NIKAYAKATISHA yale mazungumzo yetu.
“Sasa shoga subiri nikupeleke kwa gari.”
“Itakuwa vyema shoga. Kila saa kukodi bodaboda, hizo hela ziko wapi? Wanaume wenyewe ndio hao wanaokimbia wake zao,” Raisa alisema kisha akacheka.
Nikaingia chumbani na kuvaa nguo za kutokea. Nilichukua funguo ya gari. Nikazunguka kwa mlango wa nyuma na kulitoa gari langu ambalo huwa naliweka kwenye banda.
Raisa pia nilimtoa kwa mlango wa nyuma nikampakia kwenye gari. Nilipolitoa gari hilo nililisimamisha. Nikafunga geti la nyuma kisha nikarudi kwenye gari na kuondoka. Ule upande uliokuwa na gari la Shefa niliukwepa, nikapita upande mwingine.
“Mbona unapitia upande huu?” Raisa akaniuliza.
“Nakwepa mashimo. Upande huo una mashimo mengi, yananiharibia gari,” nikamdanganya.
Raisa akanikubalia kwa kichwa.
“Shoga umehangaika bure kuja huku. Ungenipigia simu kule kule tu,” nikamwambia Raisa huku nikiendesha.
“Ningejua bora ningekupigia tu. Nimeharibu pesa yangu bure.”
“Siku nyingine unaponihitaji, kama sipo, nipigie simu tu nitakuja mimi.”
“Wakati mwingine si nakuja kukusalimia?”
“Nipigie simu kwanza ujue niko wapi. Wakati mwingine sipo nyumbani.”
Nilimwambia hivyo kusudi asije tena pale nyumbani mpaka nitakapopata ufumbuzi wa kuiondoa ile maiti ya Shefa pamoja na lile gari lake.
Nilimfikisha Raisa saluni nikamuagiza mfanyakazi wangu mmoja anayeitwa Susana amsuke rasta Raisa. Suzana alikuwa akishughulikia mteja mwingine. Nilipomwambia hivyo, alimuachia mwenzake mteja huyo, akamshughulikia Raisa.
Mimi sikuwa na moyo wa kukaa pale saluni. Nikawaacha na kurudi nyumbani.
Sikuliingiza gari kwenye banda, nikaliegesha nje na kuingia ndani. Nilifikiria kuchemsha chai. Nikanywa chai tupu bila kitafunio.
Ile chai ilinichangamsha kidogo, nikakaa kwenye kochi na kuendelea kuwaza. Akilini mwangu kulikuwa na wazo moja tu: la kwenda kuliondoa lile gari la Shefa na kuliegesha mahali pengine.
Niliinuka na kwenda kulichungulia gari hilo kwenye dirisha. Kitu ambacho kilinitia wasiwasi ni kuwa barabara ile ilikuwa imechangamka sana. Kulikuwa na watu waliokuwa wanapita wakati wote. Isitoshe, watu wengine walikuwa wamesimama karibu na lile gari wakiwa na hamsini zao.
Hali ile ilinifanya nisite kwenda kuliondoa gari hilo kwani wakati nikiliondoa sikutaka kuonekana na mtu yeyote. Nikajiambia pengine wakati wa jioni watu watakuwa wamepungua.
Nikaondoka dirishani na kuingia chumbani ambako nilijiulaza kitandani.
Hapo kitandani niliendelea kuwaza hili na lile. Nikajiambia kwamba endapo nitakamatwa kutokana na kuuawa kwa Shefa nyumbani kwangu, utakuwa ndiyo mwisho wangu kwa vile nilifahamu kesi za mauaji hazina msalie mtume. Ukikamatwa unaweza kufia jela kabla hata ya kesi kufikishwa mahakamani. Uchunguzi wa kesi hizo huchukua muda mrefu.
Suala la msingi, nikaendelea kujiambia, ni kuendelea kujitahidi kuziondoa tuhuma za kuuawa kwa Shefa karibu yangu. Kama nitafanikiwa kuliondoa gari lake na kuihamisha maiti yake, ni nani atakayenituhumu mimi kuhusu kuuawa kwake? Nikajiuliza.
Hilo ndilo jambo ambalo nilikuwa nimepanga kulipigania ili kunusuru maisha yangu.
Kwa upande mwingine, nikajiuliza, huyo aliyemuua Shefa alikuwa na dhamiri gani? Alikuwa na kisasi na Shefa mwenyewe au alitaka kunikomoa mimi?
