Mastaa Yanga wampa presha kocha Angola

WALE wapinzani wa Yanga, Waliete Benguela, wanaendelea kujipanga kabla ya kukutana na Yanga Septemba 19, lakini kocha mpya wa kikosi hicho amewataja mastaa wawili ambao wanampa presha.

Yanga ikimaliza sherehe za kilele cha wiki ya Mwananchi, itakuwa na akili ya kujipanga kwenda kukutana na Simba, kwenye mchezo wa ngao ya jamii, utakaopigwa Septemba 16, 2025.

Baada ya mchezo huo Yanga itakuwa na hesabu kubwa siku nne kwenda kukutana na Waliete, ugenini kwenye mchezo wa kwanza wa mtoano wa Ligi ya Mabingwa Afrika.

Kocha wa Waliete Bruno Ferry alizungumza na Mwanaspoti kwa njia ya simu kuwa, mchezo dhidi ya Yanga hauwezi kuwa rahisi kutokana na ubora wa wapinzani wao.

Ferry alisema, amewaambia mabosi na wachezaji wake, wanatakiwa kujipanga sawasawa na kama wanataka ushindi lazima wawe tayari kwenda kuwazuia mastaa wa timu hiyo kama Pacome Zouzoua na Clement Mzize.

“Tunaendelea na maandalizi, unaona muda siyo rafiki sana lakini tunazidi kuimarika taratibu, kama unavyojua tunaanzia nyumbani sehemu ambayo lazima tuhakikishe tunatumia hiyo nafasi kutengeneza ushindi,” alisema Ferry.

“Kwenda kukutana na timu kama Yanga hiyo ni ratiba inayohitaji tuweke nguvu kubwa, nilikwambia viongozi na hata wachezaji hii ni timu kubwa yenye wachezaji wenye uzoefu.

“Unapotaka kushinda mbele ya Yanga unatakiwa kuwa tayari zaidi yao, lakini uweze kuwazuia wachezaji wao Bora kama Zouzoua (Pacome), Mzize (Clement), hata yule Dube (Prince.

Aidha Ferry ambaye ni kocha msaidizi wa zamani wa Azam ilipokuwa chini ya Msenegali Yusuf Dabo, alisema bahati nzuri kwao kuna wachezaji wengine bora ambao wapinzani wao wamewapoteza huku akiendelea kutafuta taarifa za wachezaji wapya wa Mabingwa hao wa Tanzania

“Bahati nzuri kwetu wapo wachezaji Bora wamepungua Yanga kama Aziz KI (Stephanie), Aucho (Khalid) nawajua wakati nikiwa hapo Tanzania.

“Hatuwezi kulala kwa kuwa hawapo, najua wapo wachezaji bora wengine wamewaongeza tunaendelea kuwatafuta tuwajue na tuijue timu yao zaidi.”

Yanga itaanzia ugenini Angola, mchezo wa kwanza ukipangwa kupigwa Septemba 19 na wiki moja baadaye mchezo huo utarudiwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam.