Wasichana wataka kushiriki utekelezaji wa dira 2050

Dar es Salaam. Licha ya hatua mbalimbali kuendelea kuchukuliwa kuhakikisha kunakuwa na usawa kwa watoto wa jinsia zote, bado kuna ombwe la ujuzi wa ujasiriamali na stadi za maisha kwa wasichana , jambo linalozuia kundi hilo kufikia uhuru wa kiuchumi.

Hayo yameelezwa na wasichana wakati wa uzinduzi wa jukwaa la Ajenda ya Msichana 2025 linalolenga kuwakutanisha wadau wanaotetea haki za wasichana, kufanya tathmini ya maendeleo waliofanikiwa hadi sasa katika kulinda na kuendeleza haki za wasichana nchini Tanzania na kwingineko.

Jukwaa limebebwa na kauli mbiu isemayo; ‘Wasichana na Ujuzi kuelekea Dira 2050’ inayoakisi uhitaji wa ongezeko la  wa kuwaandaa wasichana kwa maisha ya baadaye kupitia kuwajengea uwezo katika uongozi, teknolojia, ubunifu wa sanaa na ujasiriamali.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Princess Wilfred ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha nne wa Shule ya Sekondari ya Kijitonyama jijini Dar es Salaam amesema  licha ya maendeleo yaliyopatikana, wasichana nchini bado wanakabiliwa na vikwazo mbalimbali katika kupata elimu na kumaliza shule, ukosefu wa fursa sawa katika kupata ujuzi wa kidijitali, nafasi za uongozi, na ajira.


Amesema kwa sababu hiyo ipo haja kwa jamii na Taifa kwa ujumla kufikiria kwa pamoja ili kutengeneza fursa zaidi kwa ajili ya wasichana.

Akiwasilisha tamko la wasichana katika uzinduzi wa jukwaa hilo, Princess amesema Tanzania kuna zaidi ya wasichana milioni  14.9  hivyo kundi hilo likiwezeshwa kwa rasilimali na fursa sahihi, wanaweza kuwa kundi kubwa zaidi la viongozi, wabunifu, wajasiriamali na wawezeshaji mabadiliko katika historia ya Taifa.

Hata hivyo, takribani watoto  milioni 3.2  wenye umri wa miaka saba hadi 17 hawapo shuleni wengi wao wakiwa ni wasichana hususani waliopo katika hatua za mpito kutoka elimu ya msingi kwenda sekondari kutokana na ndoa za utotoni na mimba za mapema.

“Mpango unaoratibiwa na Shirika la Watoto Duniani (Unicef) kupitia mradi wa Ujuzi kwa Wasichana (Skills4Girls), umebaini kuwa kuwawezesha wasichana kupitia ujuzi unaoweza kutumika katika nyanja mbalimbali ni jambo lisilokwepeka.”

 “Hapa tunazungumzia ujuzi wa kidijitali, ujasiriamali, na maandalizi ya ajira ni hatua muhimu ya kuvunja mifumo ya kutokuwa na usawa wa kijinsia   na kuwaandaa kwa ulimwengu wa ajira unaoendelea kubadilika.”

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo Mkurugenzi wa Shirika la Msichana Initiative, Consolata Chikoti amesema changamoto nyingi zinazowakumba wasichana kwa sasa zipo kwenye mifumo ya kijamii zinasababishwa na kutokuwepo usawa wa kijinsia.

“Kwa upande wake mwakilishi wa Shirika la Wotesawa, Jackline Martin amesema ndani ya miaka minane, jukwaa hilo limewaunganisha zaidi ya wasichana na wanawake vijana 15,000 na  kuwapa fursa endelevu ya  kukutana na kuimarisha nguvu ya pamoja na wadau ili  kuwawezesha kutetea haki zao katika ngazi ya jamii na Taifa.