Kama alikuwa na kisasi na Shefa, nikaendelea kujiuliza, ni kwa nini alikuja kumuulia nyumbani kwangu tena siku ile ambayo tumepanga kutenda dhambi?
Na kama alikuwa na kisasi na mimi, ni kwa nini asije kuniua mimi mwenyewe, amuue mgoni wangu?
Hapo sikupata jibu kabisa. Mawazo yalipozidi kichwani mwangu, nikapitiwa na usingizi hapo hapo. Nikalala fofofo.
Nilipokuja kuzinduka, nilitazama saa yangu na kuona ilikuwa saa kumi na mbili jioni, tena mvua ilikuwa inanyesha. Nikainuka na kwenda kuoga. Nilipomaliza, nilivaa nikaenda kuuchungulia mwili wa Shefa. Wakati nautazama, nilijiambia, ama kweli mshahara wa dhambi ni mauti.
Pengine Shefa asingeuawa kama asingekuja kwangu usiku ule. Pia nikajiambia, kama mshahara wa dhambi ni mauti, bado mauti yangu mimi. Nitakapokamatwa ni lazima nitahukumiwa, na hukumu ya kosa la mauaji ni kunyongwa kwa kitanzi mpaka ufe.
Sikutaka kuwaza zaidi. Nikaufunga mlango wa stoo na kurudi chumbani kwangu. Nikataka nimpigie simu mke wa Shefa nimuulize amefikia wapi, lakini nilisita. Niliona kama vile anaweza kunishitukia kwamba ninahusika na kupotea kwa mume wake. Nikaamua kuacha kumpigia hadi hapo atakaponipigia mwenyewe.
Niliendelea kuhaha hadi saa mbili usiku ambapo nilitarajia huko nje kungekuwa kutulivu ili niweze kuliondoa gari la Shefa. Muda huo kulikuwa kutulivu lakini yule mlinzi ambaye sikutaka anione wala anijue, alikuwa ameshafika.
Nikajiambia sitaweza tena kutimiza azma yangu ya kulihamisha gari la Shefa usiku huo na kwamba gari hilo litaendelea kubaki pale pale hadi asubuhi.
Wakati nawaza hivyo, mfanyakazi wangu wa saluni aliyeitwa Susana akanipigia simu.
“Unataka kufunga?” nikamuuliza kwenye simu.
“Nilikuwa nataka kujua kama utakuja,” sauti ya Susana ikasikika.
“Mimi sitakuja, kama unataka kufunga, funga tu.”
“Basi acha nifunge kwa sababu mvua inanyesha na hatuna wateja.”
“Wewe funga tu, tutaonana kesho asubuhi.”
“Asubuhi utakuja?”
“Nitakupigia simu. Kama nitakuja nitakwambia.”
“Sawa dada. Basi acha nifunge.”
“Sawa.”
Susana akakata simu.
Simu ilipokatwa tu, mke wa Shefa akanipigia. Moyo wangu ulishituka kidogo. Nikaipokea ile simu.
“Habari ya saa hizi?” mke wa Shefa akaniuliza.
“Nzuri, sijui wewe?”
“Mimi bado tupu kama mwenyewe hatakwenda kuliondoa.”
“Sasa utafanyeje?”
“Mimi sina la kufanya. Hilo lori ni lake mwenyewe. Mimi halinihusu. Hata kama litaibiwa, atajua mwenyewe.”
“Mmh… hiyo ni hasara sasa!”
“Ni hasara ndiyo, lakini atajua mwenyewe. Polisi wameniambia kama mume wangu hatatokea usiku huu, niende kituo cha polisi kesho asubuhi.”
“Sasa utakwenda?”
“Nitakwenda kuwasikiliza.”
Baada ya kuagana na mwanamke huyo kwenye simu, wazo la kuihamisha maiti ya Shefa pale nyumbani likanijia tena akilini mwangu. Nikajiambia kuwa hata mume wangu akirudi ghafla anaweza kuikuta. Pia, kama itaendelea kukaa kwa muda mrefu, itaharibika kutokana na joto liliomo katika kile chumba na inaweza kutoa harufu ya kusikika.
Kitu ambacho kilinitia hofu zaidi ni kusikia kuwa polisi walikuwa wakimtafuta Shefa kwa juhudi.
Sikutaka ile maiti ikae mle ndani hadi asubuhi. Nikafikiria kuwa niitoe usiku ule ule na kwenda kuitupa mahali popote ambapo sitaonekana, hata kama ni nje ya mji.
