…………….
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara anayeshughulikia Uhifadhi, Kamishna wa Polisi (CP) Benedict Wakulyamba ametoa kauli hiyo jijini Arusha alipokuwa akifunga mafunzo ya kikazi kwa majaji, wadau wa haki jinai na Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) yaliyolenga kuimarisha uhifadhi endelevu wa maliasili.
“Miongoni mwa hatua tunazochukua ni kutoa elimu ya uhifadhi, kuimarisha uwajibikaji wa watendaji, na kufanya upelelezi wa kesi za ujangili kwa weledi mkubwa na kwa kuzingatia sheria zilizopo,” amesema.
Aidha, amebainisha kuwa Wizara itaendeleza mafunzo ya aina hiyo katika kanda mbalimbali za uhifadhi, hususan maeneo yenye mahakama, sambamba na kushirikisha taasisi zote za mnyororo wa haki jinai ili kuongeza uelewa wa sheria za uhifadhi nchini.
Hata hivyo, CP Wakulyamba amesema Wizara haitasita kuchukua hatua hatua kali za kinidhamu na kisheria kwa watumishi wake na taasisi za uhifadhi zitakazobainika kushirikiana na wahalifu kuhujumu maliasili.
Ameishukuru Mahakama ya Tanzania chini ya uongozi wa Jaji Mkuu kwa kuruhusu mafunzo hayo kufanyika pamoja na washiriki wote waliotoa mchango wao.
Naye, Naibu Kamishna wa Uhifadhi TANAPA, Steria Raphael Ndaga, amesema mafunzo hayo yamekuwa na mafanikio makubwa kwa kuwa yamewaleta pamoja wadau muhimu wa serikali wenye jukumu la kulinda na kusimamia maliasili.