Dar es Salaam. Bonny Sagati ni kijana mwendesha bodaboda anayefanya shughuli zake maeneo ya Tegeta mkoani Dar es Salaam.
Aghalabu siku yake inaanza mapema mno, kabla hata jogoo hajawika. Akiwa bado na usingizi mzito, anapiga mswaki kwa haraka, anakunjua suruali yake iliyochakaa na kuivaa pamoja na jaketi ambalo halijui lini liliona maji!
Saa chache baadaye, anaegesha chombo mahala anatafuta kinywaji pendwa kwa vijana cha kuongeza nguvu maarufu ‘energy’.
Hapo hajala staftahi na anapolazimika kufanya hivyo, Bonny atatafuta kikombe cha chai yenye sukari tele na maandazi. Kama tayari alishapata senti za maana asubuhi hiyo atakunywa na supu iliyojaa mafuta, pilipili na chumvi nyingi kwenye sahani. Hiki ndicho chakula anachoanzia kila siku.
Pikipiki yake ndiyo maisha yake. Bonny hubeba abiria, mizigo, hajali anachobeba hata mbuzi hana ajizi kumbeba madhali anaingiza pesa mfukoni!
Wakati jua linawaka, jasho humtiririka mgongoni, lakini bado anasukuma gurudumu akiamini ule msemo “mwendesha bodaboda bila jasho, hana kesho.” Mchana ikifika, chakula chake cha mchana huwa wali maharage au chipsi mayai, akishushia kwa soda baridi katika vibanda vya mama ntilie ambavyo vingi usafi wake umo shakani.
Mara nyingine akipata hela ya haraka, hujitoma kwenye mgahawa wenye afadhali, akijipa nyama choma na bia mbili, akisema moyoni mwake” “mwili nao unataka starehe.”
Usiku ukifika, Bonny lazima achangamane na marafiki zake kijiweni au kwenye duka la pombe. Hapo ndipo vilevi huchukua nafasi.
Ataanza na bia ikifuatwa na pombe kali za bei chee maarufu kwao kama ‘visungura’ sambamba na supu ya pweza.
Hapa watacheka, wakisahau machovu ya siku. Siku nyingine fedha alizovuna huisha hapohapo,
Akiwa hapo ndipo Bonny atakapoumwa sikio kuwa mzigo mpya wa ‘energy umeingia mjini. Bila hata ya kuuujua undani wake kama vile kusoma maelezo ya viambata vya bidhaa hiyo mpya, atafakamia kinywaji akipoza roho.
Katika maisha yake Bonny hajui kinachoitwa maelezo ya onyo yaliyo kwenye vifungashio vya bidhaa anazotumia kama chakula kama pengine bidhaa husika zina chumvi nyingi, sukari au mafuta yaliyozidi kiwango.
Kwake ladha ya chakula ndio kila kitu, ndio maana leo anaposikia kuna bidhaa mpya sokoni ya kuongeza nguvu, haulizi mara mbili. Anafakamia!
Lakini hata kama angejihimu kusoma maelezo hayo ya onyo, Bonny wa watu atajua wapi maana ya maneno ya kimombo ya PH, Calcium, Chloride na mengineyo yaliyomo kwenye maelezo ya mbele ya bidhaa?
Usiku ukiwa mwingi, Bonny hurudi nyumbani usiku wa manane, akiangukia kitandani bila hata kuoga. Huyu ndiye Bonny boda boda. Huu ndio mtindo wake wa maisha siku saba kwa wiki, siku 30 kwa mwezi.
Kile Bonny asichokijua ni kwamba mtindo wa maisha yake wa ulaji wa vyakula vya mafuta, pombe na vinywaji vya kuongeza nguvu kila siku, sambamba na milo isiyo kamili, huku akikosa mazoezi, unamwandalia kaburi taratibu.
Moyo wake unachoka, ini linabeba mzigo, na sukari inapenya bila yeye kujua. Anadhani anabeba maisha, kumbe maisha ndiyo yanambeba taratibu kuelekea hatari ya magonjwa na kifo kisicho na hodi.
