Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam | 10 Septemba 2025
Tanzania iko katika hatua ya mageuzi ya viwanda ambayo huenda ikafungua fursa ya mapato ya ziada ya hadi dola bilioni 11.7 kwa mwaka pamoja na kuzalisha ajira zaidi ya 25,000, kwa mujibu wa ripoti iliyowasilishwa katika mkutano wa ngazi ya juu wa CEO Roundtable of Tanzania (CEOrt) uliofanyika jijini Dar es Salaam tarehe 9 Septemba 2025.
Kupitia kaulimbiu “Kufanikisha Uzalishaji Afrika: Mnyororo wa Thamani wa Madini hadi Uzalishaji,” kikao hicho kiliwaleta pamoja viongozi wa sekta binafsi, watunga sera waandamizi, wawakilishi wa kidiplomasia, na washirika wa kimkakati katika hoteli ya Hyatt Regency Kilimanjaro, Dar es Salaam, kwa lengo la kujadili namna Tanzania inavyoweza kupanda juu kwenye mnyororo wa thamani wa madini kwa kuchakata madini ndani ya nchi badala ya kuyauza ghafi.
Kwa mujibu wa utafiti mpya uliofadhiliwa na Uingereza kupitia mpango wa Manufacturing Africa, uliotekelezwa na kampuni za McKinsey & Company na BDO, kwa ushirikiano na ASNL Advisory. Ripoti hiyo imebaini fursa 14 zenye matokeo makubwa ya uwekezaji katika aina 11 ya madini nikiwemo dhahabu, grafiti, madini adimu, nikeli, shaba, kobalti, chokaa na fosfati.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Tanzania inaweza kuongeza mapato yake ya kiuchumi na ushindani wa viwanda kwa kubadilisha madini ghafi kuwa bidhaa zenye thamani kama saruji, vigae, glasi, dhahabu iliyosafishwa, vito vya dhahabu, na madini ya betri ambayo ni muhimu katika mabadiliko ya dunia kuelekea uchumi wa kijani.
Akizungumza katika tukio hilo lililodhaminiwa na Kioo Limited, Balozi wa Uingereza nchini Tanzania, Bi. Marianne Young, alisema kuwa Tanzania imejaaliwa kuwa na madini mengi yenye thamani ambayo yatawanufaisha wananchi wake, huku akithibitisha kuwa Uingereza itaendelea kuiunga mkono Tanzania katika juhudi zake za kuimarisha viwanda kupitia mnyororo wa thamani wa madini.
“Majadiliano haya yanakuja wakati muhimu sana kwa Tanzania. Kwa utajiri mkubwa wa madini ulionao, nchi hii inaweza kuwa kitovu cha uzalishaji kwa ukanda huu na mshiriki muhimu katika uchumi wa kijani duniani,” alisema Bi. Young.
“Kupitia ushirikiano wa pamoja na mpango wa Uzalishaji Afrika ‘Manufacturing Africa’, Uingereza imejidhatiti kushirikiana na sekta binafsi na serikali ya Tanzania ili kubadilisha fursa hii kuwa ajira endelevu, ukuaji jumuishi, na ustawi wa muda mrefu.”, amesema.
Amelisifu jukwa la Watendaji Wakuu (CEOrt) hapa nchini kwa kuandaa majadiliano yenye tija ambayo yanaonyesha namna rasilimali za madini zinavyoweza kuchochea ndoto ya Tanzania ya kuwa taifa la viwanda, na kusaidia juhudi za serikali.
Mwenyekiti wa CEOrt, David Tarimo, alisisitiza umuhimu wa Tanzania kutoka kwenye utegemezi wa kuuza madini ghafi na kuelekea kwenye uchakataji wa ndani kama njia ya kufanikisha ukuaji wa kiuchumi wa kudumu na jumuishi.
