Mambo 11 yaliyoibeba sekta ya utalii dhidi ya Uviko-19

Dar es Salaam. Wakati sekta ya utalii duniani ikirejea katika nafasi iliyokuwapo kabla ya ugonjwa wa Virusi vya Korona (Uviko-19), haya hapa mambo 11 yaliyoibeba sekta hii kwa Tanzania.

Mambo hayo kwa mujibu wa Ripoti yamechangia kuongezeka kwa mapato ya utalii nchini kwa asilimia 15.7 hadi kufikia dola za Kimarekani bilioni 3.903 (Sh10.15 trilioni) mwaka 2024 kutoka dola bilioni 3.373 (Sh8.77 trilioni) zilizokusanywa mwaka 2023.

Hii imetokana hasa na kuongezeka kwa idadi ya watalii waliowasili kutoka 1,808,205 mwaka 2023 hadi 2,141,895 mwaka 2024 ikiwa imerejea kikamilifu na hata kuvuka viwango vya kabla ya janga la Uviko-19 kwa asilimia 40 huku mambo 11 yakitajwa kuwa sababu.

Katika kipindi cha miaka mitano kabla ya Uviko-19, idadi ya wageni wa kimataifa iliendelea kukua kwa wastani wa asilimia saba kwa mwaka, wakati baada ya janga hilo, kiwango cha ukuaji wa wageni wa kimataifa kimeongezeka kwa wastani wa asilimia 48 kwa mwaka.

Hata hivyo, mwaka 2024 ulionekana kuwa wa kipekee kutokana na kupaa kwa idadi ya wageni na mapato huku mambo yaliyochangia miongoni mwake ikiwa ni tamasha la Land Rover festival lililofanyika Oktoba 2024.

Tamasha hili lililenga kusherehekea uimara na matumizi mbalimbali ya aina hiyo ya magari, pamoja na nafasi yake muhimu katika sekta ya safari jambo lililoifanya Arusha kung’ara kimataifa, kwa kuonyesha utajiri wake wa kitamaduni.

Kuanza kwa safari za moja kwa moja za ndege nayo imetajwa kuwa sababu nyingine ya ukuaji huo ambapo Juni 2024, Shirika la World2fly lilifanya safari yake ya kwanza kutua Zanzibar, likiwa limeleta zaidi ya watalii 400 kutoka Madrid, Hispania. Safari hii inaashiria mwanzo wa njia mpya ya ndege ya kila wiki kati ya Madrid na Zanzibar, ambayo itakuwa ikifanyika kila Jumamosi.

Jambojet nao Julai 2024 ilizindua njia mpya ya safari ya ndege kati ya Mombasa na Zanzibar. TUI Fly nayo Novemba 2024 ilianzisha safari mpya ya ndege kati ya Zanzibar na Uholanzi likifanya safari mara mbili kwa wiki, likileta wasafiri 300 hadi visiwani Zanzibar kila wiki.

Akizungumzia suala hili, Profesa Abel Kinyondo amesema ili kusaidia watalii kutoka nchi za mbali kuongezeka na kurudi tena wanapotoka nchini ni vyema kuhakikisha kuwa visa kwa wageni zinapatikana kwa urahisi.

Haijalishi wametoka wapi, kuna kitu kimefanyika wanaotoka mbali kurudi kwenye utalii kitu muhimu kuliko vyote, hawapendi mambo mengi shida yetu kubwa ni upatikanaji wa visa shida iliyopo bado nchi ndogo hatuna balozi kila sehemu duniani kuna maeneo mengi hata ulaya ya magharibi hawana balozi

“Unakuta balozi moja inasimamiwa na balozi moja, visa ipatikane mtandaoni tunaweza kufanya vizuri na kuwaleta hao, mtu aweze kuomba sehemu yoyote na kama kuna kitu kinabakia awasilishe akishafika nchini,” amesema Profesa Kinyondo.

Amesema kukosena kwa balozi katika baadhi ya nchi inaongeza gharama kwa wasafiri kwani ili kuipata visa wanatakiwa kuingia gharama za kusafiri na malazi ili aweze kushughulikia visa ya kuja Tanzania.

Bidhaa gani zinazotolewa mbali na Serengeti, Ngorongoro na Zanzibar ambazo zimefanya baadhi ya watu kuzizoea hivyo ni vyema kuwa na vivutio ambavyo wageni hawawezi kukipata sehemu zozote.

“Ndiyo maana nchi za wenzetu wanawekeza katika vivutio vya kutengeneza ndiyo maana Marekani wanakuonyesha Disney Land hakuna wanyama wala nini lakini ni eneo kubwa ambalo unaweza kuzunguka wingi nzima, Paris wana mnara mrefu ambao kila mtu anataka kufika hapo na unavutia watu wengi,” amesema.

Amesema hiyo ni tofauti na Tanzania ambayo imesimamia vivutio asili pekee wakati ambao dunia imehama kutoka huko.

