Mikoa hii kupata mvua pungufu za vuli, tahadhari magonjwa ya milipuko yatolewa

Dar es Salaam. Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetangaza utabiri wa msimu wa vuli unaoanza Oktoba hadi Desemba, ikiitaja mikoa saba kupata mvua pungufu.

Akitangaza utabiri huo leo Septemba 11, 2025, jijini Dar es Salaam,  Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dk Ladislaus Chang’a amesema mvua zinatarajiwa kuwa za wastani hadi chini ya wastani katika maeneo mengi.

Amesema zinatarajiwa kuanza wiki ya kwanza na ya pili ya Oktoba, 2025 katika maeneo ya Mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, Mara na kaskazini mwa Mkoa wa Kigoma, na kisha kusambaa katika maeneo ya mikoa ya Simiyu na Shinyanga katika wiki ya nne ya Oktoba, 2025.

Katika wiki ya kwanza na ya pili ya Novemba 2025, mvua zinatarajiwa kuanza katika maeneo ya nyanda za juu kaskazini mashariki na pwani ya kaskazini, zikitarajiwa kuisha Januari, 2026 katika maeneo mengi.

Dk Chang’a amesema msimu huu unatarajiwa kutawaliwa na vipindi virefu vya ukavu na mtawanyiko wa mvua usioridhisha, hususan katika maeneo ya pwani ya kaskazini

na nyanda za juu kaskazini mashariki akibainisha kwamba ongezeko la mvua linatarajiwa kujitokeza Desemba, 2025 katika maeneo mengi.

Amesema mbali na mvua za wastani hadi chini ya wastani zinazotarajiwa katika maeneo mengi, pia kutakuwa na vipindi vya joto kali kuliko kawaida.

Amesema joto la bahari la wastani hadi chini kidogo ya wastani linatarajiwa katika eneo la tropiki ya kati ya Bahari ya Pasifiki.

“Aidha, joto la bahari la wastani linatarajiwa magharibi mwa Bahari

ya Hindi (Pwani ya Afrika Mashariki) ikilinganishwa na joto la bahari la juu kidogo ya wastani upande wa mashariki.

“Hali hii inatarajiwa kupunguza kasi ya msukumo wa hewa yenye unyevunyevu kutoka Bahari ya Hindi kuelekea maeneo ya ukanda wa pwani pamoja na maeneo ya jirani,” amesema.

Amefafanua kuwa kwa upande mwingine, joto la bahari la wastani hadi chini kidogo ya wastani linatarajiwa katika eneo la pwani ya kusini mashariki mwa Bahari ya Atlantiki (Pwani ya Angola).

“Hali hii inatarajiwa kuimarisha msukumo wa hewa yenye unyevunyevu kutoka misitu ya Congo kuelekea maeneo ya magharibi.

Akitaja athari zinazotarajiwa katika msimu huu, Dk Chang’a  amesema ni upungufu wa unyevunyevu katika udongo unatarajiwa kujitokeza katika maeneo mengi na hivyo kuathiri shughuli za kilimo.

“Pia kunatarajiwa kupungua kwa kina cha maji katika mito, mabwawa na hifadhi ya maji ardhini, kunatarajiwa kujitokeza kwa magonjwa ya mlipuko, kutokana na upungufu wa maji safi na salama,” amesema Dk Chang’a.

Ametoa tahadhari kwa sekta mbali zikiwamo za maafa kushirikiana na wataalamu ikiwemo wa hali ya hewa ili kukabiliana na athari zinazoweza kujitokeza.

Pia ametoa angalizo la kuwapo matukio ya hali mbaya ya hewa ikiwemo vipindi vya mvua kubwa hata katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za wastani hadi chini ya wastani.

Amesema wadau wa sekta mbalimbali za kiuchumi na kijamii wanashauriwa

kupanga na kutekeleza shughuli zao kwa kuzingatia taarifa mahususi za hali ya hewa zinazotolewa na TMA.

Akigusia kwenye kilimo na usalama wa chakula, amesema maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za wastani hadi chini ya wastani yanaweza

kukumbwa na upungufu wa unyevu, ambao unaweza kuathiri ukuaji wa mimea na kusababisha upungufu wa mavuno hususan kwa mazao yanayotegemea mvua.

Pia, kuna uwezekano wa ongezeko la wadudu waharibifu kama vile panya na mchwa.

 Aidha, vipindi  vya unyevu wa kuzidi kiasi pamoja na mafuriko vinaweza kujitokeza na kuathiri ukuaji wa

mazao katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za wastani hadi juu ya wastani.

Katika mifugo na uvuvi amesema katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za wastani hadi chini ya wastani upungufu wa maji unaweza kujitokeza na hivyo unaweza kuathiri upatikanaji wa maji na malisho ya mifugo, hivyo kusababisha migogoro kati ya wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi.

Katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za wastani hadi juu ya wastani, wafugaji na wavuvi wanatarajiwa kunufaika na upatikanaji wa malisho, maji na chakula cha samaki.

“Hata hivyo, milipuko ya magonjwa ya mifugo kama vile homa ya bonde la ufa, ugonjwa wa miguu na

midomo, na kuzaliana kwa wadudu wanaodhuru mifugo kunaweza kujitokeza.

Wafugaji wanashauriwa kuweka mipango mizuri ya matumizi na uhifadhi wa maji na vyakula

Kwenye sekta ya afya, Dk Chang’a amesema maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za wastani hadi chini ya wastani, jamii inaweza kulazimika kutumia maji yasiyo safi na salama hivyo hatua stahiki za kiafya zinashauriwa kuzingatiwa ili kupunguza athari zinazoweza kujitokeza.

Amefafanua hali hiyo itakuwa tofauti kwenye  maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za wastani hadi juu ya wastani, uharibifu wa miundombinu ya maji unaoweza kusababishwa na maji ya mvua kutuama na kutiririka katika makazi ya watu, unaweza

kusababisha uchafuzi wa maji na hivyo kusababisha kutokea kwa magonjwa ya mlipuko.

Katika sekta binafsi, amesema shughuli za kilimo biashara na uzalishaji viwandani zinaweza kuathirika kutokana na upungufu wa malighafi za kilimo utakaotokana na upungufu wa mvua hususani kwenye maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za wastani hadi chini ya wastani.

kusababisha ongezeko la gharama za upatikanaji wa malighafi na uendeshaji. Aidha, upungufu wa mvua unaweza kuathiri ubora wa bidhaa mfano miti ya nguzo, mbao, nyama na asali.

Kwenye taasisi za benki, mikopo na bima zinashauriwa kuandaa na kutoa huduma mahususi kwa wadau

ili kujenga ustahimilivu katika biashara.

“Idara ya usimamizi wa maafa, kwa kushirikiana na wadau mbalimbali nchini, inashauriwa kuendelea

kuratibu na kutekeleza mipango ya kupunguza athari zinazoweza kujitokeza,”amesema.