DK.SAMIA AAHIDI SERIKALI KUENDELEA NA MWENDO ULE ULE UTEKELEZAJI MIRADI YA MAENDELEO

Na Said Mwishehe,Michuzi TV- Tabora.

MGOMBEA Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Rais Dk.Samia Suluhu Hassan ameahidi katika miaka mitano ijayo Serikali itakwenda ma mwendo uleule kutekeleza miradi ya maendeleo ya jamii ya elimu, afya, umeme na maji.

Dk.Samia ameyasema hayo leo Septemba 11,2025 alipokuwa akihutubia maelfu ya wananchi wa Wilaya ya Uyui Mkoani Tabora ambapo amefanya mkutano wa hadhara kwa ajili ya kuelekea Uchaguzi Mkuu unaotarajia kufanyika Oktoba 29 mwaka huu.

Wakati anazungumza na wananchi hao Mgombea Urais Dk.Samia Suluhu Hassan licha ya kuelezea mambo makubwa ya maendeleo yaliyopatikana katika miaka mitano iliyopita kupitia utekelezaji wa Ilani lakini katika sekta ya elimu,afya,umeme na maji Serikali itakwenda na mwendo uleule.

“Kwa sababu tunajua jinsi watu wetu wanavyokuwa na mahitaji yanaongezeka. Katika mahali tutamaliza haja ya umeme tutakapounganisha vitongoji vyote kwa umeme kitakachobaki ni kuunganisha katika nyumba za watu.

“Na huo ndiyo utashi wa watu anayetaka mwenye uwezo akaunganisha umeme wake basi tanesco kupitia wakala wake wa umeme vijijini watakwenda kuunganisha.

“Kwenye maji kadri tunavyoongezeka mahitaji ya maji yanaongezeka, afya na elimu ni hivyo hivyo. Tutaendelea kujenga madarasa lakini tutajenga vyuo vya veta vilevile ili kuwapa vijana wetu ujuzi wa fani mbalimbali.

Alisema: “Kubwa zaidi tunakusudia kuweka viwanda vidogo ambavyo vitawafanya vijana wetu waweze kuongeza thamani kwa kuchakata mazao yanayozalishwa kwenye wilaya ili kutengeneza ajira kwa vijana.” 

Alieleza kuwa kwa sababu hiyo serikali inafahamu umeme unahitajika kwa kiasi kubwa na ajira zitapatikana kwa vijana.