununu ya ukaguzi.

Anasema wamebaini hapa nchini kuna viwanda bubu vinavyozalisha bidhaa feki na mara nyingi zinauzwa kwa bei rahisi.

Mlawa anasema hiyo inasababisha wafanyabiashara wasiojali ubora wakizinunua kwa kupata faida tu, na tatizo linakuja kwa watumiaji wao ambao wanalalamikia kiwanda fulani bidhaa zao ni feki bila kujua walichochukua si halisi.

Anasema bidhaa feki ni janga kubwa na linapaswa kushughulikiwa ipasavyo kwa mamlaka kushirikiana katika udhibiti wake, “Nashauri TBS, FCC, TPA, TMDA wafanye ukaguzi hasa mipakani, viwandani, bandarini yaani kwenye sehemu zote za usafirishaji na uzalishaji nahisi tutadhibiti hili kwa kiasi.”

Anaendelea, “TBS wanajitahidi kufanya mikutano na wafanyabiashara, wazalishaji na wasambazaji wa bidhaa, wanatoa elimu ya umuhimu wa kuwa na barcodes na alama maalumu ambayo mzalishaji bidhaa atakuwa nayo, hata mzalishaji wa bidhaa feki hataweza kuitumia alama hiyo, kwa maana ukiiscan kama ni feki haitakupa taarifa za bidhaa lakini kama ni yenyewe ukiiscan itakupa taarifa ya bidhaa husika,” anasema.

Mlawa anabainisha kuwa kwenye mabati hutumia muhuri wa kompyuta ambao utaonyesha tarehe, muda wa uzalishaji na mwisho wa matumizi.

Lakini anasema changamoto huja kwa wanunuaji, hawana elimu ya bidhaa feki wao wanaangalia chapa tu kama ni Kiboko au Alaf wanachukua bati, ikivuja baada ya muda mfupi au imepauka tofauti na matarajio yake hufika kulalamika kuwa bidhaa zao ni feki hazina ubora, ilhali hakutambua bidhaa halisi.

Mfanyabiashara wa duka la vipodozi Kariakoo, Johnson Pius anasema, “Leo tuna bandari nyingi sana bubu zinazotumika kupitishia bidhaa za magendo na feki zinajulikana kabisa. Sasa kwa nini kisiundwe kikosi maalum cha kukabiliana na janga hili la uingizwaji wa bidhaa za magendo na feki kitakacho jumuisha vyombo vyote vya usalama?

Anataja jinsi sukari, mafuta, matairi ya magari, spare party za magari na nk vinavyoingizwa nchini kwa njia zisizo halali jambo ambalo si hatari tu kwa maisha ya Watanzania pia ni hatari kwa ustawi wa uchumi kwani hazilipiwi kodi.

“Shida nyingine inakuja kwa watumiaji nao wanapenda vitu vya bei rahisi, kwa hiyo akiuziwa mafuta ya kupakaa kwa bei rahisi anaona bora kuliko kuuziwa kitu original (halisi) kwenye duka lingine kisa bei yake iko juu, kwa hiyo watu wanaangalia unafuu wa gharama na si ubora wa bidhaa. Na wafanyabiashara wasio na huruma wanawauziwa feki kwasababu yeye anaangalia faidi zaidi kuliko madhara kwa mteja,” anasema.

Anashauri mamlaka husika zishughulikie uingizwaji bidhaa feki, zisifurahie kukamata na kuteketeza wakati tayari zimeshatumiwa na Watanzania wengi, wazizuie kabisa zisiingie nchini.

Naye Justine Yona, mfanyabiashara wa duka la jumla la vyakula anasema, Sheria ya Kudhibiti Uingizaji Bidhaa Zenye Athari Kiuchumi, Sura ya 60 inaelezea vizuri kuhusu bidhaa za magendo zinavvyodhibitiwa nchini na inapiga marufuku Tanzania kuwa shimo la bidhaa zilizochoka, lakini waingizaji wao wanaangalia zaidi maslahi yao.

Aidha, Chacha Mussa mfanyabiashara wa mabati na msambazaji wa vifaa vya ujenzi, anasema usipokuwa mtaalamu wa kuzijua bidhaa halisi, utajikuta unaingiza mzigo kwa gharama kumbe mzigo uliuobeba ni feki.

