Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. CPA Amos Gabriel Makalla leo Alhamisi Septemba 11, 2025 amekutana na kuzungumza na Kaimu Balozi wa Marekani nchini Tanzania Balozi Andrew Lentz, akimuhakikishia usalama na mazingira rafiki ya uwekezaji na utalii Mkoani Arusha.
Katika mazungumzo yao CPA Makalla amemshukuru Balozi Lentz kwa ushirikiano na mchango wao mkubwa kwenye maendeleo ya Tanzania hususani katika sekta ya utalii, akieleza kuwa Mkoa wa Arusha na Tanzania kwa ujumla ni wanufaika wa idadi kubwa ya watalii kutoka nchini Marekani, akimsisitiza kuendelea kuwashawishi Raia wa Marekani kuja kutalii na kuwekeza nchini.
“Mkoa wa Arusha una utulivu mkubwa wa kisiasa, amani, usalama unaosababisha wananchi wetu kuendelea kujikita kwenye shughuli zao za maendeleo hivyo niwahakikishie raia yeyote wa Marekani na Mataifa mengine hawana sababu ya kuwa na wasiwasi wa kutembelea vivutio vya utalii vinavyopatikana Arusha ama kuja kuwekeza na kufanya biashara. Ofisi yangu ipo wazi na ipo tayari kutoa ushirikiano kwa yeyote anayekuja kuwekeza na kutalii Arusha.” Amesema Mhe. Makalla.

Naye Balozi Lentz amempongeza CPA Makalla kwa dhamira yake ya kusimamia maelekezo ya serikali katika kukuza utalii unaoongeza pato la Arusha na Taifa kwa ujumla kwa kuimarisha usalama Mkoani Arusha pamoja na jitihada zake za kurahisisha ufanyaji wa biashara kupitia mpaka wa Namanga kwa kuimarisha usalama na kuhimiza upatikanaji wa skana kwenye mpaka huo ili kupunguza muda wa wageni na mizigo kuhudumiwa wanapoingia nchini kupitia mpaka huo.
Viongozi hao pia wamejadiliana uwezekano wa kuanzisha Ukanda wa teknolojia ya kilimo cha Kibiolojia ( Bio- Agricultural technology Corridor) ili kuboresha uzalishaji kwenye sekta ya kilimo, kuimarisha usalama wa chakula na kujenga sekta ya kilimo inayostawi na endelevu kwa kuunda mfumo wa Ikolojia unaostawi kwa manufaa ya wakulima wa Arusha na soko la Marekani.
Related