JUZI Jumatano mida ya mchana wakati tukifuatilia Tamasha la Simba Day, Azam FC wakatushtua na taarifa ya kuwaacha nyota wanne wa kigeni ambao walikuwa nao msimu uliopita.
Wachezaji hao ni Jhonior Blanco, Ever Meza, Mamadou Samake na Franck Tiesse.
Katika hao wanne, wawili kijiwe kinaweza kutokuwa na deni nao sana ambao ni Blanco anayecheza nafasi ya ushambuliaji na Meza ambaye ni kiungo.
Na sababu hapa ni rahisi tu juu ya uamuzi wa kijiwe kutowapiga sana fimbo wawili hao nayo ni ya kimazingira kulinganisha na ilivyo wa Samake na Tiesse ambao wao tumegoma kusimama upande wao.
Meza na Blanco walikuwa katika mazingira ya tofauti kabisa na huko kwao walikotoka ambako ni bara jingine la tofauti na Afrika. Hivyo walilazimika kucheza huku wakiwa katika juhudi za kujaribu kuendana na maisha ya tofauti na kwao.
Bado kwenye uwiano wa kucheza, Meza na Blanco wamecheza sana kuliko Samake na Tiesse. Mfano katika msimu uliopita kwenye Ligi Kuu, Samake alianza kikosini mara moja tu huku Tiesse akiwa hajawahi kuanza.
Katika kikosi cha kwanza, Meza alianza mara nane wakati huo Blanco yeye akiwa ameanzishwa kikosini katika michezo minne.
Bahati mbaya nyingine ambayo iliwakatili Meza na Blanco ni majeraha ambayo yaliwanyima fursa ya kuonyesha viwango vyao kwa namna ya kutosha ingawa mara kadhaa walipocheza walionyesha viwango vya kuridhisha.
Nadhani kijiwe kinaamini Meza na Blanco hawaondoki na taswira mbaya na maisha ya Tanzania kipindi hiki wanaporejea kwao. Mazingira tu yaliwafanya washindwe kutupatia kikubwa tulichotegemea kutoka kwao.