Wanaodaiwa kughushi vibali vya kumiliki silaha, upelelezi wao upo hatua za mwisho kukamilika

Dar es Salaam. Upelelezi wa kesi ya kughushi vibali vya kumiliki silaha inayowakabili watu tisa wakiwemo maofisa sita wa Jeshi la Polisi, upo hatua za mwisho kukamilika.

Wakili wa Serikali, Clemence Kato, ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, leo Alhamisi Septemba 11, 2025 ilipofikishwa mahakamani hapo kwa ajili ya kutajwa.

Wakili Kato ametoa maelezo hayo, mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Geofrey Mhini, anayesikiliza kesi hiyo.

Washtakiwa katika kesi hiyo ni Mkaguzi wa Polisi mwenye namba PF. 19931 Fredrick Malekela(45)mkazi wa Kilwaroad; E. 4627 Sajenti Kalemwa Kaunga(54) mkazi wa Chanika; E.7855 Sajenti Edger Mlogo (54) mkazi wa Kibamba; F.1126 Sajenti Robert Titus (47) mkazi wa Kisarawe na F.5092 Sajenti John Kaposwe (46) mkazi wa Kurasini na WP 10050 Julieth Moshi (30) mkazi wa Kisarawe.

Wengine ambao sio maofisa wa jeshi hilo ni Damson Mnyilenga (59) mkulima na mkazi wa Chanika; Simon Aloyce (60) mfanyabiashara na mkazi wa Mwanza pamoja na Venrand Liberio (29) mfanyabiashara na mkazi wa Tataba.

Kato amedai kuwa kuna vitu vichache ambavyo wanamalizia na hivyo ameomba mahakama impe wiki mbili ili waweze kukamilisha upelelezi huo.

Kato baada ya kueleza hayo, hakimu Mhini alikubaliana na upande wa mashtaka na kuahirisha kesi hiyo hadi Septemba 25, 2025 itakapotajwa na washtakiwa wapo nje kwa dhamana.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, washtakiwa wanakabiliwa na kesi hiyo ya jinai ya mwaka 2025, yenye mashtaka 16 ya kughushi vibali vya kumiliki silaha.

Washtakiwa kwa pamoja wanadaiwa kutenda makosa hayo, kinyume na kifungu namba 333 na 335A na kifungu 337 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu , Sura ya 16 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2019.

Katika mashtaka yao, wanadaiwa kuwa vibali hivyo, vimetolea kati ya Desemba 5, 2024 hadi Aprili 4, 2025

Katika shtaka la kwanza, washtakiwa kwa pamoja wanadaiwa katika kipindi cha mwaka 2024, ndani ya Mkoa wa Dar es Salaam, kwa nia ya kudanganya walitengeneza nyaraka ya uongo ambayo ni kibali cha kumiliki silaha cha Desemba 5, 2024 chenye jina la Ahmed Ally, wakati wakijua kuwa sio kweli.

Shtaka la pili hadi la 13, washtakiwa wanadaiwa katika kipindi cha mwaka 2024 ndani ya Mkoa wa Dar es Salaam, walitengeneza vibali vya kumiliki silaha vyenye majina ya Ahmed Ahmed Sandrudin, Omary Abdallah, Robert Koka, Fathi Ally, Mohamed Salim, Suleman Mbewa, Mickdad Chakindo, Irfan Nafari, Gulam Abbas Najafi, Ismail Ismail na Salim Salim.

Shtaka la 14 hadi 16, washtakiwa hao wanadaiwa mwaka 2025 katika mkoa wa Dar es Salaam, kwa nia ya kulaghai walitengeneza nyaraka za uongo ambazo ni kibali cha kumiliki silaha chenye jina la Marwaan Habretsh, Maurice Kitiwe na Said Mohamed,wakati wakijua kufanya hivyo ni kinyume cha sheria.

Kwa mara ya kwanza, washtakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo Julai 28, 2025 na kusomewa mashtaka hayo ambayo waliyakana na wapo nje kwa dhamana.