Dar es Salaam. Kesi ya Bernardo Sepeku ambaye ni mtoto wa marehemu John Sepeku aliyekuwa Askofu wa kwanza wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Dayosisi ya Dar es Salaam, inaendelea leo Ijumaa, Septemba 12, 2025 Mahakama Kuu, Divisheni ya Ardhi.
Bernardo amefungua kesi Mahakama hapo, akipinga kunyang’anywa zawadi ya kiwanja alichopewa baba yake mwaka 1978 na kanisa hilo.
Amefungua kesi hiyo ya ardhi ys mwaka 2023, dhidi ya Bodi ya Wadhamini wa Kanisa Anglikana Tanzania, Askofu Jackson Sostenes wa Dayosisi ya Dar es Salaam pamoja na Kampuni ya Xinrong Plastic Waste Industry Co Ltd.
Katika madai yake, pamoja na mambo mengine anaomba alipwe Sh3.72 bilioni ambayo ni fidia ya hasara ya kifedha iliyopatikana kutokana na uvamizi wa ardhi katika kiwanja hicho.
Kesi hiyo imepangwa kusikilizwa leo Ijumaa Septemba 12, 2025 mbele ya Jaji Arafa Msafiri anayesiliza shauri hilo, ambapo mashahidi wa upande wa wajibu maombi watatoa ushahidi wao dhidi ya Sepeku.
Sepeku anatetewa na mawakili wawili ambao ni Deogratias Butawantemi na Gwamaka Sekela, huku wajibu maombi wakitetewa na wakili Dennis Malamba.
Tayari mashahidi wanne wa wajibu maombi wameshatoa ushahidi mahakamani hapo.
Miongoni mwao ni Katibu wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Mchungaji George Lawi, Askofu Johnson Chinyong’ole (63) wa Dayosisi ya Shinyanga na Askofu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Central Tanganyika (Dodoma), Dk Dickson Chilongani(59).
Katika utetezi wake, Askofu Chinyong’ole alidai kikao cha Sinodi sio chombo cha kutoa zawadi kwa sababu hakina mamlaka na hata zawadi ya kiwanja aliyopewa marehemu Sepeku, haikufuata taratibu, licha ya kukiri kikao hicho ndicho chombo cha mwisho cha kutoa uamuzi ambao hauwezi kupingwa na vikao vingine vya kanisa.
Hata hivyo, alipohojiwa na wakili Gwamaka Sekela na Deogratias Butawantemi wa mleta maombi katika shauri hilo kuhusu utaratibu uliotakiwa kufuatwa ili Sepeku apewe zawadi hiyo, shahidi huyo alishindwa kufafanua.
Vilevile katika utetezi wake Askofu Chilingano, alidai alijisikia furaha na huzuni, Askofu Mkuu wa Kwanza wa kanisa hilo, marehemu John Sepeku alipopewa zawadi ya shamba na nyumba.
Dk Chilongani ambaye pia alishawahi kuwa Katibu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania kuanzia mwaka 2010 hadi mwaka 2013, alidai Novemba 23, 2014 aliteuliwa kuwa Askofu wa Dayosisi ya Dodoma nafasi ambayo anaitumikia mpaka sasa.
Alidai kikao cha Sinodi kina nguvu katika imani na utawala, lakini hakina nguvu katika masuala ya kutoa mali au zawadi.
Alidai hata utaratibu uliotumika kumpa zawadi Askofu Sepuku haukufuata sheria na taratibu kwa kuwa Bodi ya Wadhamini wa Kanisa hilo, haikuwa na kikao cha kuidhinisha zawadi hiyo.
Alidai ili mali itolewa na bodi ya wadhamini hao ni lazima wakae kikao ndipo watoe.
Dk Chilongani alidai bodi ya wadhamini ina uwezo wa kupinga uamuzi uliofanywa na kikao cha Sinodi, na Sinodi nayo ina uwezo wa kupinga uamuzi uliotolewa na Bodi ya Wadhamini wa Kanisa la Anglikana.
Aliendelea kudai hata mgogooro huo wa ardhi baina ya Bernardo Sepetu dhidi ya wadhamini wa bodi hiyo, ameufahamu miaka minne iliyopita baada ya kufunguliwa kwa kesi mahakamani.
Katika ushahidi wa upande wa madai uliotolewa na mashahidi mbalimbali wakiwemo wajumbe wa Bodi ya Wadhamini na maaskofu wengine wa kanisa hilo, akiwemo Askofu Oscar Mnung’a alidai Askofu Sepeku alipewa zawadi hiyo na Dayosisi ya Dar es Salaam mwaka 1980.
Pendekezo la kumzawadia Askofu Sepeku shamba na nyumba lilitolewa awali na Kamati ya Kudumu ya Kanisa hilo Dayosisi ya Dar es Salaam katika kikao chake cha Desemba 8, 1978.
Sinodi ya Dayosisi hiyo katika kikao chake cha Machi 8 na 9, 1980 iliridhia na kuazimia kumpatia Askofu Sepeku zawadi ya ardhi, shamba la eka 20 lililoko Buza wilayani Temeke, Dar es Salaam na nyumba eneo la Kichwere, Buguruni, wilayani Ilala, Dar es Salaam.
Hata hivyo, Askofu Chilongani ambaye pia ni Askofu Mkuu Msaidizi, alikana kutambua shamba na nyumba hiyo kutolewa kwa Askofu Sepeku kama zawadi kwa madai zawadi hiyo haikufuata sheria na kanuni, japokuwa amekiri katiba ya mwaka 1970 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2004, sura ya 10 inaeleza Mamlaka ya wadhamini wa bodi ya kanisa hilo ni kutunza mali za dayosisi.
Endelea kufuatilia Mwananchi kujua kitakachojiri mahakamani