Nikajiuliza, nitaitoa vipi mle ndani bila kuonekana na watu? Nikapata jibu kwamba niingize gari kwenye banda, kisha niitoe maiti hiyo kwa mlango wa nyuma na kuitia kwenye gari hilo, kisha nilitoe gari na kufunga geti.
Baada ya hapo, niliendelea kujiambia, nitafute sehemu ya kwenda kuitupa.
Nikapanga nisubiri hadi saa sita usiku ambapo kutakuwa kumetulia ndipo nifanye kazi hiyo. Nikasubiri.
Wakati nasubiri, nilitoka nikaliingiza gari langu ndani ya banda. Mvua ilikuwa imeacha kunyesha. Baada ya kuliingiza gari, nikaenda kukaa sebuleni hadi saa sita. Nikachungulia nje kupitia dirishani. Nikaona kulikuwa kutulivu. Nikaenda kule stoo na kuishika miguu ya Shefa na kumburuza kumtoa uani.
Mwili wake ulikuwa umekakamaa kama vile haukuwa mwili wa binadamu. Kuishika ile miguu tu, ilibidi nijikaze kwa vile sikuwa na jinsi. Maiti inatisha, asikwambie mtu.
Hata hivyo, kwa kutumia ujasiri wangu niliweza kuiburuza hadi uani kunako banda la gari, nikaiweka chini kisha nikajiuliza, maiti hiyo niiweke wapi? Niilaze kwenye siti ya gari au niiweke kwenye buti la nyuma kama mzigo?
Nikapata jibu kuwa niilaze kwenye siti. Nilijiambia, kama nitaiweka kwenye buti ikitokea bahati mbaya nikakutana na askari akalitilia shaka gari langu na kulipekua, sitakuwa na jibu endapo ataona nimeweka mtu aliyekufa ndani ya buti.
Lakini kama nitailaza maiti hiyo kwenye siti, naweza kusema kuwa ni mgonjwa namuwahisha hospitali.
Nikafungua mlango mmoja wa siti ya nyuma nikaingia, kisha nikaishika tena miguu ya Shefa na kuivutia ndani ya gari. Sikuweza kumuinua mzima mzima kwa sababu alikuwa mzito.
Miguu ilipoingia kwenye gari nikaanza kuingiza kiuno. Nilimshika kwenye mkanda wa suruali yake nikamvuta mpaka mwili wote ukaingia kwenye gari. Baada ya kuulaza vizuri kwenye siti, niliikunja miguu yake. Miguu ilikuwa imekakamaa, imekataa kukunjika. Nikaikunja kwa nguvu kisha nikafunga mlango.
Nilikwenda kufunga nyumba yangu kisha nikafungua geti na kulitoa gari. Nikasimamisha gari mbele ya geti na kwenda kulifunga geti hilo. Nilipomaliza, nilirudi kwenye gari na kuliondoa.
Sikujua ni ujasiri wa kiasi gani nilioupata kiasi kwamba niliweza kuliendesha gari hilo huku nikijua kuwa nilikuwa nimebeba maiti ya mtu anayetafutwa na mke wake pamoja na polisi, mtu ambaye kama nitakamatwa naye, moja kwa moja ninakabiliwa na kosa la mauaji.
Usiku huo, barabara za Tanga zilikuwa tupu na kimya. Pikipiki moja moja ndizo zilizokuwa zikipita barabarani kwa mwendo wa kasi. Niliomba Mungu nisikutane na gari la polisi lililoko kwenye doria. Polisi hao wangeweza kunisumbua na kukatisha azma yangu ya kuihamisha maiti ya Shefa nyumbani kwangu.
Wakati natoka nyumbani sikuwa nimepanga nikautupe wapi mwili huo. Sasa nikawa najiuliza, niende nao wapi mwili huo ambao nilitakiwa nisiwe nao kwenye gari kwa muda mrefu?
Sikupata jibu la haraka. Nikawa naendesha gari taratibu huku nikiwaza. Katika kuzunguka na gari, nikatokea kwenye makaburi ya Msambweni.
Nilipoyaona yale makaburi, nikajiambia bora niitupe maiti hiyo kwenye makaburi hayo kwa vile palikuwa mbali na mtaa niliokuwa ninaishi. Isitoshe, niliona hapo ndiyo mahali muafaka wa kuiacha maiti ile.
Bado Watatu – 25 | Mwanaspoti
