Manara: Maji, umeme, heshima ya wafanyabiashara Kariakoo niachieni mimi

Dar es Salaam. Mgombea udiwani Kata ya Kariakoo kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Haji Manara ameahidi kutatua kero ya maji taka, kukatika kwa umeme inayolikabili eneo maarufu la biashara la Kariakoo, Wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam.

Sambamba na hilo ameahidi kuilinda heshima ya wafanyabiashara wa Kariakoo ambapo amesema wanalipa kodi kubwa hapa nchini, hivyo mazingira bora ya kufanyia biashara yanastahili kuboreshwa.

Manara ameyasema hayo leo Alhamisi Septemba 11, 2025 katika uzinduzi wa kampeni za udiwani Kata ya Kariakoo zilizohudhuriwa na wagombea wa chama hicho Wilaya ya Ilala akiwemo mgombea ubunge Jimbo la Ilala, Mussa Zungu.

“Kariakoo ni kongwe, kitovu cha biashara na yenye historia. Tunasema inalipa kodi sana hivyo shida kama umeme, maji taka na safi lazima tuitatue hapa kuna wafanyabiashara na wakaazi ni lazima tulinde masilahi ya wote,” amesema.

Amesema haiwezekani umeme kukatika mara kwa mara, pia maji kuwa kero kwa eneo linalolipwa kodi kwa wingi. Kuhusu wafanyabiashara ndogondogo, amesema atasimama na Serikali katika kuwawekea mazingira bora.

Akizungumza kwenye mkutano huo, Waziri wa Maji, Jumaa Aweso ambaye anagombea ubunge Jimbo la Pangani amesema maji hayatakuwa kikwazo kwa wananchi wa Kariakoo akisema ni haki kwa Watanzania.

“Changamoto ya majitaka nakiri kama waziri lakini tumepanga kutatua kero hiyo,” ameeleza Aweso.

Awali mgeni rasmi katika mkutano huo ambaye ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Abbas Mtemvu amesema CCM ina kila sababu ya kupata kura kutokana na maendeleo iliyoyafanya.

“Tulipoona jina la Haji, tukasema huyu sahihi kwa kuwa anaijua Kariakoo. Kwa uzoefu wake atakuwa kiongozi mzuri hapa. Sisi pia tutamuongoza,” amesema.

Zungu amesema Manara ana sifa kwa kuwa ana nyota ya kipekee kwani pia alishawahi kuwa mwenezi wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam.

“Hata kabla hajaanza kazi ameshatambua shida za Kariakoo kama shida ya maji taka, maji safi, shida ya umeme na ameshaanza kushirikiana na viongozi kuona watatatuaje,” amesema.

Ameelezea suala la mgambo kufanya uonevu pamoja na sheria zilizopo lakini wanawaonea wafanyabiashara kwa kuwanyang’anya mali zao.

Aidha, amesema mgombea urais kupitia chama hicho Samia Suluhu Hassan anastahili kupewa kura kwa maendeleo aliyoyafanya ndani ya muda mfupi ikiwemo kutekeleza ilani kikamilifu.

“CCM tumejipanga kushinda uchaguzi Rais Samia akipata hata kura 39 milioni zitatosha,” amesema Zungu.