“Sekta ya madini inachangia takribani asilimia 10 ya Pato la Taifa (GDP), huku dhahabu peke yake ikichangia karibu asilimia 80 ya mauzo ya madini nje ya nchi. Tunaona fursa zaidi ya hapa na kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha viwanda vya uchakataji vinavyolenga masoko ya nje,” alisema Tarimo.
“Kwa kipindi cha robo karne tangu kuanzishwa kwake, CEOrt imekuwa ikileta pamoja viongozi kupitia sekta binafsi kushiriki katika mchakato wa maboresho ya sera na kipaumbele cha kitaifa. Kikao hiki kinaonyesha kuwa sekta binafsi na serikali wanaweza kuendelea kushirikiana kujenga taifa lenye ushindani zaidi.”
“Ikiwa tutaimarisha uboreshaji wa mnyororo wa thamani wa madini, tutaongeza mapato na pia kujenga kitovu cha uzalishaji kinacholingana na mustakabali wa uchumi wa kijani Afrika. Utajiri wa madini wa Tanzania unaweza kuendesha maendeleo kwa miaka 25 ijayo kulingana na Dira ya Maendeleo ya 2050, ikiwa tutapa kipaumbele kwenye ongezeko la thamani,” aliongeza.
Wajumbe wa jukwaa la CEOrt linalojumuisha zaidi ya kampuni 200 za sekta binafsi walitoa wito kwa kuandaliwa miradi ya uwekezaji wa viwanda vya mnyororo wa thamani wenye tija, huku wakitaka kuendelezwa kwa ushirikiano na serikali ili kuendeleza mchakato huu wa mageuzi ya viwanda.
Mjadala wa wazi uliosimamiwa na Bi. Anna Rabin, Mkurugenzi Mtendaji wa Above Ground Advisory na Balozi wa Heshima wa Australia nchini Tanzania, uliangazia namna sekta binafsi inaweza kunufaika na fursa katika viwanda vinavyohusiana na madini.
Washiriki walionyesha ongezeko la mahitaji ya bidhaa kama saruji, vito vya dhahabu, vigae, na vifaa vya betri katika soko la kikanda na kimataifa, huku wakihimiza sera thabiti na mazingira bora ya uwekezaji yanayounga mkono ongezeko la thamani ya madini.
Leonard Mususa, mjumbe wa CEOrt na Mwenyekiti wa Bodi ya Tanzania Breweries Limited, alisisitiza umuhimu wa ushirikiano na hatua madhubuti katika kufanikisha ajenda ya kuchakata madini ndani ya nchi.
“Tanzania iko kwenye nafasi nzuri kuvutia uwekezaji katika sekta ya viwanda vinavyotokana na madini,” alisema.
“Lakini ili kufanikisha hili, tunahitaji miradi yenye tija, sera thabiti, na maendeleo ya wajasiriamali wa ndani.”
“Kwa kuunganisha mtaji, ushirikiano, na utetezi wa sera, Tanzania inaweza kupata thamani kubwa zaidi kutokana na utajiri wake wa madini,” aliongeza.
Bw. Terence Ngole, Kaimu Kamishna wa Madini kutoka Wizara ya Madini, alitumia nafasi hiyo kuonyesha kuwa serikali imejipanga kuendeleza ushirikiano na sekta binafsi ili kusukuma mbele uchakataji wa ndani na utofauti wa uchumi.
“Tumeendelea kushirikiana kwa karibu na sekta binafsi kuona namna sekta ya madini inaweza kuchangia zaidi katika Pato la Taifa, kupunguza utegemezi wa kuuza ghafi, kuimarisha msingi wa viwanda, na kutoa ajira kwa vijana wengi nchini,” alisema.
“Tunajivunia ushirikiano wetu wa muda mrefu na CEOrt na tunaamini kuwa kwa pamoja tunaweza kutekeleza mapendekezo haya na kugeuza utajiri wa madini wa Tanzania kuwa msingi wa ustawi wa kweli kupitia ongezeko la thamani na uzalishaji wa ndani,” alihitimisha.
Sehemu ya wadau mbalimbali walioshiriki katika mjadala huo.