Dodoma. Kampeni za Mgombea Ubunge wa Jimbo la Mtumba, Anthony Mavunde zimevuta watu wengi huku wananchi wakitamani viongozi wengine kufanya kama anavyofanya ushawishi kwa mtindo huo.
Mavunde ambaye ni Waziri wa Madini, leo Alhamisi Septemba 11, 2025 anaingia siku ya nane katika kampeni zake akitembelea makundi ya mama lishe, bodaboda, wajasiriamali na viongozi wa dini katika maeneo yao kisha kuzungumza nao, ambapo sehemu kubwa kampeni ni za maswali na majibu.
Jimbo la Mtumba lenye kata 20 lilizaliwa kutoka Jimbo la Dodoma ambalo kwa upande huo zilibaki kata 21 na mgombea wake ni Paschal Chinyele.
“Nitafanya kampeni za nyumba kwa nyumba, nitapitia makundi maalumu na kuzungumza nao, lakini nitatamani kufika maeneo magumu ili nijionee mwenyewe, nasema kote nitafika maana nilikuwa na kata 41 na zote niliweza sasa leo nikiwa na kata 20 nitashindwa nini,” alihoji Mavunde siku ya uzinduzi wa Kampeni zake Septemba 3, 2025 katika Kata ya Ipagala.

New Content Item (1)
Jana ilikuwa ni zamu ya Kata ya Makole ambako mgombea huyo alifika saa mbili asubuhi na kuhitimisha ziara yake saa 11 jioni, akipitia katika mitaa yote huku akiwa na msafara wa watu wachache.
Mwenyekiti wa CCM wa Kata ya Makole, Omari Chambala amesema aina ya kampeni anazofanya kiongozi huyo imegeuka kuwa kivutio kutokana na mbinu ya ushawishi na jinsi anavyopenya kwenye makundi ya watu ambao huwa hawafiki kwenye mikutano ya hadhara, lakini anakaa nao na kuzungumza nao.
“Huyu jamaa ni kiboko, ujue watu wanakuwa na madukuduku lakini anawapa nafasi ya kuzungumza mambo mengi na kuuliza maswali kisha anawajibu karibu wote wanafurahi, kwa kweli kampeni hii sijapata kuona huenda atakuwa na mwisho mzuri,” amesema Chambala.
Amesema katika Kata ya Makole kumekuwa na kero kubwa ya miundombinu ya barabara za ndani ikiwemo mitaro, mikopo kwa wajasiriamali ikiwemo mama lishe na vijana lakini wengi wamepewa majibu ya takwimu na wameonyesha kuridhika kwa kiasi kikubwa.
Akizungumzia kampeni hizo Mavunde amesema ni uamuzi wake kutaka kujua shida wanazoishi nazo wapiga kura wake ili naye awe sehemu ya utumishi katika kuzitatua, kuliko kufika kwenye maeneo ya wazi akapiga maneno kisha anakwenda kupumzika.
Mavunde amesema katika kipindi hiki cha awamu ya tatu ya ubunge wake, atakuwa muumini wa kushuka chini na kuzungumza na wananchi wake hasa baada ya kugundua kuna changamoto nyingine hazihitaji nguvu kubwa kuzitatua, lakini zinabaki kwenye manung’uniko kwa sababu hazifikishwi kwa wakati unaotakiwa.

New Content Item (1)
“Niliomba ubunge ili niwe sehemu ya utumishi, lakini natafuta kura za Rais na madiwani wangu ili tukiingia nitakuwa nimezibeba shida za watu hawa moja kwa moja pasi na kudanganywa,” amesema Mavunde.
Hata hivyo ameeleza kuwa kampeni hizo hazitaishia hapo tu bali zitakwenda majukwaani baada ya kumaliza maeneo yote, na atakapoanza mikutano ya majukwaani anaona itakuwa rahisi kuzungumza na watu kwa lugha moja kwa kuwa wengi anajua hata maeneo wanayoishi na shughuli wanazozifanya.