Washington. Rais Donald Trump ameagiza bendera ya taifa kupeperushwa nusu mlingoti, huku akitoa ujumbe mzito wa maombolezo kufuatia mauaji ya mwanaharakati na mshirika wake wa karibu, Charlie Kirk, yaliyotokea katika chuo kikuu huko Utah.
Trump kupitia video fupi ya dakika nne aliyoichapisha kwenye akaunti yake ya Truth Social amelaani kitendo hicho kwa kusema; “kuwafanya wapinzani wa kisiasa kuwa mashetani.
“Kwa Wamarekani wenzangu wapendwa, nimejawa na huzuni na hasira kufuatia mauaji ya kikatili ya Charlie Kirk katika chuo kikuu huko Utah. Charlie aliwahamasisha mamilioni ya watu, na usiku wa leo, wote waliomfahamu na kumpenda wameungana katika mshangao na hofu kubwa,” amesema Trump.
Trump amemuelezea Kirk kama Mmarekani mzalendo aliyeipenda nchi yake na ambaye alipenda kuzungumza na wananchi wa Marekani.
“Charlie alikuwa mzalendo aliyejitolea maisha yake kwa ajili ya hoja za wazi na taifa alilolipenda kwa moyo wote. Alipigania uhuru, demokrasia, haki, na watu wa Marekani.
“Yeye ni shahidi wa ukweli na uhuru, na hakuna aliyewahi kuheshimiwa kiasi hicho na vijana. Charlie pia alikuwa mtu wa imani ya kina sana, na tunapata faraja tukijua kwamba sasa yuko na Mungu mbinguni,” amesema Trump.

Kirk (31) ni baba wa watoto wawili, mwanzilishi wa shirika la vijana la Turning Point USA linaloandaa matukio kwenye vyuo vikuu kote nchini Marekani, alipigwa risasi shingoni katika tukio lililofanyika katika Chuo Kikuu cha Utah huko Orem, na alifariki takriban saa mbili na nusu baadaye.
Kirk ameacha mjane wake Erika Frantzve, ambaye walikuwa na binti mwenye umri wa miaka mitatu na mvulana wa miezi 16.
Licha ya Trump kuonyesha masikitiko ya mauaji hayo, wapinzani wa kiongozi huyo wametoa kauli kwenye mitandao ya kijamii wakifurahia mauaji ya Charlie Kirk huku baadhi yao wakimfananisha na Adolf Hitler, na wengine wakisema kuwa amepata alichostahili.
Mauaji ya mshirika huyo wa Trump ni mfano mwingine wa kuongezeka kwa ghasia za kisiasa nchini Marekani, zinazotokea kutoka pande zote mbili za mrengo wa kisiasa.
Charlie Kirk alikuwa mmoja wa wanaharakati w na mmoja wa watu wenye ushawishi kwenye vyombo vya habari nchini Marekani, na pia mshirika wa karibu wa Rais Donald Trump.
Alianzisha shirika lisilo la kiserikali la Turning Point USA, akiwa na umri wa miaka 18 tu.
Kirk aligeuka kuwa mhimili mkuu katika mtandao wa wafuasi wa Trump, mara nyingi akielezewa kama uso wa harakati ya “Make America Great Again” (Irejeshe Marekani kwenye ubora wake).
Trump mara kwa mara alimpongeza Kirk kwa kuhamasisha vijana wengi na wapiga kura kujiunga upande wake wakati wa kampeni za urais za mwaka 2024.
Kirk pia alikuwa mkosoaji wa vyombo vya habari na alijitumbukiza katika vita vya kitamaduni kuhusu masuala ya rangi, jinsia, na uhamiaji.
Mtindo wake wa uchokozi ulimletea wafuasi waaminifu lakini pia upinzani mkali.
Kirk alikuwa rafiki wa karibu wa mtoto wa kwanza wa Rais, Donald Trump Jr, na alikuwa mfuasi wa Makamu wa Rais, JD Vance, wakati Trump alikuwa bado anatafakari kama angemteua kuwa mgombea mwenza wake.
Kirk alikuwa na wafuasi milioni 5.5 kwenye jukwaa la X (zamani Twitter), na alikuwa mwenyeji wa kipindi cha The Charlie Kirk Show, ambacho ni podcast na programu ya redio iliyokuwa ikifikiwa na zaidi ya wasikilizaji 500,000 kila mwezi.
Alionekana mara kwa mara kwenye Fox News, ikiwemo kuwa mwenyeji mgeni kwenye kipindi cha Fox & Friends.
Kwa mujibu wa ripoti ya The New York Times, Kirk hakuwahi kutafuta nafasi ya kazi serikalini. Lengo lake lilikuwa kubadilisha Chama cha Republican na kwa upana zaidi, siasa za Marekani.
“Tunataka kuibadilisha tamaduni,” aliambia The New York Times Magazine hapo Februari.
Kirk pia alijijengea utajiri kupitia podcast yake maarufu, mialiko ya mara kwa mara ya kuhutubia hadhira, pamoja na vitabu, ikiwa ni pamoja na kitabu chake cha mwaka 2020 kilichouzwa sana kiitwacho, ‘The MAGA Doctrine’.