Miaka 90 Yanga si mchezo

TANGU mwaka 2019, ambapo Mwenyekiti wa Yanga wakati huo Dkt. Mshindo Msolla alitekeleza Wiki ya Mwananchi kwa mara ya kwanza na kuwa na kilele chake kwenye uwanja wa Benjamini Mkapa kwa burudani na mechi ya kirafiki, tayari imepita miaka sita na miezi minane.

Kumbukumbu zinaonyesha kuwa tamasha la kwanza la Yanga lilianza kwa sare ya bao 1-1 dhidi ya Kariobangi Sharks ya Kenya.

Katika mechi hiyo, Kariobangi ilitangulia kupata bao kupitia Patrick Otieno dakika ya 49, kabla ya Patrick Sibomana kusawazisha dakika sita baadaye kwa mkwaju wa penalti.

Kwa msimu huu, Yanga imewaalika Bandari FC kutoka Kenya kushiriki katika kilele cha Wiki ya Mwananchi, kitakachofanyika Septemba 12, ilikuwaje kuanzishwa kwa tamasha hilo na yapi mafanikio ya timu hiyo ya Wananchi ndani ya miaka 90.

KUANZISHWA WIKI YA MWANANCHI

Mwanzoni malengo makuu ya tamasha la Yanga yalikuwa ni kukusanya mapato kwa ajili ya usajili wa wachezaji na kugharamia uendeshaji wa klabu. Ilikuwa ni njia rahisi ya kuunganisha mashabiki, kupata fedha, na kuwezesha maandalizi ya msimu mpya wa ligi.

Kadri miaka ilivyozidi kusonga, uongozi wa klabu ulianza kubadilisha mtazamo wa kiutendaji. Yanga ilipoimarika kiuchumi na kujijengea misingi ya uongozi thabiti, umuhimu wa tamasha hili ukavuka mipaka ya ukusanyaji mapato pekee.

Tamasha likaanza kupewa sura ya tofauti si tu kwa klabu bali pia kwa mashabiki na taifa kwa jumla.

Sasa likawa ni sehemu ya burudani ambapo mashabiki hujitokeza kwa wingi kushuhudia uzinduzi rasmi wa kikosi kipya.

Mashabiki walipata fursa ya huona kwa mara ya kwanza nyota wapya waliowasajiliwa, jambo linalowapa imani na hamasa ya kuingia msimu mpya kwa nguvu.

Kila mwaka, mashabiki wanapata kumbukumbu mpya kupitia muziki, burudani, na mchezo wa kirafiki unaopangwa maalumu kwa ajili ya kusherehesha siku hiyo.

Kwa upande wa kijamii na kibiashara, tamasha hili limekuwa kivutio cha wadau mbalimbali. Wafanyabiashara, wadhamini na hata wageni wa heshima hujitokeza, jambo linaloongeza thamani ya klabu mbele ya jamii na wadau wa michezo.

Pamoja na kuwa moja ya klabu kongwe nchini, Yanga ambayo ilianza kulitumia jina hilo mwanzoni mwa miaka ya 1970 baada ya agizo la aliyekuwa Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Abeid Amaan Karume aliyezitaka timu zote kuwa na majina ya kiafrika, pia Yanga ina rekodi tamu na za kibabe.

Yanga ndio klabu ya kwanza nchini kuiwakilisha nchi kwenye michuano ya kimataifa na kuandika historia ya kufika robo fainali ikifanya hivyo mara mbili mfululizo, yaani 1969 na 1970.

Kitu cha ajabu ni kwamba Yanga ilifika hatua hiyo na kucheza na Asante Kotoko ya Ghana na moja ya mechi yao iliamuliwa kwa kurushwa kwa sarafu baada ya kushindwa kupata mbabe katika mechi zote mbili za awali.

Achana na rekodi hiyo, Yanga pia ndio klabu ya kwanza ya Tanzania kucheza hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika ikifanya hivyo mwaka 1998, msimu mmoja tu tangu Klabu Bingwa Afrika ibadilishwe mfumo wake mwaka 1997.

Kubwa zaidi ni kwamba 2023, Yanga iliweka historia ya kusisimua baada ya kufika Fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika na kulikosa taji kwa nchi ya kidole baada ya matokeo ya mwisho kuwa sare ya 2-2, lakini USM Alger ya Algeria ilitwaa kwa faida ya bao la ugenini.

Yanga ilipoteza nyumbani mabao 2-1 na kwenda kushinda ugenini 1-0.

Mbali na rekodi hiyo, Yanga pia ilikuwa klabu ya kwanza Tanzania Bara kucheza robo fainali ya Kombe la Washindi Afrika mwaka 1995, mwaka mmoja tu baada ya Malindi kufika hatua 1994.

