Watu 33,000 hufariki kila mwaka kuvuta hewa chafu

Dar es Salaam. Kwa Tanzania watu takribani 33, 000 hufariki dunia kwa mwaka kutokana na magonjwa ya mfumo wa kupumua ambayo huchangiwa na uvutaji wa moshi unaotokana na matumizi ya nishati ya kupikia isiyosafi.

Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mkuu Wizara ya Nishati Mhandisi Felchesmi Mramba leo Ijumaa Septemba 12, 2025 wakati akizungumza kwenye Jukwaa la Nishati Safi ya Kupikia 2025 lililoandaliwa na Kampuni ya Mwananchi Communications Ltd kwa kushirikiana na Wizara ya Nishati.

“Mama anaweza kuwa anapika na mtoto wake mgongoni au jirani yake anapika katika mazingira ya moshi kwa miaka mingi, ile athari ya moshi inaathiri miili yao taratibu. Kwa sababu ya athari hizo ndipo Serikali imekuja na mkakati wa kitaifa wa matumizi ya nishati safi ya kupikia wa miaka kumi,” amesema Mramba.



Kinachoendelea Mlimani City kongamano la Nisha safi

Mhandisi Mramba amesema ni lazima elimu iendelee kutolewa kwa jamii na nguvu ya pamoja inahitajika ili watu waendelee kuhama kutoka kutumia nishati isiyosafi kuanza kutumia nishati safi.

Mwananchi Communications Limited (MCL) imesema kaulimbiu ya mwaka huu ya “Nishati Safi ya Kupikia, Okoa Maisha na Mazingira” inalenga kusisitiza kuwa matumizi ya nishati hiyo si suala la kiteknolojia pekee, bali ni njia ya kuokoa maisha, kulinda afya na kuhifadhi mazingira.

Hayo yameelezwa leo na Mkurugenzi Mtendaji wa MCL. Rosalynn Mndolwa-Mworia wakati wa kufungua kongamano la Nishati Safi ya Kupikia 2025 linaloendelea katika ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam.

Rosalynn amesema zaidi ya asilimia 80 ya Watanzania bado hutegemea kuni na mkaa kwa ajili ya kupikia, hali inayosababisha madhara makubwa ya kiafya, kuongeza uharibifu wa mazingira na kudhoofisha uchumi.

“Hata hivyo, mabadiliko chanya yameanza kuonekana kupitia jitihada za pamoja kati ya Serikali, sekta binafsi na wadau wa maendeleo,” amesema Mndolwa-Mworia.

Rosalynn ametoa wito kwa washirika wa maendeleo na wafadhili kuongeza ushirikiano na ufadhili endelevu, akibainisha kuwa kupitia majukwaa ya habari ya MCL, uwekezaji wao unaweza kusaidia kufikisha suluhu za nishati safi vijijini na kuifanya ajenda hiyo kuwa kipaumbele cha kitaifa.

Serikali imeipongeza Kampuni ya Mwananchi Communications Ltd (MCL) inayochapisha magazeti ya Mwananchi, The Citizen, Mwanaspoti na majukwaa yake ya mitandao ya kijamii kwa kubuni Jukwaa la Nishati Safi ya Kupikia 2025 ambalo ni shirikishi.

Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba, amesema jukwaa hilo limewakutanisha wadau mbalimbali kwa ajili ya kujadili na kuja na mikakati ya kusukuma mbele jitihada za Serikali kufanikisha ajenda ya matumizi ya nishati safi.

Mhandisi Mramba ameyasema hayo leo wakati wa Jukwaa la Nishati Safi ya Kupikia 2025 lililoandaliwa na MCL kwa kushirikiana na Wizara ya Nishati.

Jukwaa hilo ni sehemu ya kuwaleta pamoja wadau wa nishati safi ya kupikia ili kutoa elimu kwa Watanzania kuhusu umuhimu wa matumizi ya nishati safi ikiwemo gesi na umeme hivyo, kuachana na matumizi ya kuni na mkaa ambayo imekuwa na athari kubwa kwa afya za watumiaji.

