AKILI ZA KIJIWENI: Mligo asahau ya nyuma ajikite na mpira Simba

ANTHONY Mligo ni miongoni mwa wachezaji waliofanya vizuri sana katika kilele cha Tamasha la Simba maarufu kama Simba Day, juzi Jumatano.

Ni beki wa kushoto ambaye Simba imesajili kutokea Namungo FC baada ya kuondokewa na wachezaji wawili wa nafasi hiyo, Mohamed Hussein na Valentine Nouma.

Mligo alipandisha vyema timu mbele na muda ambao alitakiwa kulinda alitimiza vizuri jukumu lake kwa utulivu wa hali ya juu akiwa na mpira na hata pale alipokuwa hana mpira.

Kwa presha ambayo imekuwapo baada ya Mohamed Hussein aliyeicheza nafasi hiyo kwa muda mrefu kuondoka, kijiwe kilihisi huenda mwanzo wake ndani ya Simba ungekuwa mgumu lakini imekuwa kinyume na siku ya kwanza tu ameyakosha macho ya mashabiki wa Simba.

Lakini kitu kingine ambacho kilidhaniwa kinaweza kumfanya Mligo ahitaji muda mrefu kupata utulivu ni sakata la usajili wake ndani ya Simba kwani ilikuwa imebaki kidogo tu ukwame na yeye kubakia Namungo.

Alipendekezwa na kocha Fadlu Davids lakini timu hiyo iliamua kumsajili Miraji Abdallah kutoka Coastal Union jambo ambalo benchi la ufundi halikukubaliana nalo na likalazimisha anayetakiwa kusajiliwa ni Mligo na sio vinginevyo.

Kucheza vizuri siku ya kilele cha Tamasha la Simba kuna maana kubwa sana kwa mchezaji mpya kama Mligo kwa vile idadi kubwa ya mashabiki wa timu hiyo wanakuwa wanalitazama na hapo wanaanza kukupokea vizuri jambo ambalo linakupunguzia presha mchezaji.

Usipocheza vizuri Simba Day utalazimika kutumia nguvu kubwa hapo baadaye kuwaaminisha mashabiki kwamba usajili wako ulistahili hivyo inaweza kuchangia kwa namna fulani kukupa ugumu.

Mpira sasa upo miguuni mwa Mligo mwenyewe. Ameshaanza vizuri na kinachohitajika ni muendelezo. Kufanya vizuri katika Simba Day hakupaswi kumfanya abweteke bali anatakiwa kujituma zaidi.