Samia aahidi neema kwa wakulima wa tumbaku

Uyui. Mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan amewahakikishia wakulima wa tumbaku mkoani Tabora kulipwa madai yao ya fedha na kwamba Serikali iko kwenye mazungumzo na kampuni mbili zinazodaiwa.

Samia amebainisha hayo leo Septemba 11, 2025, wakati wa mkutano wake wa kampeni katika Wilaya ya Uyui, yenye majimbo mawili ya uchaguzi ambayo ni Uyui na Igalula, ikiwa ni siku ya pili ya kampeni zake mkoani Tabora.

Akizungumzia madai ya wakulima hao, Samia amesema anatambua kwamba wakulima wa tumbaku wanadai fedha zao na wameanza kulifanyia kazi ili walipwe stahiki zao.


“Wakulima wa tumbaku wenye madai ya siku nyingi, bado tunafanya mazungumzo na kampuni zinazodaiwa, nawahakikishia kwamba wakulima watalipwa fedha zao,” amesema.

Samia amewapongeza wakulima hao kwa kuzalisha kwa wingi zao hilo, huku akieleza kuwa hilo linachochewa na ruzuku ya pembejeo za kilimo wanazozipata kutoka serikalini.

Amesisitiza kwamba wameongeza kampuni za kununua tumbaku, kwa hiyo kuna ushindani mkubwa katika ununuzi wa tumbaku na lile suala la kuchelewesha malipo yao, halitakuwepo tena.

Akizungumzia yaliyofanyika Uyui, Samia amesema wameajiri walimu 412 na watumishi wa afya 161 katika wilaya hiyo. Ameongeza kuwa wakichaguliwa tena, wataajiri watumishi wa afya 6,000 na watumishi wa elimu 7,000 nchi nzima.


Amesema wanaweka madarasa ya awali kupitia programu ya kuwaandaa watoto mapema, ndiyo maana shule mpya zinazojengwa zinakuwa na madarasa hayo ili waanze mapema.

Kwenye sekta ya kilimo, amesema wataendelea na ujenzi wa majosho na dawa kwa ajili ya mifugo ili kuwawezesha wafugaji kuwa na mifugo bora itakayoshindana kwenye soko la kimataifa.

Wakati huohuo, Samia amehimiza umoja na mshikamano ndani ya Wilaya ya Uyui, amewataka kuvunja makundi na kuwa chama kimoja ili waende kwenye uchaguzi wakiwa na nguvu kubwa.

“Niwaombe viongozi ndani ya wilaya kufanyia kazi jambo hilo, turudi kuwa kitu kimoja tukakitafutie chama chetu ushindi,” amesisitiza mgombea huyo.


Kwa upande wake, mgombea ubunge katika Jimbo la Igalula, Juma Mustapha amesema watapigana usiku na mchana kumtafutia mgombea urais kura nyumba kwa nyumba, ili kuhakikisha chama hicho kinapata ushindi wa kishindo.

Amesema yeye ni mgombea anayetokea ngazi ya balozi, jambo ambalo alinaonyesha demokrasia imekomaa ndani ya CCM kwa kutoa nafasi hata kwa viongozi wa chini ndani ya chama.

“Mheshimiwa mgombea, umetupa heshima kubwa sisi watu wa Igalula, umetuletea fedha kwa ajili ya miradi mbalimbali ya maendeleo, tunakushukuru na tunakuahidi kura nyingi za kishindo,” amesema.

Kwa upande wake, mgombea ubunge Jimbo la Uyui, Shaffin Sumar amesema wananchi wa Uyui wanampenda Samia kwa sababu wamenufaika na kazi anazofanya, ikiwemo kupeleka Sh121.8 bilioni ndani ya miaka minne.


Amesema Uyui imepata maji ya uhakika kupitia mradi wa maji kutoka Ziwa Victoria. Pia, amesema wamejengewa vyumba vya madarasa katika wilaya hiyo na zaidi ya yote, wamejenga na madarasa kwa ajili ya watoto wa chekechea.

“Tunakushukuru na tunakuahidi ushindi wa kishindo. Oktoba 29 tutamiminika kwenda kupiga kura kukipa ushindi chama chetu,” amesema mgombea huyo, huku akiomba kujengwa barabara kwa kiwango cha lami ili kuunganisha wilaya hiyo na Wilaya ya Kahama.