“Nilishawahi kuagiza mzigo wa vifaa vya ujenzi kutoka nchi jirani, ulikamatwa tu ulipofika nchini kwa madai ni mzigo wa magendo. Nilipata hasara ya Sh500 milioni ambazo nilikopa. Mamlaka zetu zinapaswa kutoa elimu kwa wafanyabiashara, pia zifanye ukaguzi hasa kwenye mipaka maana wakizembea tu huko, bidhaa ishafika sokoni walaji wanatumia,” anasema.

Biashara ya bidhaa feki inaendelea kuathiri uchumi wa nchi, huku takwimu zikionesha Serikali inapoteza zaidi ya matrilioni ya kodi kutokana na uchepushaji wa bidhaa kupitia njia haramu.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Ushindani (FCC), Khadija Ngasongwa, anasema biashara haramu inaleta madhara makubwa, ikiwamo kupunguza mapato ya Serikali, kuhatarisha afya ya umma na kudhoofisha ushindani wa haki, ambao ni msingi wa ukuaji wa sekta ya viwanda.

Bidhaa feki zinazoingizwa nchini huathiri mapato ya Serikali, sababu huingia kimagendo bila kukaguliwa, zinakwepa kodi na ushuru, hivyo serikali inakosa mapato ambayo yangeweza kutumika kwa ajili ya maendeleo ya nchi.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Prof Abel Kinyondo anasema, bidhaa za magendo huuzwa kwa bei ya chini zaidi ikilinganishwa na bidhaa zinazozalishwa ndani ya nchi, na kusababisha ushindani usiokuwa sawa.

Anasema hiyo inaathiri viwanda vya ndani na inaweza kusababisha kufungwa kwa baadhi ya viwanda, na hivyo kusababisha upotevu wa ajira na wafanyabiashara wanaozalisha bidhaa halali kushindwa kushindana na bidhaa feki kwa sababu huuzwa kwa bei ya chini, hali inayoweza kusababisha kufungwa kwa viwanda na biashara za ndani na kusababisha upotezaji wa ajira.

“Bidhaa feki ni janga kubwa hasa katika uchumi wetu, zinaua viwanda vya ndani, madhara yake wananchi kukosa ajira, maana mwenye kiwanda halali kutokana na gharama za uzalishaji anazotumia hawezi kuuza ile bidhaa kwa bei nafuu lakini anayeingiza bidhaa feki za magendo atauza kwa bei ya chini sana mwisho wake soko la ndani litashuka,” anasema Profesa Kinyondo.

Kupoteza imani kwa watengenezaji wa bidhaa halali, wakati watumiaji wanapokumbana na bidhaa feki, wanaweza kupoteza imani kwa chapa halisi, hata kama chapa hiyo haihusiki na bidhaa feki. Hii inaathiri soko na sifa ya bidhaa halisi.

Anataja pia kupoteza ubora wa viwango vya kimataifa, kama bidhaa feki zikizalishwa kwa wingi nchini ni hatari kwa soko la Tanzania kimataifa kwa kuwa soko litapoteza imani kwa watangazaji wa bidhaa na kusababisha mdororo wa uchumi nchini hata kwa washindani wa kibiashara itakuwa fursa kwao kutangaza bidhaa zao.

“Ni vigumu kwa watumiaji kujua nani wa kumwamini. Soko linajaa bidhaa zisizoaminika, na kufanya ununuzi wa bidhaa kuwa jambo la hatari,” anasema Profesa Kinyondo.

Ili kupunguza athari za bidhaa za magendo, ni muhimu kwa serikali kuimarisha udhibiti wa mipaka, kuongeza ukaguzi katika bandari na mipaka, na kutoa elimu kwa wananchi kuhusu hatari za kutumia bidhaa hizi.

Pia uanzishwaji wa vikundi vya kulinda uchumi ngazi za serikali za mitaa itaweza kusaidia kuwabaini wenye nia ovu, wanaoanzisha viwanda bila kufuata utaratibu wa kisheria, wanaoingiza bidhaa feki, wanaosambaza na wanaosafirisha ili sheria ichukue mkondo wake.

Kupambana na bidhaa feki kunahitaji ushirikiano kati ya serikali, wafanyabiashara halali, na watumiaji wenyewe. Unapokuwa mwangalifu unaponunua bidhaa, unasaidia kupunguza matatizo hayo na kuunga mkono uchumi halali wa nchi.