Mwanza. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Serikali imeweka mkakati wa kuhakikisha shughuli zote za ufuatiliaji na tathmini zinaimarishwa, huku akizitaka taasisi husika kukamilisha maandalizi ya Sera ya Taifa ya Ufuatiliaji na Tathmini ili kuwezesha kutungwa kwa sheria itakayosimamia utekelezaji wake.
Akifungua Kongamano la Kitaifa la Ufuatiliaji, Tathmini na Kujifunza (MEL) leo Alhamisi Septemba 11, 2025 jijini Mwanza, Majaliwa amesema lengo la hatua hiyo ni kuhakikisha ufuatiliaji na tathmini unakuwa wa kitaasisi.
Pia uwe unaoendeshwa kwa uwazi na uwajibikaji, na takwimu zinazokusanywa zinatumika moja kwa moja katika kufanya maamuzi na kupanga afua mbalimbali za maendeleo.

Baadhi ya washiriki wa Kongamano la Kitaifa la Ufuatiliaji, Tathmini na Kujifunza (MEL) linalofanyika jijini Mwanza kuanzia Septemba 10 hadi 13.
“Kwa idara zote zenye dhamana zikamilishe maandalizi ya Sera ya Taifa ya Ufuatiliaji na Tathmini kwa upande wa Serikali zote mbili ili hatimaye tuweze kutunga sheria itakayotuongoza. Tukifika hatua hiyo tutapata mafanikio makubwa,” amesema Majaliwa.
Amesema Serikali tayari imeanzisha vitengo vya ufuatiliaji na tathmini katika wizara zote, mikoa na taasisi kwa lengo la kuongeza uwajibikaji, uwazi na kuimarisha utekelezaji wa majukumu ya Serikali.
Amesema ili kufanikisha azma hiyo, ni muhimu vitengo hivyo kuimarishwa kwa kutengewa rasilimali fedha, kununuliwa vitendea kazi, kuajiri wataalamu pamoja na kuandaa mpango wa mafunzo ya kuwajengea uwezo watendaji.
“Kwa maofisa masuuli wote, hakikisheni kwamba idara na vitengo mnavyovitumikia vinaimarishwa na kutengewa rasilimali fedha. Pia wekeni mpango wa mafunzo ili wataalamu wawe na uelewa wa kutosha kwa ajili ya kupata matokeo bora,” amesema.
Aidha, Waziri Mkuu ameagiza Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) kufanya tathmini ya utekelezaji wa maagizo ya kuanzishwa kwa vitengo hivyo na kubaini kama mapungufu ya kimuundo yamefanyiwa kazi.
Amesema Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kushirikiana na Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) imeanza ujenzi wa mfumo wa Taifa wa kielektroniki wa ufuatiliaji na tathmini ambao utapokea taarifa kutoka mifumo yote ya Serikali, kuzichakata na kutoa taarifa sahihi kwa wakati.
“Ofisi ya Waziri Mkuu pamoja na mamlaka ya kufuatilia na kutathmini kwa mfumo wa kielektroniki lazima kuhakikisha mfumo huu unakuwa mfumo mkuu wa Serikali. Lengo ni kuweza kufuatilia idara vizuri na kuwezesha viongozi, watoa maamuzi na wananchi kupata taarifa na takwimu sahihi kwa muda wowote,” amesema Majaliwa.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza jambo alipotembelea banda la Tanea wakati wa Kongamano la Kitaifa la Ufuatiliaji, Tathmini na Kujifunza (MEL) linalofanyika jijini Mwanza kuanzia Septemba 10 hadi 13, 2025.
Amesema uwekezaji katika teknolojia za kisasa ni muhimu ili kuhakikisha takwimu zinakusanywa, kuhifadhiwa na kutumika kwa usahihi na kwa usalama, jambo litakalosaidia kufanya maamuzi bora kila inapohitajika.
“Watendaji wakuu wote tumieni taarifa zinazozalishwa kutokana na kazi ya ufuatiliaji na tathmini ili kuyaweka maamuzi yenu katika mikakati imara na pia tuweze kuhabarisha umma juu ya matokeo ya utekelezaji wa kazi za Serikali kwa uhakika zaidi,” amesema.
Amesema pia Serikali imeendelea kufanya tathmini ya miradi na matumizi ya fedha, ikiwemo daraja la JP Magufuli pamoja na Sh14.1 bilioni zilizotolewa Mkoa wa Mwanza kwa ajili ya kuwawezesha wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, ambapo Sh8.9 bilioni zilifikia walengwa kupitia vikundi mbalimbali vikiwemo vya wavuvi wadogo.
Kwa upande wa Zanzibar, Majaliwa amesema shughuli za ufuatiliaji na tathmini zinaendelea kuratibiwa na Tume ya Mipango ya Zanzibar ambayo tayari imetoa miongozo mbalimbali.
Awali, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), William Lukuvi amesema mpaka sasa vitengo vya ufuatiliaji na tathmini vimeanzishwa katika wizara zote, sekretarieti za mikoa 26, halmashauri za wilaya 184 pamoja na taasisi za umma.
Amesema uwepo wa mfumo wa kielektroniki utasaidia kupokea data, kuzichakata na kuzitafsiri kwa wakati na kuiwezesha Serikali kutumia takwimu sahihi, katika kupanga na kuboresha afua zinazotekelezwa.
Naye, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda amesema Serikali imewekeza zaidi ya Sh5.6 trilioni katika miradi ya maendeleo mkoani Mwanza ambapo baadhi imekamilika.
Amesema miradi mingine inayoendelea kutekelezwa ikikamilika, mkoa huo utaunganishwa na miundombinu ya ziwani, anga na ardhini.