Ni kweli Simba ndio mabingwa wa kihistoria wa michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame), ikitwaa taji mara sita, lakini Wekundu hao kwa Yanga wamekaa.

Ndio, licha ya Simba kushikilia rekodi ya kubeba taji hilo mara nyingi, lakini hawajawahi kutwaa nje ya Tanzania, tofauti na Yanga ambao inashikilia rekodi mpaka sasa kwa kufanya hivyo.

Vijana wa Jangwani waliandikia historia kwa kutwaa taji la michuano hiyo mwaka 1993 nchini Uganda, tena ikienda Kampala kinyonge kulinganisha na watani wao walioenda kwa ndege wakiwa ndio watetezi na kurudi mikono mitupu.

Kama kuna watu waliodhani Yanga ilibahatisha mwaka huo, basi walikosea kwani ilirejea tena rekodi hiyo mwaka 1999 walipoenda kutwaa ubingwa nchi Uganda kwa mara nyingine.

Rekodi zinaonyesha hadi sasa Yanga imetwaa taji hilo mara tano ikiwa nyuma ya taji moja dhidi ya watani wao, huku Azam FC ikifuatia kwa kulibeba mara mbili, 2015 na 2018.

Licha ya kubeba mataji matano ya Afrika Mashariki na Kati, lakini Yanga bado ni Baba Lao katika Ligi Kuu ya Bara kwani tangu ilipoasisiwa mwaka 1965 imetwaa ubingwa mara 31.

Wao ndio vinara wakifuatiwa na watani wao waliobeba mara 22 hadi sasa, pia ndio wababe wa kwanza katika mechi ya watani walipofumua Simba bao 1-0 Juni 7, 1965.

Katika mchezo huo bao pekee la Yanga liliwekwa kimiani na Mawazo Shomvi kabla ya pambano kuvunjika dakika ya 80 na kugoma kurudiana na watani wao waliokuja kupewa ubingwa mwaka huo wa kwanza kwa kuasisiwa kwa Ligi ya Bara.

Pia kama hujui ni Yanga haohao iliyokuwa ya kwanza kutoa kipigo kikali katika mechi ya watani kwa kuifunga Simba mabao 5-0 katika mchezo uliopigwa Juni 1, 1968.

Mabao ya Yanga yaliwekwa kimiani na Maulid Dilunga na Saleh Zimbwe waliyefunga mawili kila mmoja na Kitwana Manara ‘Popat’.

Hata hivyo ni Yanga hao hao waliokuja kuandikia historia ya aibu kwa kufumuliwa mabao 6-0 na watani wao Julai 19, 1977 ikiwa sasa imetimia miaka 46 inaahaha kufuta aibu hiyo bila mafanikio.

Aidha Yanga ndio klabu ya kwanza nchini kunyakua ubingwa wa nchi mara tano mfululizo ikifanya hivyo miaka ya  1968-72, japo Simba nayo ilikuja kufanya hivyo baadaye kati ya 1976-80 na misimu minne iliyopita ilibeba mara mfululizo.

Lakini ni Yanga tena waliandika rekodi ambayo mpaka leo haijawahi kufikiwa na timu yoyote katika Ligi Kuu ikiwamo Simba kwa kutwaa mataji mara tatu tatu mfululizo katika vipindi vitatu.

Ilitwaa mara tatu mfululizo kwa mara ya kwanza mwaka 1991-93 kisha ikarudia tena 1996-98 na 2007-2010, ingawa Simba ilijibu misimu minne mfululizo kulitwa taji hilo kabla ya msimu uliomalizika Juni 29, Yanga kuwazidi akili.

Hata hivyo Simba misimu nne mfululizo iliyopita ilitwaa taji hilo kabla ya Yanga kuwanyang’anya kwa misimu miwili ikibeba pia ASFC na Ngao ya Jamii.

Mbali na kubeba mataji mengi ya Ligi Kuu, Yanga pia inashikilia rekodi kadhaa za kubeba mataji mengine mbalimbali ikiwamo ya michuano ya Ligi Kuu ya Muungano (sasa haipo, iliyoshirikisha timu za Bara na Zanzibar).

Imetwaa michuano ya Kombe la FA/ASFC mara tisa ikiwa ni rekodi ikifanya hivyo 1967, 1974, 1999, 2001, 2015-16, 2021-22, 2022-23, 2023-24 na 24-25), Kombe la Nyerere, Kombe la Tusker, Kombe la CCM, Kombe la Hedex mbali na kubeba pia Ngao ya Jamii mara nane ikiwa nyuma ya Simba iliyotwaa mara tisa.