Bonny hayuko peke yake, ni kielelezo cha maelfu ya vijana wa bodaaboda nchini walio kwenye hatari kubwa sio tu ya kupata ajali za barabarani kama ilivyozoeleka, bali kufikwa na magonjwa yasiyoambukiza kama shinikizo la damu, kisukari, matatizo ya figo na moyo na mengineyo ambayo ni sawa na wauaji wa kimyakimya.
Shirika la Afya Duniani (WHO) linaeleza kuwa magonjwa haya yanachukua nafasi ya kwanza duniani kwa kuua watu.
Inakadiriwa kuwa watu milioni 41 hufariki kila mwaka duniani kutokana na magonjwa haya sawa na asilimia 74 ya vifo vyote.
Kugharamia matibabu ya magonjwa haya, dunia kwa sasa inatumia zaidi ya Dola za Marekani trilioni mbili kwa mwaka.
Hapa nchini ukibainika figo zimefeli, uchujaji wa damu unagharimu sio chini ya Sh 150,000 kwa kila awamu ya uchujaji, na wastani wa awamu sio chini ya mara tatu kwa wiki.
Ni nani katika kundi la kina Bonny anayeweza kugharamia matibabu haya? Hiki ni kifo tena cha kujitakia.
Ili kuwaokoa kina Bonny waliotapakaa kila kona ya nchi na wananchi wengine kwa jumla, mipango na mikakati kabambe haina budi kufanywa na Serikali, wadau wa afya na lishe, familia na jamii kwa jumla katika kusisitiza mapambano dhidi ya magonjwa ya kuambukiza.
Mikakati hiyo inaweza kuwa elimu kwa umma, kampeni kwa jamii kuhusu haja ya kubadili mitindo ya kimaisha kama umuhimu wa kufanya mazoezi na kula milo kamili.
‘’Ni lazima tujenge uelewa wa watu kuhusu tabia bora za kiafya, ikiwemo kula vyakula bora, kufanya mazoezi na kuepuka matumizi ya pombe na sigara. Jamii zetu zinahitaji kupatiwa uelewa huu… ‘’ anasema Waziri wa Afya wa Zanzibar, Ahmed Nassor Mazrui.
Lakini mkakati mwingine ni uundwaji wa sera au miongozo inayosisitiza bidhaa za chakula kuwa na alama a u taarifa za onyo kwenye vifungashio. maarufu Kiingereza kama Front of Pack Labelling’ (FOPL).
Lengo la alama au taarifa hizi ni kumrahisishia mlaji kufanya uamuzi wa haraka na sahihi kuhusu ubora wa chakula anachonunua na kula.
Taarifa hii ya lishe inayoonyesha viambata vilivyomo kwenye chakula inapaswa kuwa fupi na iwekwe kwa namna rahisi kueleweka, mara nyingi kwa kutumia alama za rangi, alama za nyota, au nembo maalum.
Magonjwa yasiyoambukiza yanachochewa zaidi na ulaji usiofaa wa vyakula vyenye mafuta mengi, chumvi nyingi, sukari kupita kiasi na nishati nyingi.
Taarifa hizi zina uhusiano wa karibu na magonjwa haya kwa kuwa huonya mlaji endapo chakula kimejaa sukari, chumvi au mafuta, ambavyo ni vihatarishi vikuu vya magonjwa haya.
Ni taarifa zinazomsaidia mnunuzi. Kwa mfano, mtu akiwa dukani anaweza kuchagua soda yenye sukari kidogo au siagi yenye mafuta kidogo kwa kuangalia alama za mbele ya pakiti.
Kubwa zaidi kadri watu wanavyozidi kuelewa alama hizi, ndivyo jamii inavyopunguza ununuzi wa vyakula visivyo na afya na hivyo kupunguza mzigo wa magonjwa ya kuambukiza.
“Magonjwa yasiyoambukiza ni changamoto kubwa ya karne hii… Alama za tahadhari mbele ya kifurushi ni njia madhubuti za afya ya umma zinazopaswa kutumika,’’ anasema mjumbe maalum wa zamani wa Umoja wa Mataifa kuhusu afya, Dainius Pūras.