Mgombea urais UPDP atamba kuunda Serikali wezeshi kumudu gharama za maisha

Musoma. Mgombea urais wa UPDP, Twalib Kadege, amesema wakishinda Uchaguzi Mkuu wa 2025, wataunda serikali wezeshi ili wananchi waishi maisha bora na kumudu gharama za maisha.

Akihutubia mkutano wa kampeni leo Septemba 11, 2025, Kadege amesema ilani yao inagusa maisha ya kila Mtanzania na kuwataka wapiga kura kujitokeza kwa wingi kuchagua UPDP kwa maendeleo yao.

“Tutakuwa na utaratibu wa kuondoa matatizo hasa ya kiuchumi kwa Watanzania wote wakiwepo vijana, tutatengeneza serikali wezeshi kwenye masuala ya ajira, viwanda hivi vitakuwa vya kuzalisha vitu mbalimbali ikiwepo mazao ya shambani katika kila eneo,” amesema.

Kadege amesema viwanda hivyo havitaendeshwa na serikali isipokuwa kutakuwa na utaratibu maalumu wa kuvikabidhi kwa makundi mbalimbali ili kuviendesha kwa tija.

“Wale vijana wetu wanaomaliza  darasa la saba  na kidato cha nne hawatazubaa tena kwani viwanda vitakuwepo na tutawapa mitaji mikubwa kuviendesha wao na sio serikali,” amesema.

Amesema ili viwanda hivyo viweze kuendeshwa vizuri mbali na mitaji, pia vijana hao wataletewa wataalamu wa kuwafundisha namna bora ya kufanya uzalishaji ili kukuza vipato vyao huku serikali ikinufaika na kodi kutoka kwenye viwanda hivyo.

Kadege amesema serikali ya UPDP itahakikisha upatikanaji wa umeme wa uhakika kwa ajili ya kuviwezesha viwanda kufanya kazi kwa tija, ikiwemo kujenga vinu vya nyuklia kuongeza uzalishaji wa umeme bila vikwazo.

Kuhusu huduma kwa wananchi, ameahidi huduma bora na kuonya watumishi wa umma wabadhirifu, akisisitiza kuwa yeyote atakayefuja fedha za umma atafilisiwa, kufikishwa mahakamani na kuchukuliwa hatua kali bila kujali nafasi yake.

“Kuiba fedha za umma ni bora umeze misumari utapona, ukiiba tutakushughulikia hata kama ni mimi rais lazima nishughulikiwe, yaani mimi nichukue pesa za wananchi kisa mimi ni Amiri Jeshi Mkuu, hii hapana nitamuomba Mwenyezi Mungu ili roho hiyo nisiwe nayo,” amesema.

Kuhusu wazee, Kadege amesema chama hicho kimeandaa sera nzuri ili kuhakikisha wazee wanakuwa na maisha mazuri baada ya kuitumikia nchi kwa nafasi mbalimbali.

Amesema wazee wote nchini watalipwa Sh500,000 kama fedha za kujikimu kila mwezi na  uamuzi huo unatokana na ukweli kuwa wanastahili kutunzwa kwani wameitumikia nchi vema.

Naibu Katibu Mkuu wa UPDP Taifa,  Rajab Hoza amewataka Watanzania wenye sifa  kujitokeza kupiga kura Oktoba 29, 2025 kwani hiyo ni haki yao kikatiba huku akiwataka kulinda amani na utulivu.

“Msije mkaanza kulalamika vijiweni jitokezeni mkapige kura kwani hii ni haki yetu sote, mnatakiwa kutumia ipasavyo,” amesema Hoza.

Kuhusu uhuru wa vyombo vya habari, Kadege amesema endapo UPDP itaongoza nchi, vyombo hivyo vitakuwa huru na vitapewa nafasi ya kufanya kazi bila kuingiliwa.

Aidha, amesema chama chake kitaelekeza wamiliki wa vyombo vya habari kuwaajiri waandishi hadi ngazi ya vijiji ili kuripoti changamoto za wananchi kwa ufanisi na kuiwezesha serikali kuzitatua kwa wakati.

“Lakini vyombo hivyo vizingatie sheria za nchi, hatutakubali vyombo vya habari  vikavunja sheria ya nchi na kuleta mtafaruku nchini,” amesema.

Mwenyekiti wa UPDP Mkoa wa Mara, Marwa Girimba amewataka Watanzania kukipigia kura chama hicho ili kiweze kuongoza nchi akisema kuwa chama hicho pekee ndicho kinamuwezesha Mtanzania kujua leo na kesho yake.

“Hapa kwetu Mara tumekuwa na matatizo sugu na tumeyapigia kelele sana, viwanda vimekuwa magofu na matatizo mengine mengi, nikuombe mheshimiwa ukishakabidhiwa kiti cha urais uangalie namna ya kutumia rasilimali zilizopo kutatua ukata kwa wananchi,” amesema.