Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, ameieleza Mahakama Kuu kuwa hatua ya Mahakama ya Kisutu kukataa kuwaorodhesha mashahidi wake imemnyima haki na sasa hana mahali anakoweza kuipata, isipokuwa kwa huruma ya mahakama.
Ametoa madai hayo leo Alhamisi, Septemba 11, 2025, wakati akihimitisha majibu yake ya hoja za Jamhuri kuhusiana na pingamizi lake dhidi ya kesi yake ya uhaini ambapo pamoja na mambo mengine ameomba mahakama imwachie huru.
Amedai kuwa chini ya kifungu 264 cha Shereia ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai (CPA) marejeo ya mwaka 2023, mshtakiwa ana haki ya kutamka majina na anuani ya mashahidi wake wakati wa mwenendo kabidhi, lakini Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu iliyoshughulikia mwenendo wa awali, ilikataa kuwaorodhesha mashahidi hao.
Mashahidi hao ambao aliwataja na hawakuorodheshwa na mahakama ikimwelekeza kuwa hao atawataja kesi yake itakapoitwa Mahakama Kuu ni Samia Suluhu Hassan, Dk Phillip Mpango na Kassim Majaliwa. Samia ni Rais, Dk Mpango ni Makamu wa Rais na Majaliwa ni Waziri Mkuu.
Lissu amesisitiza kuwa kwa kuwa alinyimwa haki hiyo na hapa alipo hana haki ya kuita mashahidi wake, isipokuwa kwa huruma ya mahakama tu.
Hivyo amedai kwa hatua hiyo Mahakama ya Kisutu iliathiri haki ya usikilizwaji wa haki katika kesi dhidi yake.
Akihitimisha hoja zake Lissu amedai kutokana na hilo na kasoro nyingine alizozibainisha za mwenendo kabidhi wa kesi yake, ikiwemo Mahakama ya Kisutu kutokuwa na mamlaka hayo, Mahakama Kuu haina cha kufanya zaidi ya kumuachia huru.
Jamhuri katika hoja zake mbadala juzi iliiomba Mahakama Kuu kama itakubaliana na hoja za Lissu kuwa kulikuwa na kasoro katika mwenendo kabidhi, basi nafuu yake ni kuamuru kesi hiyo irejeshwe Kisutu isikilizwe upya katika hatua hiyo.
Hata hivyo, Lissu amepinga hoja hiyo akidai kuwa kwa kuwa Mahakama ya Kisutu haina mamlaka ya kuendesha kesi hiyo katika hatua ya mwenendo kabidhi (kama alivyodai), hivyo Mahakama Kuu haina mamlaka kuamuru kesi hiyo irudi Kisutu.
”Ninawaomba waheshimiwa majaji kufanya uamuzi wa haki na kwa kuzingatia Sheria za Tanzania. Msihofu”, amesema Lissu na kuwa pia hawapaswi kuamuru arudishwe kushtakiwa Mbinga alikokamatiwa, kwa kuwa mpaka sasa hana kesi Mbinga.
Mahakama baada ya kusikiliza hoja na hitimisho hilo, imeahirisha shauri hilo hadi Jumatatu, Septemba 15, 2025 itakapotoa uamuzi wa pinagmizi la Lissu.
Katika kesi hiyo Lissu anakabiliwa na shtaka moja la uhaini kinyume na kifungu cha 39(2) (d) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, linalotokana na maneno aliyoyatamka kuhusiana na kuzuia Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Anadaiwa kuwa Aprili 3, 2025, jijini Dar es Salaam, akiwa raia wa Tanzania, kwa nia ya uchochezi alishawishi umma kuzuia kufanyia kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, huku akitamka na kuandika maneno ya kumshinikiza kiongozi Mkuu wa Serikali ya Tanzania.
Alipandishwa kizimbani kwa mara ya kwanza na kusomewa shtaka hilo Aprili 10, 2025, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Dar es Salaam, ilikofunguliwa kwa ajili ya maandalizi ya awali kabla ya kuhamishiwa Mahakama Kuu, iliyo na mamlaka ya kuisikiliza.
Kesi hiyo ilipangwa kwa ajili ya usikilizwaji wa awali kwa maana ya mshtakiwa kusomewa na kujibu shtaka na kisha kusomewa maelezo ya awali ya kesi, Septemba 8, 2025, Lissu aliibua pingamizi hilo.
Katika pingamizi hilo, Lissu anapinga kesi hiyo kusikilizwa badala yake anaiomba mahakama iitupilie mbali, akidai mwenendo ya awali una kasoro za kisheria na pili, kwamba Mahakama Kuu haina mamlaka ya kuisikiliza kutokana na kasoro hizo, ikiwemo ya kushtakiwa mahali ambapo hakukamatiwa.