Mtiririko wa usajili wa vyama vya siasa, tangu kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi Julai mosi 1992, utakuonyesha chama cha Demokrasia Makini ni cha 53 na namba yake ya usajili ni 00000053.
Vyama vingi vilivyowahi kupata usajili wa kudumu vimekuwa vikipepesuka na kupotea, Demokrasia Makini bado kipo.
Agosti 25, 2024, mkutano mkuu taifa wa chama hicho, uliofanyika ukumbi wa Hoteli ya Nefaland, Manzese, Dar es Salaam, kwa kauli moja, ulibadili jina la taasisi kutoka Demokrasia Makini hadi kuwa Chama cha Makini. Utambulisho wa chama hicho kwa kifupi ni Makini.
Kuelekea Uchaguzi Mkuu 2025, unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, Makini wamejitosa kuwania nafasi za uongozi wa dola. Rais, wabunge na madiwani. Anayebeba tiketi ya chama hicho katika mbio za urais ni Coaster Jimmy Kibonde.
Mbali na kuwania urais, Kibonde pia ndiye mwenyekiti taifa wa chama hicho.
Anasema amejitosa kugombea urais kwa sababu amejipima na anaona analo kusudi la kuwatumikia Watanzania. Anakishukuru chama chake kwa kumwamini na kumteua kupeperusha bendera.
Kibonde anasema anaamini siasa ni uchumi, kwa hiyo aliingia dimbani akiamini ni sehemu ya kujenga, kwani mtu anaweza kupata kipato na kujitengeneza kiuchumi. Kingine, anaeleza ukiwa mwanasiasa unakuwa mtumishi. Mambo hayo mawili ndiyo yalimfanya achague kuwa mwanasiasa na kushindania kuongoza dola.
Anasema aliingia kwenye siasa mwaka 1995 akiwa na umri wa miaka 17. Kishawishi kikiwa ni Naibu Waziri Mkuu wa zamani wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Augustino Mrema. Kibonde anasema kutokana na kuvutiwa na Mrema, ikawa sababu yeye kuingia kwenye ulingo wa siasa akiwa mdogo.
Kuelekea Uchaguzi Mkuu 1995, ambao ulikuwa wa kwanza wa vyama vingi vya siasa tangu Tanzania ipate uhuru, Mrema alihama Chama cha Mapinduzi (CCM) na kujiunga na NCCR-Mageuzi. Halafu, akawa mwenyekiti wa chama hicho. Kwa hatua hiyo, Kibonde alijiunga haraka na NCCR-Mageuzi.
Kibonde alikuwa akiishi Kijiji cha Mbalizi, Wilaya ya Mbeya Vijijini, mkoani Mbeya. Alijisajili kama mwanachama, akapokea kadi ya uanachama, kisha akachaguliwa kuwa mwenyekiti wa tawi la Mapelele la NCCR-Mageuzi, Mbalizi, licha ya kuwa na umri mdogo.
Mwaka 1997, alihamia Dar es Salaam, makazi yake yakawa Sinza, Mtaa wa Sinza D. Alipofika Dar, aliendelea kuwa mtiifu kwa chama chake, akiwa hana cheo chochote. Mwaka 1999, kufuatia mgogoro baina ya Mrema (mwenyekiti) na Katibu Mkuu, Mabere Marando, ilibidi Mrema afanye uamuzi wa kuhama chama. Alijiunga na Tanzania Labour Party (TLP).
Kama ulivyo msemo wa “ulipo tupo”, baada ya Mrema kujiunga na TLP, kisha kupitishwa kuwa mwenyekiti wa chama hicho, Kibonde naye alimfuata. Baada ya kupokea kadi ya TLP, hakikupita kitambo kirefu Kibonde alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa TLP, Kata ya Sinza. Hiyo ilikuwa mwaka 1999, alishikilia nafasi hiyo mpaka mwaka 2000.
