Na: Calvin Gwabara
– Dodoma.
Jamii
na Wanahabari wametakiwa kutambua kuwa Katiba inabeba masharti ya jumla ya
masuala mbalimbali ya nchi lakini masharti hayo yanafafanuliwa zaidi kupitia
Sheria, kanuni na Miongozo, hivyo jamii isidai yaliyoandikwa kwenye katiba moja
kwa moja bila kutafuta ufafanuzi zaidi na kuhisi wananyimwa haki zao.
Mwandishi Mkuu wa Sheria nchini Bw. Onorius Njole wakati akizungumza na Wahariri wa vyombo vya habari jijini Dodoma. |
Hayo
yamebainishwa na Mwandishi Mkuu wa Sheria nchini Bw. Onorius Njole wakati
akiwasilisha mada yake kuhusu uanzishwaji wa Ofisi, majukumu na mafanikio ya
Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria (OCPD) kwenye kikao kazi kati ya Wahariri wa
vyombo mbalimbali vya habari nchini kilichaondaliwa na Ofisi ya Mwansheria Mkuu
wa Serikali jijini Dodoma.
“Kumekuwa
na malalamiko ya baadhi ya watu kuwa wananyimwa haki fulani fulani za kikatiba
bila kujua kuwa Katiba inabeba sharti la jumla la jambo fulani lakini jambo hilo
linafafanuliwa zaidi kwenye Sheria, Kanuni na Miongozo mbalimbali. Mfano mzuri
Katiba inasema mtu ana haki ya kuishi lakini ukiingia kwenye Sheria unakutana
na adhabu ya kunyongwa kwenye ukifanya mambo fulani ya jinai yaliyoaanishwa
hivyo huwezi kusema unasimamia katiba na ukatenda jinai” alifafanua Bwana
Njole.
Aliongeza
“Mfano mwingine mzuri katiba inasema kila mtanzania ana haki ya kuchagua na
kuchaguliwa lakini ukisoma katiba katika eneo hilo unakutana na Sheria ya
uchaguzi pengine na miongozo ya pale kwa Mkurugenzi wa uchaguzi inasema kupiga
kura mwisho saa 12 jioni hivyo ukienda saa mbili usiku utakosa haki yako ya
kuchagua na hutakiwi kusimama na haki ya katiba kwa kusema katiba inanipa haki
ya kuchagua ninayemtaka”.
Bw.
Onorius Njole amewataka Wahariri hao wa vyombo vya habari kuhakikisha
wanasaidia kutoa habari, Makala na chambuzi ambazo zitasaidia jamii kuelewa
mambo hayo ya kikatiba na Sheria ili kuodoa malalamiko na sintofahamu
zinazojitokeza kwenye jamii kwa kutojua kile wanachokidai na katika mazingira
gani.
Akieleza
mafaniko yaliyopatikana katika kipindi cha miaka mitano kwenye Ofisi ya
Mwansheria mkuu wa Serikali amesema sekta ya Sheria imekuwa kila mwaka kutokana
na mabadiliko ya Muundo na mageuzi makubwa ya uanzishwaji wa Ofisi ya Mwandishi
Mkuu wa Sheria ambayo imewezesha kukamilika kwa zoezi la Urekebu wa Sheria na
kutoa toleo la Urekebu la mwaka 2023, Kufanya ufasili wa Sheria kuu 433 kati ya
Sheria 446 kuwa kwenye lugha ya Kiswahili na kuwezesha jamii kupata Sheria kwa
lugha mama.
Aidha,
Ofisi Ya Mwandishi Mkuu wa Sheria imefanya upekuzi wa mikataba ya kitaifa na
kimataifa 3446 inayohusu ununuzi,ujenzi, ukarabati, kufanya upekuzi wa Hati za
mashirikiano (MoU) 729, kutunga Sheria 68 huku Sheria ndogo 5,708
zimetengenezwa ili kukidhi mahitaji ya sasa ya maendeleo ya nchi na jamii na
hivyo kusaidia kuchochea maendeleo kwenye sekta mbalimbali .
Mwandishi
huyo Mkuu wa Sheria nchini amesema Ofisi yake itaendelea kutoa ushirikiano wa
kina kwa Wahariri na waandishi wa habari kwenye kutoa ufafanuzi wa masuala
mbalimbali ya kisheria yaliyo chini ya ofisi yake ili kuwa na uelewa wa pamoja
wa mchakato mzima wa uandishi wa Sheria nchini kwa maslahi mapana ya jamii na
taifa.
Awali
akifungua kikao kazi hicho Naibu Mwansheria Mkuu wa Serikali Mhe.
Samweli Maneno amewataka Wahariri wa vyombo vya habari na wanahabari
wanapoandika habari zinazohusu masuala ya kisheria nchini kuhakikisha wanapata
ufafanuzi kwa mamlaka sahihi ili kuondoa upotoshwaji ambao unaweza kuleta
madhara makubwa kwa nchi na jamii.
“Tunatambua kuwa nyinyi wahariri ndio wenye
mamlaka ya mwisho ya kuamua kuhusu kutangazwa kwa kila habari ianyoonekana
kwenye vyombo vyenu hivyo mna jukumu kubwa la kuhakikisha habari hizo zimetoka
kwenye mamlaka sahihi hasa habari zinazohusu masuala ya kisheria, hivyo kwa
kupitia kikao hiki mtaweza kuelewa watu sahihi na mamlaka ambazo zinaweza
kuwasaidia kupata taarifa sahihi ili kujenga uaminifu kati yenu na walaji wa
taarifa” Alisema Mhe. Maneno.
Mhe. Samweli Maneno amesema malengo ya Ofisi hiyo ni kuhakikisha
kuwa wanakuwa vinara katika utekelezaji wa Dira ya maendeleo ya Taifa ya mwaka
2020 na ili lengo hilo liweze kufikiwa na jamii kufikia lengo hilo lazima nchi
iwe na amani na utulivu ambao unatokana na uzingatiwaji wa utawala wa Sheria
zinazowaongoza kwa kuzingatia haki na wajibu.
Amesema amani na umoja iliyopo
nchini vikitoweka hakuna shughui yoyote ya kimaendeleo itakayoweza kufanyika
katika jamii na hivyo kushindwa kutekeelza dira hiyo ambayo lengo lake ni
kuleta ustawi wa watu na kuinua maisha ya uchumi kupitia shughuli mbalimbali.