Dodoma. Mahakama Kuu Masijala Kuu-Dodoma, imemrejesha kwenye kinyang’anyiro cha urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mgombea wa chama cha ACT-Wazalendo Luhaga Mpina.
Kesi hiyo ilikuwa inasikilizwa na jopo la majaji watatu, Abdi Kagomba, Evaristo Longopa na John Kahyoza.
Katika hukumu yao, majaji wamesema Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) ni huru na haikupaswa kusikiliza maelekezo ya mtu au taasisi yoyote, ikiwemo Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa.
Pia wamesema kwa kutopokea fomu za Mpina, Tume ilimnyima haki ya kikatiba na ile ya kusikilizwa.
Hivyo, mahakama hiyo imebatilisha barua ya Tume ya kumzuia Mpina kurejesha fomu kwa kuwa ilikuwa kinyume cha Katiba na haikuwa na nguvu ya kisheria.
Mahakama imeitaka INEC impe fursa mgombea huyo kuwasilisha fomu zake na mchakato uendelee ulipoishia Agosti 27, 2025.
Mpina alikuwa anapinga kuenguliwa katika mbio za urais kwenye Uchaguzi Mkuu wa 2025 ambapo INEC ilimzuia kufika kwenye ofisi za tume kukabidhi fomu zake na kuteuliwa.
INEC ilichukua uamuzi huo, kutokana na taarifa ya Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, kuwa mgombea huyo hakukidhi vigezo vya kuteuliwa ndani ya ACT -Wazalendo, baada ya kupingwa na kada wa chama hicho.