STEVEN Mukwala ni mmoja ya nyota 30 wa kikosi kipya cha Simba kwa msimu wa 2025-2026, licha ya awali kuelezwa alikuwa tayari yupo hatua ya mwisho kupigwa bei Uarabuni kabla ya dili hilo kufa kabla ya kufungwa kwa dirisha la usajili la Tanzania usiku wa Septemba 7.
Hata hivyo, vigogo wa klabu hiyo ya Uarabuni iliyokuwa ikimtaka kwa udi na uvumba straika huyo raia wa Uganda wamefichua kila kitu kilichokwamisha dili hilo walipozungumza na Mwanaspoti.
Iko hivi. Siku moja kabla ya kufungwa kwa dirisha la usajili, Al Ittihad ya Libya ilileta ofa kubwa ya kutaka kumnunua Mukwala, aliyebakiza mkataba wa mwaka mmoja na Wekundu hao.
Hadi dirisha la usajili linafungwa Jumapili iliyopita, dili hilo lilikwama licha ya mabosi wa klabu hizo mbili kuzungumza na kukaribia kufikia makubaliano ya kufanya biashara hiyo.
Hata hivyo, Al Ittihad imefunguka kupitia Rais wa klabu hiyo, Muhammad Ismail, aliyeliambia Mwanaspoti kuwa ni kweli walikuwa wanahitaji huduma, lakini muda ulikwamisha dili hilo.
Ismail alisema baada ya kufanya mazungumzo na Simba, Wekundu hao walikuwa tayari kumuuza mshambuliaji huyo, lakini walipata shida ya kupata mbadala wake kutokana na muda wa kufungwa kwa dirisha la usajili la Tanzania.
“Tulifanya mazungumzo kweli na Simba, tulikuwa na uhitaji wa kweli juu ya Mukwala, lakini kuna mambo yalikwamisha na kubwa ilikuwa ni suala la muda,” alisema Ismail na kuongeza;
“Unajua huku kwetu Libya muda wa kusajili ulikuwa unatosha, lakini shida ilikuwa huko Tanzania. Wenzetu waliona muda hautoshi kuweza kutafuta mbadala wake, wakaomba masaa machache kutafuta mtu, lakini wakashindwa kukamilisha kwa wakati.
Aidha, Ismail aliongeza wanaendelea kufanya maboresho makubwa ya kikosi chao kwani wana malengo ya kujenga timu imara huku wakiendelea kumwangalia Mukwala kwa muda wa mbele zaidi.
“Mukwala ni mshambuliaji mzuri, lakini kwa sasa imeshindikana.
“Tutaendelea kutafuta mchezaji mwingine, tunataka kuwa na timu imara sana msimu ujao, kutakuwa na ushindani mkubwa.”
Taarifa ambazo hazikuthibitishwa na mabosi wa Simba ni kwamba hesabu za vigogo wa klabu hiyo ilikuwa ni kumvuta Allan Okello pia kutokea Uganda, lakini mambo yalikwama na kumbakiza Mukwala kikosi na juzi katika tamasha la Simba Day alitoka benchi na kufunga bao la pili dhidi ya Gor Mahia ya Kenya waliocharaza mabao 2-0 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.