Waziri Mkuu wa Israeli, Benjamin Netanyahu, ametishia kuwaua tena viongozi wa Hamas walioko nchini Qatar iwapo Doha haitawafukuza maafisa hao, na kusababisha majibu makali kutoka kwa serikali ya Qatar.
Pamoja na ukosoaji huo wa kimataifa kuhusu shambulio lililotokea katika mji mkuu wa Qatar inaarifiwa kuwa Netanyahu hajatetereshwa kwa namna yoyote.
Netanyahu amesema siku ya Jumatano kwamba mataifa yanapaswa “kuipongeza” Israel kwa mashambulizi yake ya mabomu na mauaji katika maeneo mbalimbali ya Mashariki ya Kati.
Kauli hizo zilitolewa siku moja baada ya Israel kufanya shambulio lisilo la kawaida ndani ya Qatar, kwa kuwalenga viongozi waandamizi wa Hamas walioko Doha, wakati mazungumzo kuhusu pendekezo la kusitisha mapigano lililoungwa mkono na Marekani yakiendelea.
Katika taarifa yake, Wizara ya Mambo ya Nje ya Qatar imelaani vikali kauli za Waziri Mkuu huyo wa Israeli, ikizitaja kama “jaribio la aibu … la kuhalalisha shambulio la kinyonge dhidi ya ardhi ya Qatar, pamoja na vitisho vya wazi vya kuvunja tena mamlaka ya kitaifa ya nchi.”
“Netanyahu anafahamu vyema kuwa ofisi ya Hamas ilifunguliwa nchini Qatar katika muktadha wa juhudi za upatanishi zilizopigiwa chapuo na Marekani pamoja na Israel,” Taarifa hiyo imeeleza.
“Kauli kama hizi si jambo la kushangaza kutoka kwa mtu anayejiegemeza katika misimamo mikali ili kupata ushindi wa kisiasa, huku akiwa anatafutwa na vyombo vya sheria za kimataifa, akikabiliwa na vikwazo vinavyozidi kuongezeka kila uchao hali inayozidi kumtenga katika jukwaa la kimataifa,” Taarifa hiyo iliongeza.
Wakati hayo yakijiri, ikumbukwe kwamba ndani ya kipindi cha siku tatu pekee, Israel imefanya mashambulizi katika maeneo ya Gaza, Lebanon, Yemen, Syria, Tunisia na Qatar, huku ikiendeleza uvamizi wa kila siku katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu na siku ya Jumatano, Israeli iliwaua watu 35 katika shambulio nchini Yemen.