Leo Septemba 12 ndiyo kilele cha tamasha la saba la Yanga lijulikanalo kama ‘Wiki ya Mwananchi’ litakalofanyika katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Katika kila kilele cha Wiki ya Mwananchi, Yanga hucheza mechi ya kimataifa ya kirafiki na timu kutoka nje ya Tanzania na safari hii itakabiliana na Bandari FC ya Kenya.
Yanga imekuwa na historia ya kufanya vizuri katika mechi hizo za kilele cha Wiki ya Mwananchi na leo tunakuletea nyota waliogeuka lulu katika tamasha hilo kutokana na uwezo na ubora waliouonyesha kwenye mechi husika.
Timu ya wananchi ambayo ni mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara msimu wa 2025/26, wamefanya sajili za nyota wengi ambao watakuwa sehemu ya kutoa burudani kwa mashabiki watakaojitokeza kwenye tamasha hili na baadhi ambo ni Andy Boyeli, Celestin Ecua, Balla Moussa Conte, Mohammed Hussen ‘Tshabalala’. Swali ni je, nani atakuwa nyota wa tamasha katika orodha hii.
Hili lilikuwa pambano la kwanza la ‘Wiki ya Mwananchi’ kwa Yanga na ilicheza mchezo na Kariobang Sharks ya Kenya.
Katika mchezo huu uliopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa timu hizo zilitoka sare ya bao 1-1 na Kariobang ilipata bao la utangulizi dakika ya 49 lililofungwa na Patrick Otieno kisha dakika sita mbele, Patrick Sibomana aliisawazishia Yanga kwa penalti.
Sibomana ulikuwa ni usajili mpya na alikuwa mshambuliaji kiongozi wa Yanga kwa msimu huo kutokana na mchezo huo wananchi waliamini wamepata jembe na aliitumikia kwa msimu huo na baadae kuachwa na timu hiyo.
Yanga ikionekana timu tishio, ilicheza mechi ya pili dhidi ya Aigle Noir kutoka Burundi na kuibuka na ushindi wa mabao 2-0.
Winga Tuisila aliibuka nyota wa mchezo kwa mashabiki wa timu hiyo kutokana na aina ya uchezaji wake akiwakimbiza mabeki wa timu pinzani na alitupia bao kwenye mchezo huo.
Mabao kwenye mchezo huo yalifungwa na Mghana, Michael Sarpong katika dakika ya 59 kwa kichwa kutokana na krosi ya Ditram Nchimbi huku la pili likifungwa na winga Kisinda ‘TK Master’.
Baada ya ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Aigle Noir, msimu uliofuatia Yanga ikaduwazwa kwa kuchapwa 2-1, dhidi ya Zanaco ya Zambia.
Tambasha hili ndilo liliibua ushangiliaji wa aliyekuwa mshambuliaji wa timu hiyo ambaye atakipiga Namungo msimu ujao Makambo, kwa kuwajaza mashabiki kwa kupiga makofi.
Makambo alianza kuifungia Yanga bao la utangulizi dakika ya 30 ya mchezo baada ya kupokea pasi ya Feisal Salum ‘Fei Toto’.
Zanaco ilisawazisha kupitia kwa Ackim Mumba dakika ya 60, kisha Kelvin Kapumbu akaipatia bao la ushindi dakika ya 76.
Agosti 6, 2022, Yanga ilifanya vibaya tena katika sherehe hizo baada ya kukubali kichapo cha mabao 2-0 kutoka kwa Vipers ya Uganda.
Mabao ya Vipers katika mechi hiyo yalifungwa na viungo, Milton Karisa na Anukani Bright.
Licha ya Yanga kufungwa na timu hiyo mashabiki wa timu hiyo walifurahishwa na aina ya uchezaji kwa baadhi ya wachezaji wao huku Morrison akiwa sehemu yao pamoja na kwamba alianzia benchi lakini aliwapa burudani.
Hili ndilo tamasha la mwisho lililofanyika Julai 22, 2023 na bao la Mzambia, Kennedy Musonda lilitosha kuipa timu hiyo ushindi wa pili baada ya ule wa mabao 2-0, dhidi ya Aigle Noir kutoka Burundi, mchezo uliopigwa Agosti 30, 2020.
Tamasha hili lilinogeshwa na mastaa wengi huku na aliyeteka hisia za mashabiki ni aliyekuwa kiungo mshambuliaji wa timu hiyo, Mahlatsi Makudubela ‘Skudu’ aliyesajiliwa akitokea Marumo Gallants ya kwao Afrika Kusini.
Yanga iliingia katika mchezo huo ikiwa na kocha mpya Muargentina, Miguel Gamondi aliyetambulishwa Juni 24, 2023 kuchukua nafasi ya Nasreddine Nabi aliyejiunga na FAR Rabat ya Morocco.
Msimu huo licha ya kikosi hicho kuwa na nyota wengi wenye ubora Pacome Zouzoua aliibuka kinara kutokana na uwezo mkubwa aliouonyesha na kuwa gumzo kwa mashabiki.
Walikuwapo Clatous Chama, Stephane Aziz Ki alianzia benchi, Duke Abuya, Maxi Nzengeli na Prince Dubenyota wa mchezo akawa Pacome na ndiye aliyetambulishwa wa mwisho wakati wa utambulisho wa nyota wa kikosi cha timu hiyo.
Kwenye mchezo huo, Yanga iliibuka na ushindi wa mabao 2-1 bao la utangulizi kutoka kwa wapinzani lilifungwa kipindi cha kwanza huku mabao mawili ya Yanga yakiwekwa kambani na Mudathir Yahya na Stephane Aziz Ki aliyekwamisha mpira nyavuni kwa mkwaju wa penalti.