Mkakati wa Serikali ni kuhakikisha ifikapo mwaka 2034 asilimia 80 ya Watanzania wawe wanatumia nishati safi ya kupikia.

Matumizi ya nishati isiyosafi yanaenda yanapungua nchini huku nishati kama kuni na mkaa ikianza kuwa vigumu kupatikana ikilinganishwa na zamani.

Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Felchesmi Mramba leo katika Jukwaa la Nishati Safi ya Kupikia 2025 lililoandaliwa na kampuni ya Mwananchi Communications Ltd kwa kushirikiana na Wizara ya Nishati.

Lengo la Serikali ni ifikapo mwaka 2034 Watanzania wanne kati ya watano watumie nishati safi ya kupikia, ikiwemo umeme na gesi hivyo kuachana na nishati isiyosafi kama kuni na mkaa ambazo zina athari kubwa za kiafya na mazingira.

“Tanzania takriban asilimia 80 ya kaya zetu bado zinategemea nishati za jadi za kuni na mkaa na wote tutakubaliana idadi hiyo ni kubwa na kwa pamoja tunahitaji kufanya kitu kurekebisha hali hiyo.

 “Hali hii inawaweka watu katika hatari ya kiafya kuchochea ukataji miti hovyo na mzigo mkubwa wa kiuchumi, hasa kwa wanawake na watoto,” amesema Mramba.

Hata hivyo, Mramba amesema upatikanaji wa kuni na mkaa kwa sasa ni changamoto kubwa ikilinganishwa na zamani.

Amesema hilo linafanya suala la kuhama kutoka kwenye nishati chafu kwenda safi kuwa muhimu na umuhimu wake unatokana na ugumu wa kupatikana kwa kuni na mkaa.

“Kwa upande wa mijini hali inazidi kuwa ngumu zaidi, gharama ya kuni na mkaa inazidi kupaa, bei zinazidi kupanda na kuna sehemu bei hazihimiliki.

“Kwa vijijini wananchi wanatumia muda mwingi kutafuta kuni na mkaa na wanapoteza muda wao wa uzalishaji,” amebainisha.

Vikwazo matumizi nishati safi

Imeelezwa kuwa mahitaji ya gesi ya kupikia nchini Tanzania kwa mwezi ni futi za ujazo 30,000 huku uwezo wa Bandari katika kupokea gesi kwa sasa ni mdogo.

Hayo yameelezwa na Mratibu wa Kitaifa wa Wanawake kwenye LPG, Winners Lukumay aliyeomba Serikali kuhakikisha inaendelea kuboresha bandari nchini ili kurahisisha uingizaji wa gesi ya kupikia jambo linaloweza kuchangia kushusha gharama za nishati hiyo.

Amesema hadi sasa bandari inaweza kupokea meli ya gesi yenye futi za ujazo 5,000 pekee kwa wakati mmoja wakati.

“Hii inamaanisha kuwa meli sita zinapaswa kuingia kwa mwezi ili kukidhi mahitaji kama nchi. Tukiboresha bandari hata gharama za usafirishaji ambazo zinaongeza gharama ya gesi kwa mlaji wa mwisho zitapungua” amesema wakati akizungumza leo kwenye Kongamano la Nishati safi ya kupikia lililoandaliwa na Kampuni ya Mwananchi Communication Limited (MCL) kwa kushirikiana na Wizara ya Nishati likiwa na kauli mbiu ya Nishati Safi ya Kupikia: Okoa Maisha, Linda Mazingira.

Winners amesema changamoto nyingine ambayo bado inafifisha jitihada za matumizi ya nishati safi ya kupikia ni kukosekana kwa elimu ya fedha.

Alitolea mfano wa mamalishe ambao anasema hawana shida ya kulipia gesi kwa sababu ni wafanyabiashara wenye uwezo wa kuingiza hadi Sh150,000 kwa siku, lakini wanakosa elimu ya fedha inayoweza kumfanya ashindwe kununua gesi kwa wakati mmoja.

