Dar es Salaam. Wakati uingizaji wa bidhaa za plastiki kutoka nje ya nchi ukiongezeka kwa asilimia 25.9, wadau wamependekeza matumizi ya vifungashio vya kioo au udongo katika bidhaa zinazotumia plastiki.
Hiyo ni kwa sababu wanunuzi watalazimika kurudisha chupa ya zamani ili kupata bidhaa mpya tofauti na sasa wanapotupa hovyo chupa za plastiki baada ya kumaliza kuzitumia.
Hayo yanabainishwa wakati ambao ripoti ya tathmini ya hali ya uchumi ya Agosti 2025 iliyotolewa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) inaonyesha kuwa fedha zinazotumika katika kuingiza bidhaa za plastiki nchini zilifikia Sh2.05 trilioni katika mwaka ulioishia Julai 2025, ikiwa ni ongezeko kutoka Sh1.62 trilioni kipindi kama hicho mwaka 2023.
Hali hii inatajwa kuchangiwa na ongezeko la watu linaloshuhudiwa hali inayofanya uzalishaji wa bidhaa zilizo katika vifungashio vya plastiki kuongezeka.
Akizungumza namna ya kutokomeza matumizi ya chupa za plastiki, Erika Tola amesema mbali na elimu ya utunzaji mazingira inayoweza kutolewa, pia alipendekeza kubadilishwa kwa vifungashio kutoka plastiki kwenda chupa za kioo.

“Kama ilivyo kwenye baadhi ya soda, ukinywa chupa unaiacha hapo au unahitaji chupa nyingine kwenda kuchukua bidhaa mpya hiyo pia inaweza kufanyika kwenye vitu vingine kama maji,” amesema Erika ambaye ni Mkurugenzi wa Masai Adventure Safari.
Akiwa pia mtekelezaji wa programu ya ‘plasticfree’ amesema utumiaji wa chupa za kioo unaweza kuongeza gharama kidogo lakini faida yake ni kubwa.
“Na inawezekana kutengeneza kwa ukubwa wowote ule, mwanzo ndiyo itakuwa gharama lakini baadaye itakaa dawa. Hii itasaidia kwa sababu chupa za plastiki zina athari kwetu sisi binadamu na hata viumbe hai baharini. Wanapokula chupa hizo za plastiki na sisi tukiwala tunakula moja kwa moja vipande vya plastiki,” amesema.
“Watu wajue kuwa wana dhamana ya kulinda mazingira, wapende mazingira, wanapotumia chupa akimaliza asiitupe tu hovyo bali aitunze hadi atakapopata sehemu nzuri ya kuhifadhi iliyoandaliwa,” amesema.
Tafiti ya 2017 yenye jina “Uzalishaji, matumizi, na hatima ya plastiki zote zilizowahi kutengenezwa” ya wasomi wa Marekani inasema;
uzalishaji na utupaji wa plastiki unachangia mabadiliko ya tabianchi kupitia uzalishaji wa gesi joto kwa sababu inatokana na nishati kisukuku (Fossil fuel).
“Mchakato wa kutengeneza plastiki unahitaji nishati nyingi, na utupaji mbaya wa plastiki husababisha kutoa hewa ya kaboni na methane. Uchafuzi wa plastiki unaharibu
baoanuai, ukiathiri michakato asilia inayosaidia kudhibiti hali ya hewa,” ulibainisha utafiti huo.
Hata hivyo, pia zipo tafiti zinazonyesha tani milioni nane hadi 10 zinaingia baharini kila mwaka na tafiti hizo zinaelekeza hadi 2050 plastiki itakuwa nyingi zaidi kuliko samaki kwenye maji.
Amebainisha hayo wakati aliposhiriki katika shughuli ya usafishaji wa fukwe uliofanyika leo katika Hoteli ya Serene jijini Dar es Salaam.
Mdau mwingine wa mazingira na Mkurugenzi mwenza wa Masai Adventure, Jakobo Kibori amesema upigaji marufuku matumizi ya chupa za plastiki utasaidia kuondoa tatizo hilo kwa asilimia 100 nchini.
“Kufukia haitatui tatizo hivyo tutaendelea kutoa elimu kote nchini ili kuonyesha umuhimu wa kutunza mazingira dhidi ya plastiki,” amesema
Ofisa Uhusiano wa Serene Beach Hotel, Anna Khaday amesema ni vyema elimu juu ya tahadhari za matumizi ya plastiki ikaanza kutolewa tangu shule ya msingi ili watoto wakue wakijua athari zake.