JKT Queens jioni ya leo Alhamisi imetinga nusu fainali ya michuano ya CECAFA Wanawake ya kuwania Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kuitandika Yei Joints ya Sudan mabao 2-0 kwenyw Uwanja wa Kasarani, Nairobi Kenya.
JKT inaungana na Rayon Sports ya Rwanda, wenyeji Police Bullets ya Kenya na Kampala Queens ya Uganda zilizofuzu mapema, huku watetezi wa taji hilo, CBE ya Ethiopia ikiondolewa makundi.
Mabao ya JKT yalifungwa na mshambuliaji kinda, Jamila Rajabu dakika ya 60 kabla ya dakika nane baadae beki Esther Maseke kuongeza la pili na kufanya mzani kusomeka 2-0.
Rasmi sasa JKT itakutana na Kenya Police iliyomaliza kinara wa Kundi A, huku Rayon ikiikaribisha Kampala mechi zitakazopigwa Uwanja wa Ulinzi Complex, Septemba 14.
Maafande hao wa kike walimiliki mpira, licha ya ushindani kukutana na ushindani kutoka kwa Yei Joint iliyocheza vizuri.
Hata hivyo, jitihada za Yei kuondoa hatari za mashambulizi zilizokuwa zinapelekwa na Jamila pamoja na Stumai Abdallah hazikuzaa matunda na baadae wakaambulia kichapo hicho.
Katika Kundi C, JKT imemaliza na pointi sita ikiwa haijaruhusu bao na ikitikisa nyavu za wapinzani mara saba, mechi ya kwanza iliitandika JKU Princess mabao 5-0 na leo tena kushinda 2-0.
Katika timu tisa shiriki kwa michuano ya msimu huu, JKT pekee ndio ambayo haijaruhusu bao lolote kwa dakika 180 za mechi mbili ilizocheza, huku Jamila akifunga mabao manne ikiwa ni wastani wa kufunga mawili kwa kila mechi.