::::::::
Na Mwandishi Wetu Dar es Salaam
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa tahadhari kuwa msimu wa mvua za Vuli mwaka huu (Oktoba – Disemba 2025) unatarajiwa kuwa wa mvua za wastani hadi chini ya wastani katika maeneo mengi ya nchi.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dkt. Ladislaus Chang’a, ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa (IPCC), alitoa taarifa hiyo wakati wa mkutano na waandishi wa habari uliofanyika jijini Dar es Salaam, katika ukumbi wa Ubungo Plaza, Septemba 11, 2025.
“Vipindi virefu vya ukavu na mtawanyiko usioridhisha wa mvua vinatarajiwa kutawala hasa katika pwani ya kaskazini na nyanda za juu kaskazini mashariki,” alisema Dkt. Chang’a.
Alifafanua kuwa mvua zinatarajiwa kuanza wiki ya kwanza hadi ya pili ya Oktoba katika mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, Mara na kaskazini mwa Kigoma, na baadaye kusambaa mikoa ya Pwani ya Kaskazini na nyanda za juu Kaskazini Mashariki kuanzia wiki ya kwanza ya Novemba.
Mvua hizo zinatarajiwa kuisha mwezi Januari 2026, huku vipindi vya joto kali kuliko kawaida vikitarajiwa kujitokeza katika msimu huo.
Dkt. Chang’a alisisitiza umuhimu wa wananchi kufuatilia utabiri wa kila siku, kila wiki na kila mwezi pamoja na tahadhari zinazotolewa na TMA kwa kuwa mabadiliko ya hali ya hewa yanaweza kutokea kwa muda mfupi.
Aidha, alibainisha kuwa TMA inaendelea kutoa utabiri wa msimu kwa ngazi ya wilaya. “Wilaya 86 zilizopo kwenye ukanda wa mvua mbili kwa mwaka, zitapatiwa utabiri wa kina wa maeneo madogo,” alisema.
Mamlaka hiyo imewataka wananchi, wakulima na wadau wengine waendelee kutumia taarifa hizi katika kupanga shughuli zao kwa ufanisi ili kuepuka athari zitokanazo na mabadiliko ya hali ya hewa.