Alipohamisha makazi yake kutoka Sinza hadi Mabibo, Dar es Salaam, cheo chake cha uenyekiti wa Kata ya Sinza ulikoma. Alibaki kuwa mwanachama wa kawaida, kabla ya kupitishwa na Mkutano Mkuu wa TLP jimbo la Ubungo, kuwa mjumbe wa Halmashauri Kuu Jimbo la Ubungo. Nafasi aliyodumu nayo kuazia mwaka 2000 hadi 2003.
Kisha, aliteuliwa kuwa mkuu wa idara ya usalama Mkoa wa Dar es Salaam wa chama hicho, mwaka 2003 mpaka 2004 na baadaye wadhifa huo ngazi ya taifa, mwaka 2004 – 2006. Kipindi hicho pia alikuwa mlinzi binafsi wa Mrema.
Uchaguzi Mkuu 2005, uliiacha TLP hoi. Chama hicho hakikupata wabunge wala kura za kutosha za ubunge, hivyo kukosa sifa ya kupata ruzuku. Kutokana na hali hiyo, chama kililazimika kuwaachisha kazi maofisa wengi, kwa kuwa hakukuwa na uwezo wa kuwalipa japo mishahara. Kibonde alikuwa mmoja wa waliopitiwa na fyekeo, hivyo akakaa pembeni.
Mwaka 2009, alijiunga na Demokrasia Makini, baada ya uongozi wake kumshawishi. Alipojiunga na chama hicho, aliteuliwa kukaimu nafasi ya katibu mwenezi taifa. Mwaka 2010, alichaguliwa na mkutano mkuu taifa kuendelea kushikilia nafasi hiyo ya katibu mwenezi. Alihudumia nafasi hiyo kwa miaka mitano.
Mwaka 2015, alichaguliwa kuwa naibu katibu mkuu Tanzania Bara. Alihudumu kwa miaka mitano, mwaka 2015 – 2020. Katika uchaguzi mkuu 2015, Kibonde aliwania ubunge Ubungo, kwa tiketi ya Makini.
Ulipofika mwaka 2020, aliweka nia ya kuwania uenyekiti wa chama hicho. Uamuzi huo, ulimwingiza kwenye mgogoro na aliyekuwa Mwenyekiti, Mohammed Abulla. Tofauti hiyo, ilisababisha Kibonde asihudhurie mkutano mkuu, matokeo yake alifukuzwa uanachama.
Abdulla, aligombea uenyekiti pekee akachaguliwa kuendelea kushikilia nafasi hiyo. Upande wa pili, Kibonde hakuridhishwa na uamuzi wa kumfuta uanachama, alikata rufaa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa. Alishinda rufaa akarejeshewa uanachama.
Aliporejea baada ya kushinda rufaa kwa Msajili, aliteuliwa kuwa kaimu katibu mwenezi. Desemba 20, 2021, mkutano wa halmashauri kuu taifa, ulimthibitisha Kibonde kuwa katibu mwenezi wa chama hicho.
Kutoka 2021 hadi 2023, ni miaka miwili ambayo ndani ya Makini, moshi ulikuwa ukifuka. Mgogoro wa uongozi ulishika kasi. Machi 17, 2023, mkutano wa halmashauri kuu taifa uliitishwa Zanzibar na uamuzi ukawa kumsimamisha uenyekiti Abdulla, kwa makosa ya kukiuka katiba ya chama.
Chama kilimpitisha Tabu Musa Juma kuwa kaimu mwenyekiti. Agosti 25, 2024, uliitishwa mkutano mkuu uliobeba kusudi la kusikiliza utetezi wa Abdulla kuhusu tuhuma dhidi yake, zilizosababisha asimamishwe uenyekiti.
Hata hivyo, Abdulla hakuhudhuria mkutano huo. Wajumbe wa mkutano mkuu wakaridhika na maelezo yaliyotumiwa na halmshauri kuu kumsimamisha uenyekiti, kwa kauli mojo waliridhia kumwondoa uenyekiti.
Kufukuzwa kwake kulifungua dirisha la kupatikana mwenyekiti mpya. Kibonde alijaza fomu kuomba kuwa mwenyekiti. Akawa mgombea pekee. Wajumbe halali ambao idadi yao ilikuwa 103, walimchagua wote.
