Mgombea udiwani aahidi kujenga barabara, kufunga taa za kisasa

Mbeya. Mgombea udiwani Kata ya Isanga jijini Mbeya, Dourmohamed Issa ameomba wananchi kumpa ridhaa katika kipindi kingine cha miaka mitano, kwa lengo la kukamilisha miradi ya maendeleo na kusogeza huduma muhimu kwa jamii.

Ametaja miongoni mwa miradi ni pamoja na ujenzi wa miundombinu ya barabara sambamba na kufunga taa za kisasa kwenye barabara ya Mbwiga, ambayo tayari imejengwa kwa kiwango cha lami.

Issa ambaye alikuwa Mstahiki Meya Jiji la Mbeya kwa miaka mitano iliyopita, amesema hayo jana Septemba 10, 2025 kwenye uzinduzi wa mkutano wa kampeni na kubainisha akipata ridhaa miradi itakamilika kwa wakati lengo ni kuchochea shughuli za kiuchumi.

“Natambua changamoto yenu ya barabara ndugu zangu katika kipindi cha miaka mitano nimetekeleza ahadi zangu kupitia ilani ya uchaguzi 2020/2025 kwa kujenga barabara hususan zahanati na ukarabati wa shule za msingi tatu kwa kutumia mapato ya ndani ya halmashauri,” amesema.

Ametaja fedha zilizotumika kutekeleza miradi hiyo ni pamoja na ujenzi wa zahanati Sh116 milioni, Ofisi ya mtaa Sh34 milioni, ukarabati shule za msingi Isanga, Igoma na Ilolo ambapo zaidi ya Sh140 milioni zilitumika.

Aidha, ameomba wananchi kuchagua mafiga matatu katika kuelekea Uchaguzi Mkuu Oktoba 29, 2025 kwa nafasi ya Rais, wabunge na madiwani ili kuwezesha kuunda Serikali na kuchochea utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika nyanja mbalimbali za kiuchumi.

Mgombea Ubunge  Jimbo jipya la Uyole,Dk Tulia Ackson (kushoto) akimnadi mgombea udiwani Kata ya Isanga Dourmohamed Issa  leo Jumatano  Septemba  10,2025 katika uzinduzi  wa kampeni .Picha na Hawa Mathias



Awali akizindua mkutano wa kampeni na kumnadi mgombea huyo, Dk Tulia Ackson amehamasisha wananchi kuchagua wagombea ndani ya chama hicho ili kufikishiwa maendeleo.

“Ndugu zangu niwaombe mkapige kura za kishindo Oktoba 29, 2025 kwa nafasi ya diwani na mbunge wa Mbeya mjini, Patrick Mwalunenge atakayewasilisha kero na mahitaji yenu kwa Rais Samia Suluhu Hassan,” amesema.

Katika hatua nyingine, Dk Tulia ambaye ni mgombea ubunge jimbo jipya la Uyole, amesema katika nafasi ya mgombea urais wananchi wasitishwe na idadi kubwa ya watu waliojitokeza na kwamba kura za mgombea wa CCM, Samia Suluhu Hassan tayari zimejaa.

“Tukampigie kura za kujaa na kumwagika na kutiki Oktoba 29, 2025 ili kutekeleza haki ya msingi kwa kila Mtanzania kuchagua Rais, wabunge na madiwani wa CCM,” amesema.

Osia Juma Mkazi wa Kata ya Isanga, amesema kwa sasa hawana deni kikubwa wanaomba ifikapo 2030 Tanzania iwe Taifa litakalo komesha tatizo la ajira kwa vijana kupitia uwekezaji wa miradi ya kimkakati.