“Ni vyema Serikali ikashirikiana na sekta binafsi kuwekeza katika vivutio vya kutengeneza ili watu waweze kuvutiwa tena na tena wanapokuja na zinaweza kuongezwa kila mwaka,” amesema.

Mtaalamu wa Uchumi, Profesa Aurealia Kamuzora amesema ili sekta hii ikue zaidi ni vyema kuongeza miundombinu ikiwamo ya usafirishaji na huduma ya malazi.

“Pia tuongeze vyuo vya utalii ili kuzalisha watu wanaoweza kutumika katika kutembeza watalii katika maeneo mbalimbali,” alisema Profesa Kamuzora.

Kuongeza idadi ya vivutio ni moja ya kitu alichokigusa huku akisisitiza kuwa utamaduni wa mikoa unaweza kuwa mwarobaini katika hilo.

Hiyo ikiwa na maana kuwa, kutumia asili ya mikoa husika inaweza kuvuta watalii kutoka sehemu tofauti kutembelea nchini kwa kile ambacho watakuwa wakikipata huko ikiwamo ngoma asili na vyakula vya maeneo husika.

 “Tuanzishe hata kozi za vyakula asili vya kitanzania, mtu akiingia katika hoteli kubwa awe na uwezo wa kuchagua chakula cha asili kama kisamvu, hakifundishwi sehemu yoyote lakini watu wanafundishwa nyumbani, ikiwamo hii watu wakajua itafanya tuwe na utofauti na watu wengi,” amesema.

Sababu nyingine zilizokuza utalii

Kuwapo kwa mashindano ya Kimataifa ya Kuteleza kwa Parachuti (Kite Surfing) 2024 – Zanzibar Cup Kusi yaliyozinduliwa Agosti 2024 na Baraza la Michezo la Taifa Zanzibar nayo yalichochea ukuaji wa utalii visiwani.

Hiyo pia ilihamasisha maingiliano ya kitamaduni na umoja miongoni mwa washiriki kutoka mataifa mbalimbali, kwani yalivutia washiriki kutoka nchi mbalimbali zikiwamo Austria, Italia, Afrika Kusini, Uingereza, Poland, Jamhuri ya Czech na Hispania.

Mambo mengine yaliyobeba utalii mwaka 2024 ni Hifadhi ya Taifa ya Ruaha kuzindua Ziara za Puto la Hewa (Hot Air Balloon), Shirika la Umoja wa Mataifa la Utalii Duniani (UNWTO) liliidhinisha Chama cha Wawekezaji wa Utalii Zanzibar (ZATI) kuwa mwanachama mshirika mpya Novemba 2024, Zanzibar kujiunga rasmi na Baraza la Kimataifa la Utalii Endelevu (Global Sustainable Tourism Council – GSTC) mwezi Mei 2024.

Ziara za kutumia puto la hewa katika Hifadhi ya Taifa ya Ruaha zilizinduliwa mwezi Oktoba 2024, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 60 tangu kuanzishwa kwa hifadhi hiyo. Hifadhi ya Ruaha ni mshiriki muhimu katika utalii wa mazingira (ecotourism), ikiwapa wageni uzoefu wa kipekee kama vile safari za wanyamapori, utazamaji wa ndege, na matembezi ya miguu ndani ya hifadhi.

Uzinduzi wa ziara za puto la hewa unatarajiwa kuvutia watalii wengi zaidi na kuongeza ubora wa uzoefu wa wageni ndani ya hifadhi hiyo. Tanzania Imzindua Tuzo za Kitaifa za Utalii na Uhifadhi

Ili sekta hiyo ikue zaidi, Waziri wa Utalii na Maliasili, Dk Pindi Chana alipokuwa anawasilisha bajeti alisema wamechukua hatua madhubuti ili kukuza sekta hiyo kwa kupunguza na kuondoa tozo na kero zilizokuwa zinawakwaza wadau.

Amesema wizara imefanya mabadiliko ya viwango vya ada ya leseni ya Biashara za Utalii (TTBL) kwa ajili ya wawekezaji wazawa wa huduma za malazi zilizopangwa katika daraja za ubora na zile ambazo hazijapangwa katika daraja kwa lengo la kuhamasisha uwekezaji.

Dk Pindi amezitaja ada nyingine zilizopungua ni daraja la nyota tano kutoka Dola za Marekani 2,500 hadi Dola1,500 (Sh6.5 milioni hadi Sh3.9 milioni) daraja la nyota nne kutoka Dola 2,000 hadi Dola 1000 (Sh5.2 milioni hadi Sh2.6 milioni).

Nyingine zilizopungua ni daraja la nyota tatu kutoka Dola 1,500 hadi Dola 500 (Sh3.9 milioni hadi Sh1.3 milioni), daraja la nyota mbili kutoka Dola 1,200 hadi Dola 300 (Sh3.12 milioni hadi Sh780,000) na daraja la nyota moja kutoka Dola 1,000 hadi Dola 200 (Sh2.6 milioni hadi Sh520,000).