Mei 17, 2025, ulifanyika mkutano mkuu ukumbi wa Mrina, uliopo Tip Top, Mnzese. Ajenda ilikuwa kumteua mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, vilevile mgombea urais wa Zanzibar. Awali, Kibonde alikuwa ameshatangaza nia na alichaguliwa kupeperusha bendera hiyo.
Kibonde anasema amejitosa kuwania urais wa Tanzania akiwa na mkazo katika maeneo matatu; elimu, kilimo na afya. Anasema, akiwa Rais, wanafunzi wote watasoma bure kwenye shule za Serikali na za umma, kuanzia ngazi ya awali mpaka chuo kikuu.
Anasema Serikali itawagharimia wanafunzi popote duniani, pale watakapokuwa wanakwenda kuchukua masomo ambayo yatakuwa na manufaa makubwa kwa nchi.
Kuhusu kilimo, anasema atatoa ekari tano kwa kila kijana wa Kitanzania atakayekuwa na umri kati ya miaka 21 mpaka 35. Mashamba hayo, vijana watapewa yakiwa na hatimiliki.
Anasema vijana wengi hawaamiki kwenye taasisi za kifedha. Hivyo, akiwapa ardhi na hatimiliki, itakuwa rahisi kuaminiwa na kukopeshwa fedha, ambazo zitawasaidia kujenga mitaji.
Anaeleza anakusudia kuanzisha viwanda vitakavyotengeneza pembejeo za kilimo kwa wingi. Kibonde anatamba akiwa Rais, wakulima hawatahangaika kupata pembejeo, badala yake pembejeo ndizo zitawangoja wakulima.
Eneo la afya, anasema atajenga hospitali kila kata, zikiwa na vifaatiba vya kutosha. Halafu kila Mtanzania atapewa bima ya afya, ambayo itaitwa Makini Care.
Ahadi nyingine eneo la afya ni mjamzito atatibiwa bure kuanzia anapoanza kliniki hadi anapojifungua. Kwa kujiamini, Kibonde anasema Serikali ya Makini haitageuza maiti kuwa chanzo cha mapato. Hakuna maiti itashikiliwa hospitalini.
Julai mosi, 1978, ndiyo tarehe Kibonde alizaliwa katika Hospitali ya Meta, mkoani Mbeya. Mama yake mzazi ni Hilda Mwakajumba na baba ni Jimmy Kibonde Mwakalobo. Mama yake bado yu hai, wakati baba yake alishapokea wito wa mauti.
Kibonde ni mtoto wa sita kati ya saba, kutoka kwa mama yake, wakati upande wa baba yeke ni mtoto wa 21 kati ya 25. Mwaka 1987 alianza darasa la kwanza Shule ya Msingi Majengo, Mbeya Mjini. Mwaka 1992, akiwa darasa la sita, alihamishiwa Shule ya Msingi Mbalizi 2, Mbeya Vijijini. mwaka 1993, alihitimu elimu ya msingi.
Mwaka 1994, aliendelea na kidato cha kwanza Shule ya Sekondari Mbalizi, Mbeya Vijijini. Alihitimu kidato cha nne mwaka 1997. Mwaka 1998 alijiunga Chuo cha Ufundi Rena, Mbeya, kusomea ufundi wa magari, mwaka 1999, alipohamia Dar es Salaam, alijiunga na Chuo cha Ufundi Stadi (Veta), alikoendelea na masomo ya ufundi wa magari.
Tangu alipopanda ngazi kuwa kiongozi wa kisiasa kitaifa, anasema amekuwa akipokea mafunzo kupitia kozi fupi, hivyo kumwimarisha na kumpa ari ya kujiamini kwamba akichaguliwa kuwa Rais, atakuwa na maarifa makubwa ya kiuongozi.
Kibonde ni mume na ana watoto watatu Jane, Jimmy na Hilda. Mkewe ni Zena Nzegula.