NAHODHA wa Azam FC, Lusajo Mwaikenda amesema wanajua wana kazi kubwa ya kufanya msimu huu kuhakikisha wanafikia malengo, huku akimtaja kocha Florent Ibenge ni wa viwango na hawapaswi kumuangusha.
Mwaikenda aliyemaliza msimu uliopita na mabao saba na asisti tatu, aliliambia Mwanaspoti, wachezaji wapo tayari kwa ushindani na kila mmoja anajua kazi kubwa iliyopo mbele yao.
“Ni mapema sana kumzungumzia, kwani nimefanya mazoezi siku moja chini yake, ila nazungumza kutokana na CV aliyonayo Ibenge. Ni kocha mwenye uwezo mkubwa amefanya mambo makubwa kwenye timu alizopita mikakati ni kuhakikisha tunafanyia kazi maelekezo tunayopewa,” alisema Mwaikenda na kuongeza;
“Malengo ya benchi la ufundi ba wachezaji ni kuwa timu bora na shindani naamini kama tutaweza kuingia kwenye mifumo yake haraka tutakuwa na kazi moja tu uwanjani kuhakikisha tunafanyia kazi kwa usahihi maelekezo tunayopewa uwanja wa mazoezi.”
Akizungumzia mikakati binafsi alisema atafanya kazi kwa usahihi uwanjani suala la kufunga atafanya hivyo kila itakapotokea nafasi ya kufanya hivyo, huku akiweka wazi kuwa sio kazi yake lakini hawezi kuacha kuifanya akipata nafasi.
“Ni kweli msimu uliopita nimehusika katika mabao mengi nilifanya hivyo kwa sababu nilipata nafasi ya kufunga hivyo siwezi kuweka mikakati ta kuvunja rekodi yangu mwenyewe wakati sio kitu ambacho ni lazima nikifanye kama ilivyo kwa washambuliaji,” alisema Mwaikenda na kuongeza;
“Ukiniambia mpango wangu kwenye kuhakikisha namlinda kipa wangu asiruhusu mabao mengi nitakuwa na mengi ya kuzungumza lakini sio kufunga japo nikipata nafasi ntafanya ivyo.”
Alisema atashirikiana na wachezaji wenzake kuhakikisha wanaipambania timu hiyo kufikia mafanikio ligi ya ndani na michuano ya kimataifa.