Profesa Ndoto awapigia chapuo vijana wa Veta

Dodoma. Makandarasi wanaojenga majengo makubwa wameagizwa kutenga nafasi za kuwachukua wanafunzi wanaosoma katika Vyuo vya elimu na mafunzo ya ufundi stadi (Veta), ili kujifunza kwa vitendo.

Wito huo umetolewa jana  Septemba 10, 2025 na Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Carolyne Ndombo alipotembelea na kukagua jengo la makao makuu ya Tume ya Sayansi na Teknolojia (Costech) linalojengwa eneo la Tambukareli Jijini Dodoma.

Costech wanajenga jengo hilo kwa gharama ya Sh7.3 bilioni na linatarajia kuchukua zaidi ya watu 600 kwa wakati mmoja litakapokamilika Machi 2026, huku wakilengwa vijana wabunifu  wanaochipukia.

Profesa Ndombo amesema kitendo cha kujenga majengo ya Serikali lakini hakiwahusishi vijana wanaoandaliwa kwa ajili ya kuwa mafundi si uungwana na kinaondoa muunganiko kutoka hatua moja kwenda nyingine.

“Wale vijana wanasoma mambo ya ufundi, hivi mkiwaleta hapa watashindwa hata kuchanganya zege, kazi zote za vibarua wapewe maana ni sehemu ya darasa na pale mnapolipa posho walipeni na wao, naamini makandarasi mmenielewa katika hilo nataka lianze sasa,” amesema Ndombo.

Akizungumzia kuhusu jengo hilo, amesema ndilo litakalokuwa makao makuu ya Tume hiyo na lile jengo la makao makuu kwa sasa lililopo Jijini Dar es Salaam litakuwa ni jengo la kijiji cha wabunifu.

Katibu amesisitiza jengo kukamilika kwa wakati na ubora ili liendane na thamani kama ilivyoainishwa kwenye Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET), ambao ndiyo waliotoa fedha za ujenzi wa mradi huo.

Mkurugenzi Mkuu wa Costech, Dk Amos Nundu amesema bunifu nyingi za vijana ambao wanapitia kwao zimekuwa na mafanikio makubwa, hivyo Serikali iliamua kupanua wigo kwa kujenga jengo kubwa la kisasa ambao litakuwa na uwezo wa kuwaweka watu wengi kwa wakati mmoja.

Dk Nundu amesema hakuna kijana atakayetozwa fedha pindi anapotaka kutumia jengo hilo kwa ajili ya kuonyesha kipaji chake na kupewa usaidizi, kwani ndiyo maana halisi ya kuwa na kituo cha pamoja cha kuwainua ili nao waweze kutambulika na kutimiza ndoto zao.

Mkurugenzi amesema jengo la kijiji cha ubunifu litakalokuwa Dar es Salaam watabaki watumishi pia na kutakuwa na mahusiano ya moja kwa moja na makao makuu kwa ajili ya kuwaendeleza vijana wote wanaofikia viwango katika bunifu zao ambapo hutumiwa kwa kipindi cha miaka miwili, kisha wanakuwa na uwezo wa kuendeleza miradi yao na akasema wengi wamefanikiwa kupitia njia hiyo.