Dar es salaam. Wadau wa afya wameiomba Serikali kuboresha huduma za utengamao nchini, wakisema bado hazijawafikia wananchi wengi hasa walioko vijijini.
Hoja hiyo ni kutokana na kile walichoeleza kuwa wananchi wanatembea umbali mrefu kupata huduma pamoja na uelewa mdogo wa jamii kuhusu umuhimu wa huduma hizo.
Wito huo umetolewa Septemba 10, 2025, katika mkutano wa wadau wa afya uliofanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC), jijini Dar es Salaam. Mgeni rasmi katika mkutano huo alikuwa Mratibu wa Tafiti kutoka Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), James Keingia.
Huduma ya utengamao ni msaada maalumu unaotolewa kwa watu wenye ulemavu wa aina mbalimbali ili kuwasaidia kuishi kwa uhuru, kushiriki kwenye jamii na kujitegemea zaidi.

Mkurugenzi wa Rehab Health Remla Shirima akizungumza kwenye mkutano uliowakutanisha wadau wa afya leo kwenye ukumbi wa JNICC
Akizungumza katika mkutano huo, Mkurugenzi wa taasisi ya Rehab Health, Remla Shirima alisema kuna haja ya Serikali kuongeza idadi ya wataalamu wa afya pamoja na vifaa saidizi vinavyotumika katika huduma za utengamao.
“Sisi kama taasisi tunalenga kuhamasisha huduma za utengamao, lakini wananchi wengi bado hawana uelewa kuhusu huduma hizi. Hali ni mbaya zaidi kwa maeneo ya vijijini ambako huduma hizi hazipatikani kabisa,” amesema Remla.
Aliongeza kuwa kongamano hilo linatarajiwa kuwa chachu kwa Serikali na wadau wengine wa afya katika kuhakikisha huduma hizo zinawafikia wananchi wote kwa usawa.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) nchini Tanzania, Dk Galbert Fedjo alisema huduma za utengamao bado hazijapewa kipaumbele katika mifumo ya bima ya afya, hali inayowafanya wananchi wengi kubeba mzigo mkubwa wa gharama za matibabu.
“Wananchi wengi wanaishi bila kinga ya kifedha. Hata wale walio na bima ya afya ya jamii, mara nyingi huduma za utengamao hazijajumuishwa katika vifurushi vyao,” amesema Dk Fedjo.
WHO imeitaka Serikali kupitia upya sera zake za afya ili kuhakikisha huduma kama tiba ya viungo, ushauri wa kisaikolojia na huduma kwa watu wenye ulemavu zinapatikana kwa wote bila mzigo wa kifedha.
Sharifa Mohamed, mzazi wa mtoto aliyepata huduma ya kunyooshwa viungo kutoka taasisi ya Rehab Health, alishukuru kwa msaada walioupata, akieleza kuwa mwanaye alipooza ghafla lakini baada ya huduma hizo, hali yake imeendelea kuimarika.
“Nawashukuru sana Rehab. Mtoto wangu alipata huduma bora, walimpatia mazoezi ya viungo na hata waliwashawishi klabu ya Yanga kucheza mechi ya hisani ili kusaidia kupatikana kwa fedha za matibabu na vifaa tiba,” amesema Sharifa.
Ametoa wito kwa Serikali kuisaidia taasisi hiyo kutokana na mchango mkubwa inayoutoa kwa jamii.

Mratibu wa Tafiti kutoka Tamisemi James Keingia akizungumza na wadau wa afya ambao hawapo pichani leo Septemba 9,2025 kwenye ukumbi wa JNICC wakijadili upatikanaji wa huduma za utengamao.
Akifungua kongamano hilo litakalofanyika kwa siku tatu, Keingia, alikiri kuwepo kwa upungufu wa wataalamu wa huduma za utengamao nchini, lakini akabainisha kuwa Serikali inalifanyia kazi suala hilo.
“Serikali imejipanga kuboresha huduma zote za afya, ikiwemo huduma za jamii, kinga, tiba na utengamao. Mwaka jana tulifanya kongamano kama hili, lakini mwaka huu idadi ya washiriki imeongezeka, jambo linaloonesha ushirikiano wa dhati kati ya Serikali na wadau wa afya,” alisema Keingia.
Aliongeza kuwa Serikali ina mpango wa kuongeza vituo vya utoaji huduma za utengamao pamoja na wataalamu wenye ujuzi wa juu ili kukidhi mahitaji ya wananchi.
Alihitimisha kwa kuishukuru taasisi ya Rehab Health kwa mchango wake katika kuisaidia Serikali kubaini maeneo yenye changamoto katika huduma hizo, akisema wizara itanufaika na taarifa hizo katika mipango ya kuboresha sekta ya afya.