“Huyu mamantilie yuko radhi anununue mkaa wa Sh3,000 kila siku, lakini je tuna mpango maalumu ambao utamuwezesha huyu mama kununua gesi kidogo kidogo,” amesema.

Eneo lingine alilogusia ni watumiaji wengi kushindwa kupata majiko kulingana na mahitaji yao kwani, yale yanayogawiwa na Wakala wa Umeme Vijijini (Rea) hayakidhi mahitaji hivyo, wanapogawiwa majiko wanaweka pembeni au wanakwenda nayo nyumbani bila kuyatumia.

“Ni vyema kutengeneza majiko yanayoendana na majitaji ya watumiaji. Pia watu wa nyumbani hawana ujuzi wa matumizi ya nishati safi ya kupikia mbali na gharama,” amesema.

Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) imeanza kutoa elimu juu ya matumizi ya nishati safi ya kupikia kuanzia shule za msingi ikiwa ni mkakati wa kuziba pengo la ukosefu ya elimu sahihi.

Hayo yameelezwa leo na Mkurugenzi wa Idara ya Nishati na Madini, Wizara ya Maji, Nishati na Madini Zanzibar, Said Mdungi wakati akizungumza kwenye Kongamano la Nishati Safi ya Kupikia lililoandaliwa na Kampuni ya Mwananchi Communication Limited (MCL) kwa kushirikiana na Wizara ya Nishati likiwa na kauli mbiu ya Nishati Safi ya Kupikia: Okoa Maisha, Linda Mazingira.

“Unapompa mtoto ujuzi atakwenda kushawishi nyumbani siku mzee wake akipata uwezo itakuwa ni rahisi kupata nishati safi ya kupikia. Mtoto huyu akikua na kuanza kujitegemea si rahisi kuchagua nishati za jadi bali ataendelea kutumia nishati safi ya kupikia,” amesema.

Mdungi amesema hatua hiyo itasaidia kujenga kizazi bora cha baadaye ambacho kitakuwa tayari kutumia na kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia.

Kuhusu wananchi kwenye maeneo mengine, Mdungi amesema kuwa wamekuwa wakipata elimu kwa njia mbalimbali ikiwemo vyombo vya habari sambamba na kuwafikia katika maeneo yao kwa kushirikiana na wadau ili kuwaelekeza athari za kutumia njia za kizamani katika kupika.

“Pia tumekuna na teknolojia ambazo mwananchi anaweza kutumia fedha kidogo kwa ajili ya kutumia nishati safi ya kupikia kama ambavyo angeweza kutumia kununua nishati nyingine,” amesema.

Uelewa, ushirikishwaji na gharama ya nishati safi ya kupikia ni miongoni mwa vikwazo vinavotajwa kuchangia vijana kutokutumia nishati safi ya kupikia.

Hayo yameelezwa na Mtaalamu wa masuala ya jinsia kutoka TANGSEN, Gaudensia Malongo wakati wa Kongamano la Nishati Safi ya Kupikia lililoandaliwa na Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) kwa kushirikiana na Wizara ya Nishati.

“Kuna vikwazo mbalimbali ambavo wanapata wanawake au vijana wadogo katika nishati safi ya kupikia. Moja ni suala la ushirikishwaji katika mipango ya kuhakikisha nishati safi inawafikia,” amesema.

Amesema ili kuondokana na kikwazo hicho suala la ushirikishwaji linapaswa kupewa kipaumbele zaidi ili kupata mawazo yao kuhusu mkakati mzima.

“Suala la gharama nalo ni changamoto kwa vijana, wanahitaji kutumia nishati hiyo ila kwa uwezo wao wa kifedha ni ngumu kidogo,” amesema na kuongeza: “hata uelewa bado ni mdogo jambo linawafanya wengi kuogopa kutumia nishati safi.”