Iwe unanunua katika duka la rejareja au unaagiza chakula mtandaoni, kulipa si changamoto tena kwani salio hupunguzwa moja kwa moja. Hakuna tena foleni ndefu wala usumbufu wa kutafuta chenji; kila kitu hukamilika kwa sekunde chache tu.
Urahisi huu wa mifumo ya kielektroniki umekubalika kwa kasi miongoni mwa Watanzania, ukirahisisha biashara na kupunguza kabisa hitaji la kubeba pesa taslimu. Hata hivyo, kwa sababu hatuoni noti zikiondoka mikononi mwetu, mara nyingi ni rahisi kusahau thamani halisi ya kile tunachotumia kila siku.
Tofauti na malipo ya pesa taslimu, ambapo unamkabidhi muuzaji noti au sarafu na hivyo kuhisi kupungua kwa fedha zako, malipo ya kidijitali hufanyika bila kushika au kuona fedha halisi, jambo linalofanya usione wazi kama unatoa au unapokea.
Katika tabia za kifedha, inaaminika kwamba mtumiaji anaposhika fedha na kuzitoa mkononi, hupata hisia zinazomkumbusha kuwa akiba yake inapungua. Hisia hiyo humfanya kujiuliza kama kweli anahitaji kile anachonunua.
Lakini anapobonyeza kitufe cha lipa kwenye programu ya simu, hisia hiyo hupungua sana, na hatua ya kufanya malipo inakuwa ya haraka zaidi.
Matokeo yake, mtu anaweza kutumia zaidi ya alivyopanga. Katika mazingira haya, mwenendo wa matumizi yasiyopangwa au pupa (impulsive purchase) huwa na uwezekano mkubwa kuongezeka, hasa kwa vizazi vinavyozoea teknolojia tangu wakiwa wadogo.
Takwimu za sekta ya fedha zinaonyesha kwa wazi jinsi urahisi huu ulivyoenea. Mwaka 2024, thamani ya miamala ya simu ilipanda hadi Sh198.9 trilioni, ongezeko la asilimia 28.54 kutoka Sh154.7 trilioni mwaka uliotangulia.
Idadi ya akaunti na watumiaji wa huduma hizi imevuka milioni 63.2, jambo linalodhihirisha upanuzi mkubwa wa ujumuishaji wa kifedha nchini. Takwimu zinaweza kuwa zinaashiria kuongezeka kwa imani ya umma katika teknolojia ya malipo. Vilevile, zinaonyesha namna upatikanaji wa mtandao na simu janja unavyoendelea kubadilisha mienendo ya kifedha hata maeneo ya vijijini kuna pia upande wa akiba. Thamani ya akiba zinazohifadhiwa katika mifumo hii iliongezeka hadi Sh1.2 trilioni. Hata hivyo, idadi ya miamala ya kuweka akiba imepungua, ikimaanisha watu wanahifadhi kidogo na kutoa mara kwa mara.
Pengine urahisi wa kutoa pesa unachochea matumizi haraka na kuacha akiba katika kiwango cha chini. Bila tabia ya kuokoa mara kwa mara, familia zinaweza kukosa uhakika wa kifedha inapozuka dharura.
Mazingira haya mapya yanahitaji elimu ya kifedha iliyo maalum na ya kina. Watumiaji hawapaswi kufundishwa tu namna ya kutuma na kupokea pesa, bali pia jinsi ya kudhibiti matumizi yao ya kila siku. Kupanga bajeti, kuweka mipaka ya matumizi, na kutathmini gharama halisi ya mikopo kabla ya kukopa ni mambo ya msingi yanayoweza kulinda uthabiti wa kifedha.
Vilevile, waendeshaji wa huduma pia wanawajibika kutoa taarifa zilizo wazi kuhusu ada na viwango vya riba, ili kuepusha mkanganyiko kwa wateja.
Vilevile, watoa elimu wanapaswa kusisitiza kwamba ingawa kulipa ni rahisi zaidi kwa zama hizi, lakini kila bonyeza ina athari katika bajeti ya mtu na inaweza kupunguza uwezo wake wa kuweka akiba na kuongeza changamoto ya matumizi ya pupa.
Kwa ujumla, tatizo si matumizi ya pesa yenyewe bali ni matumizi yasiyopangwa. Urahisi wa huduma hizi haupaswi kuwa sababu ya kupoteza usimamizi wa fedha binafsi.
Hali kadhalika, ni muhimu sasa kuoanisha maendeleo ya teknolojia ya malipo na nidhamu ya kifedha. Kujiwekea malengo ya kifedha na kuyazingatia kwa uthabiti kutasaidia kuepuka matumizi yasiyo ya lazima.
Kwa kufanya hivyo, Watanzania wanaweza kufurahia urahisi wa huduma za kidijitali huku wakiepuka bila kuathiri malengo yao ya kifedha.