Umuhimu wa mipango ya kifedha na elimu ya fedha wakati wa uzeeni

Ni vigumu kama ni kijana kuamini kuwa uzee unaweza kukukuta haraka sana. Uzee unafuatana na mambo mbalimbali ikiwamo kuwa na maarifa.

Dunia pia inabadilika sana na majanga mbalimbali yametoa fundisho mbalimbali kwa jamii kuhusiana na umuhimu wa kuweka mipango ya kifedha na elimu ya fedha uzeeni.

Maisha marefu ni neema, lakini yanazalisha “hatari ya maisha marefu”: uwezekano wa kuishi zaidi ya akiba. Bila mpango, gharama za afya, mfumuko wa bei na dharura hutishia heshima na uhuru wa mstaafu. Linapofika suala la kustaafu inabaki ni swala la mtu binafsi na sio jukumu la kijamii, serikali au familia.

Tumeshasikia vilio vingi vya wazee kutelekezwa na nchi nyingine kuna nyumba za wazee wahudumiwe wakiwa pamoja. Hii ni namna ya kuhakikisha kuwa wanapata usalama. Watu wengi wenye pensheni wameishia kwenye hatari nyingi za athari za uzee zimehamishwa kutoka kwa waajiri/serikali kwenda kwa mtu binafsi.

Kuna tafiti zinaonyesha kuwa hata mifuko ya pensheni duniani inaelekea kubadili namna ambavyo watu wanachonufaika na mifuko ya fedha, wanufaika wakuu wawe wale wanaochangia zaidi.

Pia kuna mijadala mbalimbali kuhusiana na namna ambavyo michango mtu anaweza kuchagua kutokana michango, uwekezaji, ada na chaguo za malipo wakati wa pensheni.

Elimu ya fedha husaidia kutafsiri makadirio ya mapato ya baadaye, athari za michango kwenye mifuko ya kijamii, na mbinu za kupunguza hatari ya kuishi zaidi ya akiba kwa kutumia njia mbalimbali wakati wa kustaafu.

Kwenye jamii yetu sio watu wengi wana ajira na vipato ambavyo ni thabiti vinavyoweza kutengeneza akiba ya uzeeni inayoweza kuhimili mahitaji baada ya kustaafu.

Akiba wakati wa uzeeni huathiriwa na mambo mbalimbali kama kuporomoka kwa thamani ya fedha, ulimbikizaji wa madeni, kubadilika kwa mabadiliko ya hali ya hewa na pia namna ya uchumi unavyoendeshwa kwa mfano mabadiliko kwenye mfumo wa kifedha, kama kulipa kwa kutumia njia za kidigitali.

Kwenye elimu ya kifedha mabadiliko wa mifumo ya malipo ya kidigitali yana athari kubwa sana kwa wazee kuliko vijana kwa sababu matumizi ha kidigitali yameathiri wazee bila ujuzi wa kidijitali wa kutosha na hivyo kudumbukia katika athari za matumizi ya kidigitali hasa kwenye huduma za kifedha.

Katika kundi la wastaafu wanawake pia wanakuwa na hatari zaidi kuliko wanaume. Wanawake wamekuwa wanajihusisha na shughuli ndogo ndogo za kibiashara ama shughuli za nyumbani zikiwaacha bila akiba ya uzeeni, na hivyo kukosa ulinzi wa kuwa kwenye mfumo rasmi wa pensheni.

Ni vizuri sana kuwe na elimu bora ya fedha kwa uzee ambayo inapaswa kuzingatia mambo kadhaa muhimu ikiwa ni pamoja na namna pensheni zinavyotolewa. Kwa mfano namna ya kuweka akiba ya uzeeni na namna ambavyo unaweza kutumia mafao ya uzeeni.

Ni muhimu kuwa na mbinu mbali mbali na walengwa kuhimizwa kuelewa umuhimu wa akiba, kujenga tabia njema ya kujiandaa kifedha uzeeni pamoja na ulewa wa mipango ya kifedha, bajeti na akiba ya dharura, gharama za afya na bima, usimamizi wa madeni, na ulinzi dhidi ya ulaghai unaoweza kufanyika kwa wastaafu, hasa kupitia mipango ya kilaghai ya kuwekeza na kupata faida kubwa na za haraka.

Ni vizuri kama mtu binafsi kuweza kuchukua hatua za haraka na mahususi ikiwa ni pamoja na kuanza mapema kutenga akiba, na kugawa uwekezaji kulingana na umri na uwezo wa kubeba hatari; na kujenga uhimilivu wakati wa uzee, bila kuathiri hali ya maisha kabla ya kustaafu.

Ni vizuri kujifunza ujasiriamali na kuwa na biashara ndogo kwa waajiriwa mapema kuliko wakati wa kustaafu.